Tume ya uchaguzi yatoa mwaliko kwa taasisi na asasi za kiraia kutoa elimu kwenye uchaguzi mkuu wa 2020

Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania imetoa nafasi kwa taasisi au
asasi zenye nia ya kutoa elimu ya mpiga kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu
mwaka 2020 kuwasilisha maombi yao kwa tume hiyo.


Taarifa
iliyotolewa Novemba 22, 2019 na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Gerald
Mwanilwa imesema hatua hiyo inatokana na kifungu cha 4C cha sheria ya
taifa ya uchaguzi sura ya 343 kinaeleza Tume ina jukumu la kutoa elimu
ya mpiga kura nchi nzima, kuratibu na kusimamia watu wanaotoa elimu
hiyo.

Mwanilwa
amebainisha vigezo ni; taasisi au asasi itakayowasilisha maombi hayo
inatakiwa kuwa na usajili kwa mujibu wa sheria za taifa, iwe imefanya
kazi nchini si chini ya miezi sita tangu kusajiliwa kwake.

Vingine
ni; asasi au taasisi iwe haina taarifa ya kuvuruga amani au kuchochea
fujo ndani ya nchi na nchi nyingine, iwe tayari kujigharamia katika
kutoa elimu ya mpiga kura na watendaji wake wakuu watatu, wawili
wanapaswa kuwa Watanzania.

Kaimu
mkurugenzi huyo amesema maombi hayo yanatakiwa kuambatanishwa na cheti
cha usaili, katiba ya taasisi au asasi, majina ya viongozi wakuu wa
taasisi au asasi, anuani kamili ya makazi na ratiba kamili ya maeneo
wanayotarajia kutoa elimu kwa mpiga kura.