Tumieni uchaguzi huu wa serikali za mitaa kuwamwaga viongozi wenye sifa za hovyo


CCM Blog, Dodoma
Katibu
Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally  (pichani), ameziagiza Kamati za siasa za
wilaya, Kata na Matawi kutowateuwa wagombea wenye sifa za hovyo ikiwemo
kashfa za kuhujumu Ushirika, kuuza ardhi za wananchi na wenye mwenendo
usioaminika kwenye jamii.



Taarifa
ya Makao Mkuu ya CCM Dodoma, imesema agizo hilo amelitoa leo Oktoba 12,
2019, wakati akizungumza katika mkutano wa ndani wa wenyeviti wa
mashina, viongozi wa CCM na serikali ngazi zote za  Mkoa, wilaya, kata
na matawi, katika Wilayani Liwale mkoani Lindi.



“Tukitaka
kuzuia viongozi wababaishaji, Kangomba, Obutura, wadhulumaji wa ardhi,
tuwe makini kwenye uchaguzi huu, kama kuna kiongozi aliwahi kuuza ardhi
kwa kuwaibia wananchi, asiteuliwe na vikao vya CCM, na kama akihonga
akapitishwa, wananchi msimchgue mtu huyo na sisi tutashughulika na
waliomteua.” Taarifa hiyo imemkari Dk. Bashiru akisema na kuongeza;



“CCM
haiingii kwenye uchaguzi ili tu kushinda na kupata viongozi, ila
inaingia ili ishinde na ipate viongozi bora watakao wahudumia wananchi,
kwa kuwa imeahidi kuwatumikia wananchi kwa haki”.



Katibu
Mkuu amewataka wana-CCM watakao shindwa kwa namana yoyote kwenye kura
za maoni kutosusa kwa hasira na kwenda vyama vingine kwa kwa sababu
awamu hii Chama kitaweka nguvu zaidi eneo ambalo mwana CCM amehama na
kwenda kugombea upinzani, hivyo, CCM itamshinda naye atakufa kisiasa.



Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, ameelekeza kuwa mwana-CCM yeyote atakayeshindwa
kwenye kura za maoni kwa hujuma, atulie na kushirikiana na aliyeshinda,
baada ya uchaguzi atasikilizwa na waliohusika na hujuma watawajibishwa
kwa mujibu wa katiba na kanuni za Chama.



Pia
Katibu Mkuu amesikiliza na kutolea maelekezo  kero mbalimbali za
wananchi ikiwemo migogoro ya ardhi, ndoa, huduma za kijamii na kuagiza
viongozi wa serikali ngazi za wilaya kuzishughulikia kwa kuwa nyingi
zilitakiwa kuishia huko.



 Ametumia fursa hiyo, kusisitiza viongozi kusikiliza changamoto za watu na kuzitafutia majawabu.


Taarifa
imesema ziara hiyo ya Kativu Mkuu wa CCM ni sehemu ya muendelezo wa
utekelezaji wa maelekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya  kwa
viongozi kuendelea kuwa karibu na wananchi, kuwasikiliza na
kushughulikia changamoto zao.