Tundu ainusa tanzania… yupo kenya sasa

Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki 
Tundu Lissu yupo nchini Kenya, akisubiri ‘amri’ ya kuingia nchini endapo
atahakikishiwa usalama wake.

Akizungumza na kituo cha Televisheni cha
KTN nchini Kenya jana tarehe 28 Novemba 2019, Lissu amesema amepona
lakini hali ya usalama wake bado si shwari.

“Bado kuna vitisho vya aina hii, lazima
watu wenye busara wakae na kuangalia namna nzuri ya kufanya ili niweze
kurudi nyumbani,” amesema Lissu.
Amemweleza mwandishi wa kituo hicho,
kwamba kuna watu ambao wasingependa kuona akirudi na siku moja baadaye
anapigwa risasi tena.

Lissu amesema “nafikiri hakuna mtu anayetaka kuona narudi nyumbani na keshokutwa ninapigwa risasi tena.”

Hata hivyo amesema, bado jitihada zinafanywa na ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha ataporejea kunakuwa na usalama wa kutosha.

Amesisitiza, hataki kuishi nje ya Tanzania kwa kuwa, alikwenda kwa ajili ya matibabu na sasa matibabu hayo yamekwisha

“Mimi sitaki kabisa kuishi uhamishoni.
Nilienda kwenye matibabu nimeshatibiwa nasubiri niambiwe usalama wangu
utakuwaje katika mazingira halisi,” amesema.

Lissu alishambiliwa kwa risasi tarehe 7
Septemba 2017, akiwa nyumbani kwake eneo la ‘Area D’ jijini Dodoma na
kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa mkoa huo.

Baadaye alihamishiwa Nairobi nchini
Kenya ambapo tarehe 6 Januari 2018 alipelekwa nchini Ubelgiji kwa
matibabu zaidi ambapo yupo mpaka sasa.

Shambulizi dhidi ya Lissu, lilitokea muda mfupi baada ya kutoka kwenye mkutano wa Bunge wa asubuhi.
Chanzo – MwanahalisiOnline