Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kulia)
akiwa ameshikana mkono na Mwenyekiti wa kikundi cha Upendo Beach Bw.
Mzee Makole, wakati Naibu Waziri Ulega akikabidhi msaada wa injini ya
boti yenye thamani ya Shilingi Milioni 15 kwa ajili ya kukiimarisha
kikundi hicho kwenye shughuli za uvuvi. Naibu Waziri Ulega amekabidhi
msaada huo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi akiwa nje ya jengo la ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga wakati alipofika ziara ya kikazi ya siku moja
mkoani humo. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine
Shigella na kwanza kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Tanga Mjini Mhe. Ummy Mwalimu. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari –
Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kulia)
akiwa ameshikana mkono na Mwenyekiti wa kikundi cha ushirika Songambele
Bw. Selemani Haruna Kuzu kilichopo Wilayani Mkinga wakati akimkabidhi
msaada wa injini ya boti yenye thamani ya Shilingi Milioni 15 kwa ajili
ya kukiimarisha kikundi hicho kwenye shughuli za uvuvi. Naibu Waziri
Ulega amekabidhi msaada huo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi akiwa nje
ya jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga wakati
alipofika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo. Wa kwanza kulia ni
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella (Picha na Edward Kondela,
Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Katibu
wa Kikundi Shirikishi cha Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika
Kijiji cha Tawalani, kilichopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga Bw. Salehe
Ally Sua akifafanua jambo juu ya zao la mwani kwa Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine
Shigella na Katibu Tawala wa mkoa huo Bi. Judica Omari, wakati Naibu
Waziri Ulega alipofika katika kijiji hicho kuhamasisha kilimo cha zao la
mwani na kutoa ahadi ya wizara ya kutoa msaada wa Shilingi Milioni Nne
kwa ajili ya kununulia kamba maalumu ya kupandia zao hilo ambazo
ameagiza zifike katika kikundi hicho ndani ya muda mfupi. (Picha na
Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na baadhi ya
wananchi (hawapo pichani) wanaofanya shughuli zao katika Ukanda wa
Habari ya Hindi kuchangamkia fursa ya ufugaji viumbe maji wakiwemo kaa
na jongoo bahari ambao wamekuwa na soko kubwa nje ya nchi. Naibu Waziri
Ulega alikuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Tawalani kilichopo
kata ya Manza iliyopo Wilaya ya Mkinga, Mkoani Tanga wakati wa ziara
yake ya kikazi ya siku moja mkoani humo. (Picha na Edward Kondela, Afisa
Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi) Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akitoa maelekezo kwa
Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Viumbe Maji Baharini kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (aliyevaa suti nyeusi) Dkt. Hamisi Nikuli kuhakikisha
anaharakisha mchakato wa kufikisha Shilingi Milioni Nne au kamba maalum
kwa ajili ya kilimo cha mwani zenye thamani ya fedha hiyo kwa Kikundi
Shirikishi cha Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika Kijiji cha
Tawalani, kilichopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga ikiwa ni mchango wa
Wizara ya Mifugo na Uvu kuhakikisha kilimo cha mwani kinakuwa na tija
zaidi. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na
Uvuvi)
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa kwanza kulia) akiwa
kwenye mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella
(aliyevaa kofia nyeusi) wakati Naibu Waziri Ulega alipotembelea shamba
la wakulima wa mwani katika Kijiji cha Tawalani, kilichopo Wilaya ya
Mkinga, Mkoani Tanga. Naibu Waziri Ulega amefanya ziara ya kikazi ya
siku moja Mkoani Tanga na kuwataka wakulima wa mwani wazidi kuongeza
uzalishaji na kujiunga kwenye vikundi vya ushirika na kuchangamkia fursa
ya ukuzaji viumbe maji kwa kufuga kaa na jongoo bahari ambao wana soko
kubwa nje ya nchi. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya
Mifugo na Uvuvi)
Na. Edward Kondela,MKINGA
Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewataka wananchi wanaofanya
shughuli zao katika Ukanda wa Bahari ya Hindi kuchangamkia fursa ya
ufugaji viumbe maji wakiwemo kaa na jongoo bahari ambao wamekuwa na soko
kubwa nje ya nchi.
Akizungumza mwishoni mwa wiki (24.04.2021)
katika Kijiji cha Tawalani kilichopo kata ya Manza iliyopo Wilaya ya
Mkinga, Mkoani Tanga, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani
humo, Mhe. Ulega amesema Ukanda wa Bahari ya Hindi bado haujatumiwa
vyema katika kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, hivyo
wananchi kujikita zaidi katika uvuvi na kutojishughulisha na ufugaji wa
viumbe maji ambao wamekuwa wakitakiwa nchi mbalimbali.
Mhe.
Ulega amebainisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Samia Suluhu Hassan amekuwa akizungumzia sana Sekta ya Uvuvi kuwekeza
kwenye uchumi wa bluu, hivyo wananchi hususan wanaofanya shughuli za
uvuvi wanatakiwa kuongeza wigo wa shughuli za kiuchumi katika Ukanda wa
Bahari ya Hindi zikiwemo za ufugaji wa viumbe maji hususan kaa na jongoo
bahari pamoja na kilimo cha zao la mwani.
“Shughuli za uchumi
ziwe nyingi sana, rais anataka twende na uchumi wa bluu, anataka tufanye
kazi twende baharini tufanye kazi lakini huku pwani tutengeneze vizimba
kwa ajili ya shughuli mbalimbali mfano kunenepesha kaa na majongoo
bahari na tufunge Kamba kwa ajili ya kulima mwani.” Amesema Mhe. Ulega
Ameongeza
kuwa ni wakati sasa kwa wananchi wa ukanda huo kuondoa umasikini kwa
kuendeleza shughuli za uvuvi, ufugaji wa viumbe maji pamoja na kilimo
cha mwani ili waweze kuongeza mapato na kuwa na wigo mpana zaidi wa
kuongeza kipato kwa mwaka.
Akisoma taarifa ya Kikundi Shirikishi
cha Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) mwishoni mwa wiki (24.04.2021)
katika Kijiji cha Tawalani, katibu wa kikundi hicho Bw. Salehe Ally Sua
amesema katika kipindi cha miezi kumi wamepata tani 52 za mwani na
kuziuza kwa Shilingi Milioni 52 ambapo kwa sasa wamefanikiwa kupata soko
la uhakika ambalo wanauza Shilingi 1,250 kwa kilogramu moja.
Aidha,
amesema kupitia kilimo hicho kipato cha mtu mmoja mmoja kimeweza
kuongezeka na kujikomboa kiuchumi hali ambayo imewasaidia kujipatia
maendeleo na kumudu mahitaji mbalimbali ya kijamii.
Licha ya
mafanikio hayo Bw. Sua amesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali
ikiwemo ya mabadiliko ya hali ya hewa ambayo imekuwa ikiharibu zao hilo
na kupanda na kushuka kwa bei ya zao mwani katika masoko mbalimbali hali
ambayo inawafanya wakulima kushindwa kuweka mipango stahiki ya kilimo
hicho pamoja na ukosefu wa vifaa kwa ajili ya kilimo hicho.
Katika
ziara hiyo Naibu Waziri Ulega amesema wizara itatoa Shilingi Milioni
Nne kwa ajili ya kununua kamba za kilimo cha mwani na kuelekeza fedha au
kamba zenye thamani ya hiyo pesa ziwasilishwe haraka katika kikundi
hicho.
Amesema fedha hizo ziwe chachu kwa ajili ya kukuza kilimo
hicho na kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi itazidi kutoa misaada
mbalimbali kwa vikundi vinavyojishughilisha na kilimo cha zao la mwani
kwa kutoa vifaa zikiwemo kamba ili kuongeza uzalishaji wa zao la mwani
hali ambayo pia inaweza kuchochea uwepo wa viwanda vya kuzalisha bidhaa
zitokanazo na mwani.
Akiwa katika ziara hiyo ya kikazi ya siku
moja Mkoani Tanga, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega
ametoa msaada wa injini mbili za boti kwa ajili vikundi vya uvuvi vya
Upendo Beach Group na Songambele.
Injini hizo zenye thamani ya
shilingi Milioni 30 ambapo kila moja ina thamani ya Shilingi Milioni 15,
Naibu Waziri Ulega amewataka wavuvi hao kutotumia vifaa hivyo kwa
kujiingiza katika uvuvi haramu bali watumie kwa ajili ya uvuvi unaofuata
sheria na kanuni na kwamba serikali bado inaendelea kuweka mazingira
mazuri ya uvuvi kwa kuondoa tozo ambazo zimekuwa kero kwao.
Wakizungumza
baada ya kukabidhiwa injini hizo, viongozi wa vikundi hivyo wamesema
wamefurahishwa na msaada huo ambao utakuwa na tija kwao katika kuongeza
kiwango cha uvuvi na kutumia muda mfupi baharini na kuwataka wavuvi
wengine kujiunga katika ushirika ili waweze kupata misaada mbalimbali
kutoka kwa wadau ikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi.