Mwanga wa siasa ya Lazarus Chakwera ulifufuliwa baada ya mahakama kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka jana
Hafla ya kumuapisha Lazarus Chakwera kuwa rais mpya wa Malawi imefanyika katika mji mkuu wa Lilongwe baada ya kiongozi huyo kushinda duru ya pili ya uchaguzi wa urais uliofanyika Jumanne wiki iliyopita.
Bwana Chakewera alimshinda aliyekuwa rais wa nchi hiyo Peter Mutharika kwa asilimia 58.57 ya kura katika uchaguzi wa Jumanne, tume ya uchaguzi ilitangaza usiku wa Jumamosi.
Mwezi Februari, Mahakama ya katiba nchini Malawi ilifutilia mbali ushindi wa Mutharika katika uchaguzi wa Mei 2019, kutokana na dosari zilizokumba uchaguzi huo.
Nchi iligawanyika vikali wiki kadhaa kuelekea uchaguzi wa marudio.
Malawi ni nchi ya kwanza Afrika kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais na kuandaa duru ya pili ambayo upinzani ukanyakua ushinda.
Kama ilivyotokea Malawi nchini Kenya upinzani ulipinga matokeo ya uchaguzi wa urais mwaka 2017 na kushinda mahakamani.
Hata hivyo mgombea wa upinzani Raila Odinga alisusia duru ya pili ya uchaguzi.
Rais mteule Lazarus Chakwera akipiga kura
Baada ya matokeo rasmi kutangazwa usiku wa Jumamosi, Bw. Chakwera alisema ushindi wake ni “ushindi wa demokrasia na haki” na kuongeze kusema: “Roho yangu imejaa furaha.”
Wafuasi wake walimiminika katika barabara za mji mkuu wa Lilongwe, kushangilia ushindi wao baadhi wakipiga honi za magari na wengine wakipiga fataki.
Ushindi huu unamaanisha nini?
Tukio hili lina umuhimu mkubwa katika historia ya siasa nchini Malawi, na linaonesha wadi kwamba mahatma na time ya uchaguzi hazikuwa tayari kushinikiza kufanya maamuzi kwa kwa maslahi ya ofisi ya rais.
Baada ya hatua hiyo Bw. Mutharika alikimbilia mahakama ya rufaa kupinga uamuzi huo lakini majaji walisimama kidete kutoa uamuzi usioegemea upande wowote.
Na sasa wananchi wamefanya uamuzi wao kwa kumemkataa katika duru ya pili ya uchaguzi.
Ushindi wa Peter Mutharika mwaka jana ulifutwa na mahakama ya katiba baada ya ushahidi kuonesha kuwa uchaguzi wa mwaka jana yalichakachuliwa.
Rais anayeondoka madarakani Peter Mutharika ameutaja uchaguzi wa Jumanne kuwa mbaya zaidi uliowahi kushuhudiwa nchini Malawi.
Bwana Mutharika sasa analalamika kwamba uchaguzi huo haukuwa wa haki na huenda akawasilisha malalamishi yake mahakamani, lakini raia wa Malawi wamemchagua Lazarus Chakwera kama rais wao mpya.
Akizungumza kabla ya matokeo hayo ya Jumamosi, bwana Mutharika alisema kwamba licha ya kwamba matokeo ya uchaguzi huo ”hayakubaliki” , ni ”matumaini kwamba raia wa taifa hilo watalisukuma mbele gurudumu la taifa hilo badala ya nyuma”.
Muhubiri huyo wa kanisa la Pentecostal na muhadhiri wa somo la theolojia atalazimika kuponya vidonda vya taifa ambalo limepitia miezi kadhaa ya msukosuko wa kisiasa.
Rais mteule, Lazarus Chakwera sasa anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuleta nchi pamoja kufuatia mgawanyiko uliojitokeza na kumaliza ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Pia ana kibarua cha kukabiliana na ufisadi, kupunguza umaskini na ukosefu wa ajira, mambo amabayo yalikuwa ni miongoni mwa masuala ya msingi katika uchaguzi huo.
Mpaka mwaka 2013, rais mteule wa Malawi Lazarus Chakwera alikuwa ni kiongozi wa muungano wa makanisa ya Kipentekoste nchini humo.
Maisha yake ya kabla ya siasa kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1970 yalikuwa yamejikita katika dini, baada ya kusomea Falsafa na Theolojia, na kwa zaidi ya miaka 30 akawa mwalimu wa taaluma hizo mbili pamoja na uongozi wa kanisa.
Lakini akiwa katika uongozi wa kanisa, pia alikuwa na ndoto ya kushika nafasi ya kisiasa na kuwatumikia Wamalawi wote na si wa madhebebu yake tu.
Mwaka 2013, aliwashangaza wengi pale alipoamua kujiuzulu nafasi zake zote katika uongozi wa kanisa ili kujitosa moja kwa moja kwenye siasa.
Miaka saba baada ya uamuzi huo, ameshinda urais katika uchaguzi wa kihistoria.
Kugombea urais
Mwaka 2014 akagombea urais kupitia chama cha Malawi Congress Party (MCP) na kushindwa na Profesa Peter Mutharika wa chama cha Democratic Progressive Party (DPP).
Katika uchaguzi huo, kulikuwa na minong’ono ya kuibwa kwa kura, lakini Chakwera aliyeshika nafasi ya pili na kuwa kiongozi wa kambi ya upinzani aliwaasa wafuasi wake wawe watulivu, wakubali kushindwa, wadumishe amani na kusubiri uchaguzi unaofuata.
Uchaguzi alokuwa akiukusudia Chakwera kujipanga zaidi na wafuasi wake ulikuwa wa mwaka 2019, na kwa hakika walifanya hivyo.
Mwezi Mei 2019 wananchi wa taifa hilo la kusini mwa Afrika walipiga kura, matokeo ya mwisho yakampa ushindi rais aliye madarakani, Profesa Mutharika kwa asilimia 38.5 ya kura dhidi ya asilimia 35.4 ya Chakwera.
Hata hivyo vyama vya upinzani vikiongozwa na Chakwera vilipinga vikali matokeo hayo na kwenda mahakamani.
Maandamano makubwa pia yalishuhudiwa katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo dhidi ya matokeo hayo. Waandamanaji hao walishinikiza mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jane Ansah ajiuzulu.
Mahakama ya katiba ikathibitisha kuwa kulikuwa na udanganyifu wa wazi katika uchaguzi huo na kubatilisha matokeo hayo mwezi Februari 2020 na kuamuru uchaguzi mpya ufanyike ndani ya siku 150. Bi Ansah akajiuzulu mwezi Mei kupisha uchaguzi mpya.
Kujipanga upya kwa uchaguzi
Rais anayemaliza muda wake nchini Malawi Peter Mutharika ametangaza kutokukubaliana na kushindwa na Chakwera.
Baada ya matokeo ya awali kutupiliwa mbali mahakamani, upizani nchini Malawi ukajipanga upya huku ukiongozwa na Chakwera.
Katika uchaguzi wa 2019, wagombea sita wa upinzani walikuwa wakipambana kumng’oa Mutharika. Katika kura ya marudio iliyopigwa wiki iliyopita jumla ya vyama tisa vilimuunga mkono Chakwera katika umoja wa wapinzani unaofahamika kama Tonse.
Aliyekuwa makamu wa rais wa kwanza wa Mutharika Saulos Chilima, alishika nafasi ya tatu mwezi Mei mwaka jana baada ya kupata asilimia 20 ya kura zote.
Katika uchaguzi wa wiki iliyopita, Chilima aliunganisha nguvu na Chakwera na kuwa mgombea mwenza wake. Rais wa zamani wa Malawi Bi Joyce Banda pia ameunga mkono umoja huo wa wapinzani.
Kutokana na kujipanga huko kupya, Chakwera akafanikiwa kumuangusha Mutharika kwa kupata asilimia 58.7 ya kura zote zilizopigwa.
Japo Malawi ni nchi ya pili barani Afrika baada ya Kenya kurudia uchaguzi wa rais baaada ya matokeo ya awali kupingwa mahakamani, imekuwa nchi ya kwanza kwa mgombea wa upinzani kushinda duru ya pili ya uchaguzi.
Ushindi wa Chakwera unaenda kutoa matumaini mapya kwa uhuru wa mahakama barani humo, na umuhimu wa kuwa na tume na mifumo huru ya uchaguzi.
Chakwera pia anakirudisha mamlakani chama kilichopigania uhuru wa nchi hiyo MCP na kuiongoza Malawi kwa miaka 30 ya kwanza (1964-1994) chini ya Dkt Hastings Banda. Toka Banda kushindwa kwenye uchaguzi wa 1994 chama hicho kilikuwa kwenye upinzani kwa miaka 26.
Je, Chakwera ni nani?
Lazarus Chakwera ameungwa mkono na vyama tisa vya upinzani katiku uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita.
Chakwera amezaliwa miaka 65 iliyopita kutoka katika familia ya kimasikini ambayo ilikuwa ikitegemea kilimo kujikimu.
Mwaka 1977 alihitimu Shahada ya Kwanza ya Filosofia kutoka Chuo Kikuu cha Malawi, mwaka 1990 akapata Shahada ya Uzamivu katika Theolojia kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Kusini, na hatimaye kutunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka Chuo Kikuu cha Tritinity nchini Marekani.
Kutoka mwaka 1983 alianza kufundisha katika seminari na vyuo vya makanisa ya Pentekoste (Walokole), na mwaka 1989 akachaguliwa kuwa rais wa makanisa hayo nchini Malawi na kuhudumu uongozini kwa miaka 24 mpaka pale alipojiuzulu mwaka 2013.
Wakati akijiuzulu na kuingia kwenye siasa, alisema katika mahojiano kuwa “Mungu amemtuma kwenda kuwahudumia watu wengine pia”.
Ni dhahiri kuwa Chakwera hana mizizi mirefu kwenye ulingo wa siasa, na mafanikio yake mengi kama kiongozi yamekuwa ndani ya kanisa. Lakini, ushindi wake wa urais ni jambo ambalo kamwe halitakiwi kudogoshwa.
Japo hajawahi kushika nafasi yoyote ya umma hapo kabla, kumuangusha rais aliyepo madarakani kwa kutumia chama kilichopigania uhuru na baadaye kulaumiwa kwa kuminya haki za binadamu ni mafanikio makubwa kisiasa.
Kwa wafuasi wake, Chakwera anafahamika zaidi kwa jina la utani la “Dr Laz” na wana matumaini makubwa juu yake kundosha rushwa na kukabiliana na umasikini.
Silaha yake kubwa ni uwezo wake wa ushawishi katika majadiliano, na Wamalawi wanategemea kuwa ataumia ushawishi huo kuiunganisha tena nchi yao pamoja baada ya kipindi cha mwaka mmoja wa maandamano na minyukano ya kisiasa.
Kwa upande wa familia, Chakwera na mkewe bi Monica Chakwera na wana watoto wakubwa wanne pamoja na wajukuu kadhaa.
Chanzo – BBC Swahili