Utpc yakutanisha waratibu press klabu dodoma, watakiwa kufanyakazi kwa malengo

Na Mwandishi wetu, APC Blog, Dodoma

Waratibu wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania wametakiwa kutekeleza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa malengo na kufuata mwongozo wa utendaji kazi kwa ustawi na maendeleo ya Klabu zao. 

 Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Abubakar Karsan wakati akifungua mafunzo kwa Waratibu wa Klabu kuhusu ufuatiliaji wa ukiukwaji wa uhuru wa kupata habari na uhuru wa kujieleza. 
 Lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha Waratibu wa Klabu kwa kuwapatia maarifa, juzi na uelewa wa namna ya kufuatilia na kutoa taarifa za ukiukwaji wa uhuru wa habari, uhuru wa kupata taarifa lakini pia madhila mengine mbalimbali ambayo Waandishi wa Habari wanakutana nayo katika maeneo wanayofanyia kazi. 
 Mafunzo hayo ya siku tatu kuanzia leo Disemba 14-16, 2020 yanatolewa na Mwezeshaji; Wakili Leopold Mosha kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), katika hoteli ya Royal Village mjini Dodoma. 
 Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli za mradi wa UTPC kwa kushirikiana na International Media Support (IMS), ambao umelenga kuzijengea uwezo taasisi za kihabari kushiriki katika ushawishi kuhusu uhuru wa habari na uhuru wa wananchi kupata taarifa.
 Mradi huu ni wa shirika la IMS la nchini Denmark, ambao wamefadhiliwa na Umoja wa Ulaya (European union). 
 UTPC imepewa fursa ya kushiriki kwenye mradi huu ambapo itafanya kazi na IMS kwa miaka miwili ikishirikiana na taasisi nyingine kama MisaTAN, TAMWA na MULIKA ya Zanzibar.

Picha mbalimbali za Matukio wakati wa Warsha hiyo.

Picha mbalimbali za Matukio wakati wa Warsha hiyo.