Vilio na huzuni vyatawala mgodi wa dhahabu imalanguza geita

Na Issa Mtuwa “WM” – Geita

Majonzi
na huzuni vimetawala kwenye mgodi wa wachimbaji wadogo wa Imalanguza
wilaya ya Geita kata ya Lwamgasa katika Kijiji cha Imalanguzu, mara
baada ya kuwasili Naibu Waziri wa Madini Stanslausi Nyongo mgodini hapo
akiwa na viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya Madini, uongozi wa
mkoa na viongozi wa dini kwa ajili ya kwenda kusitisha shughuli za
uokoaji wa wachimbaji wadogo wawili Karos Msukuma Paulo mwenyeji wa
Chato na Kulwa Joseph Mahungija mwenyeji wa Busolwa Nyang’wale
waliofukiwa kifusi siku ya tarehe 1/10/2019.
 
Usitishaji
wa zoezi hilo umefanyika tarehe 9/11/2019 ikiwa ni siku 39 tangu
wachimbaji hao wafukiwe na kifusi kutokana na uwepo wa changamoto
mbalimbali zilizo jitokeza katika kipindi chote cha uokoaji. Ripoti
maalam ya timu ya wataalam wa uokoji imeeleza kuwa kumekuwa na
changamoto nyingi wakati wote wa ukoji zilizopelekea kuwa na ugumu wa
kuwaokoa wachimbaji hao. 
 
Akiwasilisha
taarifa ya wataalam wa uokoaji iliyoishauri serikali kusitisha kwa
zoezi hilo la uokoaji kwa Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo,  mkuu
wa wilaya ya Geita Josephat Maganga amemwambia Naibu Waziri wa Madini
kuwa miongoni mwa changamoto zilizojitokeza wakati wa uokoaji ni pamoja
na uwepo wa maji chini ya mgodi, mwingiano wa magogo mbalimbali chini ya
shimo la mgodi, na kutokuwa na usalama katika eneo hilo hata kwa vyombo
vya uokoaji.
 
Maganga
aliongeza kuwa, kulikuwa na wataalam wa makundi mbalimbali ya uokoaji
na vifaa vya kutosha kutoka kwa jeshi na uokoaji, mgodi wa dhahabu wa
Geita (GGM), na makampuni mengine kutoka kwenye migodi mbalimbali,
lakini pamoja na juhudi zote hizo imeshindikana kupatikana kwao.
 
Taarifa
hiyo iliendelea kusema kuwa  siku ya tukio hilo, kwenye shimo hilo
kulikuwa na wachimbaji 5 ambapo 3 kati yao waliokolewa siku hiyo hiyo na
wawili hawakuweza kupatikana hadi zoezi hilo la uokoaji linasitishwa.
 
Kwa
upande wake Naibu Waziri Nyongo, akiongea kwa masikitiko na majozi
kwenye hadhara hiyo, Nyongo amesema kwanza lililotokea ni bahati mbaya
na kwamba serikali imesikitishwa na tukio hilo na kwamba iko pamoja
wafiwa na wachimbaji wote.
 
Ameongeza
kuwa, serikali inathamini sana hata uhai wa mtu mmoja kuliko dhahabu au
madini yote yaliko chini na ndio maana inasisitiza wachimbaji kuchimba
kwa kufuata utaratibu na sharia ili wachimbe kwa kuzingaatia usalama ili
kuepukana na majanga kama hayo. 
 
Nyongo
ametowa kauli ya serikali ya kuhitimisha shughuli za uokoaji na kutoa
maelekezo kuhusu eneo hilo ambalo wachimbaji hao wamefukiwa na kifusi.
 
“Na
sasa tunakwenda kufanya ibada ya kwenda kuwazika wenzetu, viongi wetu
wa dini wako hapa watatuongoza katika ibada hiyo kwa ajili ya maombi.
Natamka kuwa, shughuli zote za uchimbaji katika eneo ambalo tunaamini
kuwa ndipo wezentu hawa wapo, basi eneo hilo litambuliwe rasmi kuwa ndio
kabuli lao na kama kuna undelezaji wa shughuli ya uchimbaji utaendelea
katika eneo lingine na kwa utaratibu mwingine.” alisema Nyongo.
 
Nyongo
pia alitoa maagizo kwa afisa madini mkazi mkoa wa Geita na timu yake
kusimamia usitishwaji wa shughuli za uchimbaji katika eneo hilo mpaka
pale hatua za uzingatiaji usalama ziwe zimefuatwa ili kuepusha ajali
nyingine.
 
Kwa
upannde wake Mchungaji Nuhu Suleman alie ongoza ibada hiyo ya kuwaombea
marehemu alisema, hapana budi kumshukuru mungu kwa kila jambo na kila
jambo hukusudiwa na mungu. Amewakumbusha waumini wote kumuelekea mungu
kwani yeye ndie mwenye upekee na ufalme na kwamba maisha ya binaadamu
yana ukomo ni vyema kila mmoja akajiandaa na safari hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *