Vipamaru na taswira ya maisha ya watoto kwa mataifa yaliyo bado na mfungo wa corona.

PIX-Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Vipamaru, Anania Mlalila (Kushoto)wakiwa na wadau wengine wakiwemo wanahabari katika Studio za Redio Ndingara FM wakiendesha Kipindi cha Elimu juu ya Ukatili wa kijinsia wakati wa Corona

Na Mwandishi Wetu,Mbeya.

NI jambo lisilopingika
kuona kuona jambo linalofanywa na familia moja likifanywa pia na familia
jirani.Hii hutokana na mfumo wa maisha wenye kuwa na mienendo yenye kufanana
hata familia hizi mbili zikawa majirani.

Athari za matendo
yenye kufanana kutokana na ujirani ndiyo huzidia tafsiri hata kwa watu wa mbali
kutambua kuwa kwa mienendo ya mtu wa familia A ni wazi atakuwa akitokea jirani
na watu wa familia B.Yawezekana ni kutokana na matendo yenye
muonekano,uvaaji,matamshi,adabu,heshima na mengineyo.

Hivyo ndivyo pia
ukweli usiopingika katika mwenendo wa kimaisha ulioonekana wakati wa Uonjwa wa
Corona hapa Tanzania usivyoweza kutofautishwa na tafsiri inayoweza kuwa
inaendelea katika mataifa jirani ambayo bado yanaendelea kusumbuliwa na ugonjwa
huo wa Homa kali ya mapafu.

 

Upo uwezekano wa wadau
kutoipa uzito makala haya kwakuwa Tanzania inatajwa kutokuwa tena na Corona. Lakini
hatuwezi kuwaachia majirani zetu kuendelea kuzijadili athari za mlipuko huo
kwakuwa makwao unatajwa kuwepo bado. Uchambuzi wetu unaweza kusaidia pia
majirani kuchukua hatua madhubuti hasa kwenye kupinga ukatili dhidi ya watoto
kutokana na shule kuendelea kufungwa na wao kulazimika kuwepo majumbani.

 

“Wafanyabiashara wengi
wa mitaani kwa sasa wamegeuka watoto wadogo si wale watu wazima tuliowazoea na
imefika mahali sehemu kama maofisini watoto hawa wamegeuka kero maana
wanapoingia na biashara wanazotembeza badala ya kutamani anachokiuza unaanza
kumhurumia mtoto kutokana na umri wake ikilinganishwa na kazi.”

 

“Kwa sasa tunashuhudia
ukatili wa watoto unaofanywa na wazazi kuwatumikisha kazi zisizo salama.Tunaona
hata kwenye vibarua vya kufyatua tofali au vya kuvuna utakuta familia nzima
imebebwa hadi watoto wadogo.”

 

Hayo yalikuwa sehemu
ya maneno ya Afisa Maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya wilaya ya Kalambo
mkoani Rukwa,Marium Kimashi kwenye mkutano wa kujadili Masuala ya Ukatili wa
kijinsia na watoto katika kipindi shule zilipofungwa nchini kwaajili ya kuepuka
kusambaa kwa Homa kali ya Mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona.

 

Ni mkutano uliofanyika
kupitia mtandao wa kijamii wa Zoom ukiandaliwa na Shirika la Vijana Pambania
Maendeleo Rukwa(VIPAMARU) lenye makao yake makuu katika Manispaa ya
Sumbawanga.Watoto walikuwa sehemu ya mjadala muhimu wa mkutano huu uliolenga
kuyaangazia maisha yao katika kipindi walichokaa majumbani huku tarehe ya
kuisha kwa likizo hiyo ikiwa haijulikani.

 

Mitazamo ya wadau
katika mkutano huo ulileta taswira ya maisha halisi yaliyokuwa yakiendelea
ndani ya jamii mkoani hapa.Wengi walionesha aina za ukatili walizokuwa
wakifanyiwa watoto hususani wanaotoka kwenye familia duni.Wakati wenzao
wakipambaniwa na wazazi na walezi wao kujisomea kupitia njia mbalimbali ikiwemo
mitandao wao walikwenda kutumikishwa,wakageuka sehemu ya nguvu kazi pasipo
kujali umri wao.

 

Afisa Ufuatiliaji na
Mtathimini wa Vipamaru,Donatha Haule
 alisema watoto wanaotokea kwenye familia zilizo na wazazi
au walezi wenye ulemavu nao walikuwa na aina tofauti ya kutumikishwa.Watoto
wote walitoka majumbani mwao wakiwasindikiza mjini walemavu hususani wa macho
na walipofika huko watoto waligawiwa mitaa ya kuwasindikiza wakati wazazi wao
wakiomba.

 

“Kwa hapa mjini
tofauti na tulivyosikia kutoka maeneo mengine hapa watoto waligawiwa mitaa ya
kuwatembeza wazazi wanapoomba.Huyu anaweza akaanza asubuhi saa tatu wakatembea
na mlemavu labda mitaa kadhaa baadaye saa tano akachukuliwa mwingine.Hawakuwa
na namna ya kujitetea wabakie nyumbani walau wajisomee au hata wajikumbushe
yale waliyokwishajifunza shuleni kabla ya shule kufungwa.”alisema Dodatha.

 

Afisa Maendeleo ya
jamii wa Manispaa ya Sumbawanga,Maxmillian Babile alisema ukatili dhidi ya
watoto haukuishia kwenye kutumikishwa lakini pia ulibainika wa kisaikolojia
ikiwemo kushuhudia ugomvi wa wazazi au walezi wao wawapo majumbani.Upo pia wa
wao wenyewe kupigwa au kusemewa maneno mabaya hasa pale walipoonesha kuchoshwa
na kazi walizopewa na kuhitaji kupumzika.

 

Babile alisema pia kwa
watoto waliobahatika kuwa na wazazi walio na uwezo wa kuwajazia vifurushi
kwenye simu zao ili waweze kujisomea na wao walijikuta wanakumbana na ukatili
wa kisaikolojia.Hii ilitokea zaidi kwa watoto ambao wazazi walikosa muda wa
kuwasimamia kwa karibu wakawaacha wajifanyie wenyewe mambo yao.Hawa walijikuta
wanaacha kufanya kilichotarajiwa na kuanza kuingia kwenye mitandao mingine
ikiwemo yenye picha zisizofaa hasa za utupu.

 

“Wazazi kwa nia nzuri
wanawaachia simu watoto wao ili waweze kujisomea lakini wanapokosa usimamizi
watoto wanakwenda mbali zaidi na kudownload picha za ngono.Lakini wengine
wanaona kama line za mzazi zinamnyima kufanya mambo yake anaamua kutafuta kwa
uficho line yake hivyo akiachiwa simu pasipo uangalizi ndiyo anayoitumia kwa
mawasiliano ambayo mzazi hakunuia.”

 

Kuenezwa kwa lawama kulikokuwa
kukifanywa na wanajamii ikiwemo wazazi na walezi kupiga picha watoto wao hasa
walio na umri mdogo walipofanya makosa kama ya kumwaga mafuta,rangi,maji na
kuzisambaza nako kulionekana kuwakera wadau wa mkutano huo wakisema ni aina ya
ukatili kwakuwa umri wa watoto hao si wa kujifanyia maamuzi ya kujitangaza
mitandaoni.

 

Walisema pia kupitia
Sentensi za wazazi mitandaoni za Kuhoji Lini shule zitafunguliwa zikiambatana
na picha za michezo ya watoto iliyokuwa inaonekana haifurahiwi na wazazi
kulidhihirisha wazazi na walezi kukosa upendo kwa watoto wao.Walidhihirisha
kuwa walimu wana upendo na ulezi wa kweli kwa watoto kuliko wazazi kwakuwa
michezo wanayocheza nyumbani ndiyo hucheza na mashuleni chini ya walimu wao na
wala walimu hawajawahi kuwapiga picha wakasambaza mitandaoni.

 “Zile picha na
malalamiko ya wazazi tulianza kuyaona mitandaoni siku chache tu baada ya shule
kufungwa..na imezoeleka kila kunapokuwa likizo za wanafunzi.Sasa unajiuliza
wewe umekaa na mtoto wiki moja unalalamika unataka arudi shuleni mbona mwalimu
anakaa naye muhula mzima na hampigi picha kuzirusha.Kumbe wenye mapenzi na
watoto ni walimu na siyo sisi tunaowazaa”alisema mmoja wa washiriki mwanahabari
aliyeomba jina lake kuhifadhiwa.

 Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Vipamaru,Anania Mlalila
 anasema Mkutano huo uliofanyika Juni 8 mwaka huu ulizaa
matunda kutokana na maoni ya wadau hao kuleta msukumo kwa Shirika kupitia Mradi
wake wa Kupinga ukatili wa Kijinsia na watoto wakati wa Covid 19 kupanua wigo
wa kuyaangazia maisha ya watoto wakati shule zilipofungwa kutokana na Corona.Na
sasa uangalizi huo hata baada ya Tanzania kutangazwa kutokuwepo kwa Corona
unaendelezwa kila wakati wa likizo za shule.

 Matunda ya
mkutano huu yakawa wadau wote walioshiriki kuwa na mkakati wa pamoja katika
kuwafuatilia watoto.Kupeana taarifa mara kwa mara,kupeana mwendelezo wa hatua
zinazochukuliwa pasipo kujali utofauti wa kada zao za kazi.Washiriki hawa ni
Uliwashirikisha Maafisa Maendeleo na Maafisa Ustawi wa jamii,Maafisa kutoka
Madawati ya jinsia ya Polisi wa wilaya zote za mkoa wa Rukwa na Wanahabari.

 “Hapo ndipo
tulipoamua pia kuwa na Group la WhatsApp la wadau walioshiriki mkutano
huu.Lengo ni kuzidi kufanya kazi kwa ukaribu..yaani mwanahabari akipata tetesi
au taarifa za Ukatili dhidi ya mtoto basi asiishie tu kuripoti bali awasiliane
na Dawati la Polisi lifanye kazi yake..awasiliane na Afisa ustawi wa jamii au
Maendeleo ya jamii nao walifanyie kazi.Na wakati huo huo sote tuwe tunajua nini
kinachoendelea kupitia group.”

 

“Ni hapo pia tulipoona
kuna haja ya kutoa elimu kwa wananchi mkoani hapa.Tukaanzisha mpango wa vipindi
vya redio ili tusiishie sisi pekee kuwasiliana bali tuishirikishe na jamii ili
na wao wawe sehemu ya washiriki katika kukemea ukatili dhidi ya watoto kwenye
maeneo yao.”

 Mkurugenzi huyo
anasema kumekuwepo na matokeo chanya baada ya kuanza kuendeshwa kwa vipindi vya
kutoa elimu.Wanajamii wamejua aina ya ukatili wanaofanyiwa watoto katika
nyakati za likizo za shule sit u wakati wa likizo ya Corona.Na pia hatua za
kuchukua wanapoona mtoto wa jirani anafanyiwa ukatili zinafanyiwa kazi tofauti
na awali.

 “Kupitia vipindi
hivi tunapokea maoni mengi.Kwa mabinti wapo wasikilizaji walioshauri shule au
vyuo zifunguliwe tu kutokana na watoto kuachwa wakizurula mitaani badala ya
kubaki nyumbani kwa wakati ule.Lakini wengine wakasema baada ya shule
kufunguliwa tutarajie mimba nyingi za wanafunzi.Na tayari hadi leo hii
tunaambiwa kuna kesi nane za mimba kwa wanafunzi katika kata ya Lwiche manispaa
ya Sumbawanga kwa mujibu wa Ripoti kutoka Polisi Dawati la jinsia katika
kipindi cha Machi hadi Mei mwaka huu.”

 “Lakini sisi
kama Vipamaru tuaamini kuwa huenda jamii iliamini kwenye matokeo
mabaya ya watoto kukaa nyumbani kwakuwa hakukuwa na ushirikiano wa usimamizi wa
malezi.Kila mmoja alifanya kivyake na familia yake hivyo hata alipomuona mtoto
wa mwenzie akizurula alimwacha azurule.”

 Mlalila anashauri jamii kurejea katika malezi ya ushirikiano yawezekana
isiwe kwa ukaribu sana kutokana na kuepuka kusambaa kwa maambukizi ya Corona
lakini walau kwa kupashana habari baina ya mzazi mmoja na jirani yake pale
wanapoona kuna ukakasi kwenye malezi ya mtoto uanaosababisha ukatili au
mwelekeo mbovu kwakuwa kuharibikiwa kwa mtoto mmoja si hasara ya mzazi pekee
bali jamii yote inayomzunguka.

 Anasema ni
muhimu jamii ikatambua kuwa athari za ukatili dhidi ya mtoto ni pamoja na
mhanga kukuwa katika fikra potofu za kuamini alichokuwa akifanyiwa utotoni ni
halali hivyo na yeye akaja kuwafanyia watoto wake au wa jirani zake.Kuna athari
pia kwa wazazi na jamii inayomzunguka wakati wa makuzi yake kwakuwa siku akikua
anaweza kuamua kulipiza kisasi na ikaleta changamoto kwa jamii husika.Muhimu
tahadhari zikachukuliwa mapema kwa ushirikiano.

 Baadhi ya
wasikilizaji wa vipindi vya vijana na wanawake
ambavyo Vipamaru wamekuwa wakivitumia kutoa elimu katika kituo cha
Redio cha Ndingara FM wanasema kumekuwa na mabadiliko ya kimtazamo kwa jamii
juu ya malezi ya watoto kwakuwa wanajamii wenyewe wameanza kusemana pale
wanapoona jirani anakiuka miiko ya malezi ikiwemo mzazi kuendekeza ulevi na
kuisahau familia yake.

Haya yaliibuliwa na Shirika
la Vipamaru huko mkoani Rukwa,muhimu kwa mataifa majirani na Tanzania ni
kutumia makala haya kama chachu ya kuyaangazia maisha ya watoto ambao kwenye
mataifa yao wanalazimika kuendelea kuwafungia majumbani kutokana na uwepo wa
Corona.Nasi watanzania wakati tukiendelea kuwaombea majirani adui huyu aondoke
basi tusiache kutoa ushauri wa nini wakifanye pale tunapopata fursa kama hii.