Viwanda vinavyotumia malighafi za mifugo kutambuliwa ili kufikia uchumi wa kati

Na. Edward Kondela

Serikali
imewataka maafisa mifugo wote nchini katika maeneo yao ya kazi
kufuatilia idadi ya viwanda vinavyotumia malighafi ya mifugo ambavyo
vinafanya kazi pamoja na ambavyo havifanyi kazi kufahamu changamoto 
zake ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi na viwanda hivyo vianze kufanya kazi
kuendana na azma ya serikali ya kufikia uchumi wa kati unaotegemea
viwanda ifikapo Mwaka 2025.

Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel
amebainisha hayo jana (27.10.2019) katika Wilaya ya Simanjiro Mkoani
Manyara wakati alipotembelea kiwanda cha kuchakata mazao ya mifugo cha
Rotiana Social Investment ambacho kwa sasa hakifanyi kazi na baadhi ya
mitambo yake kuharibika na vifaa vingine kudaiwa kuibiwa na baadhi ya
watu waliokuwa wakikisimamia kiwanda hicho.

Prof.
Gabriel amesema lengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha
inasimamia vyema azma ya serikali kuhakikisha viwanda vya malighafi za
mifugo vinafanya kazi na kutaka maafisa hao wa mifugo kushirikiana na
maafisa kutoka Taasisi ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) katika
kubaini changamoto mbalimbali zinazovikabili viwanda hivyo.

“Kwa
kushirikiana na ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Manyara umuliki wa mitambo
lazima uweze kufahamika kisheria umekaaje na kuhakikisha viwanda ambavyo
vimekuwa vikichakata mazao ya mifugo vinafanya kazi ili mnyororo wa
mazao ya mifugo uendelee kufanya kazi na kufikia uchumi wa kati 2025
kupitia viwanda.” Amesema Prof. Gabriel

Kuhusu
kiwanda cha Rotiana Social Investment chenye eneo la Hekari 12,500
Prof. Gabriel ameutaka uongozi wa Mkoa wa Manyara kuendelea kufuatilia
kwa kina umiliki wa ardhi wa eneo hilo kisheria kutokana na kiwanda
hicho kutofanya kazi baada ya kuibuliwa na Taasisi ya Ilaramatak
Lorkornei na Stitching Her Groen Wout ya nchini Uholanzi na kufunguliwa
kiwanda mwaka 2011 ambapo kwa sasa hakifanyi kazi.

Kiwanda
hicho ambacho kina uwezo wa kuchinja ng’ombe zaidi ya 300 kwa siku na
pamoja na mifugo mingine wakiwemo mbuzi katibu mkuu huyo ametaka pia
uongozi wa Mkoa wa Manayara kufuatilia kwa kina umiliki wa mitambo hiyo
kisheria na hatimaye kiwanda hicho kiweze kufanya kazi baada ya taratibu
za kisheria kukamilika.

Bibi
Mary Kisyoki ambaye amewahi kuwa mmoja wa viongozi wa Shamba la Rotiana
linalomiliki kiwanda cha Rotiana Social Invetment ameshukuru uongozi wa
Mkoa wa Manyara na TCCIA katika kufuatilia kiwanda hicho ambapo amesema
kupitia serikali ya awamu ya tano ataendelea kusimamia ukweli ambao
amekuwa akiusimamia katika kulinda mali za kiwanda hicho zinasimamiwa
vyema na hatimaye kiweze kufanya kazi.

Amesema
katika kipindi chote mara baada ya kiwanda hicho kusimama kufanya kazi
amekuwa akihakikisha mali za kiwanda hazizidi kuibiwa au kuharibiwa na
baadhi ya watu.

Kwa
upande wake Katibu Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Manyara Bibi Mwanahamisi
Hussein ametoa wito kwa makatibu wenzake wa mikoa na wilaya kuzidi kutoa
ushirikiano kwa serikali na sekta binafsi na kujikita kuangalia fursa
na changamtoto zilizopo ili kuweza kuzitatua zikiwemo za wafugaji na
kuhakikisha jamii inapata faida kutokana na yale wanayosimamia.

Aidha
ameishuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuweza kufuatialia masuala
mbalimbali kwa kuweza kufanyia kazi yale ambayo yamekuwa yakifikishwa
katika wizara hiyo likiwemo la kutofanya kazi kwa kiwanda cha Rotiana
Social Investmant suala ambalo amekuwa akilisimamia ili kuhakikisha
kiwanda hicho kinafahamika umiliki wake na hatimaye kiweze kufanya kazi.