WAANDISHI
wa habari nchini wameshauriwa kujiunga na Chama cha Wafanyakazi wa
Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) na kuanzisha matawi katika ofisi
zao.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya
jana jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo kwa waandishi wa
habari wanawake yaliyoandaliwa na chama hicho.
Alisema kwa miaka
mingi waandishi wa habari wamekuwa wakipigania haki za watu wengine na
kusaha za kwao hivyo wakati umefika kwa kujenga chombo sahihi kwa
maslahi yao.
“Nitumie nafasi hii kuwaomba waandishi wa habari
nchini kote kujiunga na JOWUTA ili tuwe na nguvu moja ya kupigania
masalhi yetu kwani kwa muda mrefu tumekuwa tukipitia wakati mgumu sana,”
alisema.
Msuya alisema JOWUTA imejipanga kupita katika vyombo
vya habari ili kuweza kuzungumza na wamiliki na waandishi kuhusu
ushiriki wa pande zote kwa chama hicho.
Alisema vyama vya
wafanyakazi ni takwa la kisheria hivyo mwajiri na mwajiriwa wanapaswa
kulitekeleza kivitendo na sehemu sahihi ni JOWUTA.
Katibu huyo aliwataka waandishi wa habari kuanzisha matawi ndani ya vyombo vyao kwa kuwa hiyo ni haki yao ya kisheria.
Aidha,
alisema taaluma ya habari imekuwa na changamoto ikilinganishwa na fani
nyingine, ikiwamo ajira, usalama duni na kusababisha wengi wao kukosa
haki za kustaafu kisheria hivyo JOWUTA wamejipanga kupigania hilo.
Mwezeshaji
wa mafunzo hayo, Simbarashe Msasanuri, wanahabari ili kubadili mfumo
uliopo kwenye vyombo vya habari, inapaswa kuvunja ukimya kwa kuwawezesha
hususan wanawake wanahabari.
Alisema ili kufikia usawa ndani ya
vyumba vya habari, inatakiwa kubadili utamaduni uliopo kwa wanawake
kujiendeleza na kuwa viongozi.
“Waandishi kwa muda mrefu
mnatimiza wajibu wenu wa kuwa sauti ya wasio na sauti, lakini msisahau
kujisemea wenyewe kwa kuzitatua changamoto zenu,” alisema Msasanuri.
Alieleza
kuwajumuisha wanaume katika kufahamu changamoto zinazowakumba wanawake,
kama vile za kijinsia kutatatua tatizo la rushwa ya ngono ambayo
imekuwa ikitumika kwa baadhi yao kuinua mazingira ya kazi.
Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Tanzania (JOWUTA), Suleiman
Msuya, akimkabidhi cheti mshiriki Christina Mwakangale.
Katibu Mkuu akiwa na washiriki wa mafunzo