Wabunge morogoro wafagilia umeme vijijini

 

Waziri
wa Nishati Dkt. Medard Kalemani Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi
wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa
Pili, Mkoa wa Morogoro, Juni 17, 2021. Hafla hiyo ilifanyika kijiji cha
Muheza Ititu Wilaya ya Gairo.

*Mbunge wa Kilosa ambaye
pia ni Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza
wakati wa uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini
Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Morogoro. Uzinduzi huo
ulifanyika katika kijiji cha Muheza Ititu wilayani Gairo, Juni 17,
2021.

Mbunge wa Gairo, Ahmed
Shabiby akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa
Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mkoa wa
Morogoro. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Muheza Ititu
wilayani Gairo Juni 17, 2021.


Mbunge wa Morogoro Kusini, Innocent Kalogeris akizungumza wakati wa
hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya
Tatu Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Morogoro. Uzinduzi huo ulifanyika katika
kijiji cha Muheza Ititu, Juni 17, 2021.


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigela akizungumza wakati wa uzinduzi
wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa
Pili, Mkoa wa Morogoro. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Muheza
Ititu, wilayani Gairo Juni 17, 2021.


Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Dennis Londo akizungumza wakati wa hafla ya
uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu
Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Morogoro. Uzinduzi huo ulifanyika katika
kijiji cha Muheza Ititu wilayani Gairo, Juni 17, 2021.

Wananchi wakiwa katika hafla ya
uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu
Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Morogoro. Uzinduzi huo ulifanyika katika
kijiji cha Muheza Ititu wilayani Gairo, Juni 17, 2021

Mwakilishi
wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi
Elineema Mkumbo akipunga mkono kuwasalimu wananchi wa Gairo wakati wa
hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya
Tatu Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Morogoro. Uzinduzi huo uliofanyika Juni
17, 2021 katika kijiji cha Muheza Ititu wilayani Gairo. Kulia kwake ni
Mjumbe wa Bodi ya Wakala huo, Florian Haule.

Na Veronica Simba – REA

Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa
Morogoro hususani Wabunge wameipongeza Serikali kwa utekelezaji mzuri wa
Miradi ya Umeme Vijijini.

Walitoa pongezi hizo kwa nyakati
tofauti jana, Juni 17, 2021 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe
wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa
wa Morogoro, uliofanyika kijiji cha Muheza Ititu, wilayani Gairo.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha
Mgeni Rasmi Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, Mkuu wa Mkoa huo,
Martin Shigela alitoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi
wake mzuri uliowezesha sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya nishati
kuendelea kufanya vizuri.

Akifafanua, alisema kuwa
alipokabidhiwa Ofisi Machi 15 mwaka huu, idadi ya vijiji vilivyokuwa na
umeme mkoani humo ni 433 na kuongeza kuwa amefarijika kuona Waziri
Kalemani ameenda kuwakabidhi rasmi Wakandarasi kwa ajili ya kumalizia
vijiji 235 vilivyobaki.

“Mheshimiwa Waziri, tufikishie
shukrani zetu kwa Mheshimiwa Rais na tunamwahidi kuwa umeme huu unaenda
kuleta tija kwa maisha ya wananchi wa Morogoro.”

RC Shigela alisema kuwa wananchi wa
Morogoro watautumia umeme huo pamoja na mambo mengine kuanzisha viwanda
vya kuongeza thamani ya mazao ambayo wanazalisha kwa wingi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kilosa
ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi
alibainisha kuwa alipochaguliwa kuwa Mbunge, alikuwa akilionea wivu
jimbo la Gairo kutokana na kuwa na vijiji vingi zaidi vyenye umeme,
lakini sasa anafarijika kuona kwamba vijiji 63 vya jimbo lake vitapata
umeme kupitia Mradi uliozinduliwa.

Haya ni mapinduzi makubwa ambayo tunajivunia sana, ” alisema Prof. Kabudi.

Aidha, aliwataka Watanzania
kujivunia mafanikio iliyopata katika usambazaji umeme vijijini kwani kwa
sasa ndiyo kinara wa kupeleka umeme vijijini katika Bara la Afrika.

“Watanzania hatupendi kujisifia.
Hizi siyo zama za kusubiri kusifiwa. Ukifanya jambo zuri usisubiri
wakusifu. Jisifu mwenyewe. Na kwa hili tunastahili kujisifu, ” alisema.

Naye Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby
alibainisha kuwa kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali, vijiji
ambavyo havijapata umeme katika jimbo lake vimebaki saba tu na
wakandarasi wanaendelea na kazi.

“Niwapongeze sana REA na TANESCO.
Wamefanya kazi kubwa sana. Hata mimi mwenyewe na ubunge wangu huu, kuna
baadhi ya maeneo sikuwahi kutegemea umeme utafika lakini umefika.”

Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Dennis
Londo pamoja na kuipongeza Serikali, alisema kuwa anaamini uwepo wa
umeme utawezesha mapinduzi katika sekta zote za uzalishaji na hivyo
kuwawezesha wananchi kupambana na umaskini.

Mbunge wa Morogoro Kusini, Innocent
Kalogeris alisema amefarijika kuona ahadi zilizoahidiwa na Chama chake
(CCM) wakati wa kampeni zinaendelea kutekelezwa kwa kasi.

“Katika jimbo langu la Morogoro
Kusini, vijiji ambavyo vinakwenda kupata umeme kupitia mradi huu ni 51.
Huu ni ushindi mkubwa sana kwetu,” alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo,
Waziri Kalemani alibainisha kuwa uzinduzi huo ni moja ya matukio ya
mafanikio makubwa ya Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kusambaza
nishati vijijini kwani ni ukamilishaji wa ngwe ya mwisho ya kupeleka
umeme katika vijiji vilivyosalia.

“Itakapofika Desemba 2022, Tanzania itaandika historia katika vitabu vyake kuwa vijiji vyote vya Tanzania Bara vimepata umeme.

Aidha, Waziri alibainisha kuwa
Serikali imetenga takribani shilingi bilioni 66.8 kwa Mkoa wa Morogoro
pekee ili kuhakikisha vijiji vyote 233 vilivyosalia bila umeme kati ya
673 vilivyopo, vinapatiwa nishati hiyo.

Hafla hiyo ya uzinduzi ilihudhuriwa
na viongozi pamoja na wataalam wengine mbalimbali kutoka Wizara ya
Nishati, REA na TANESCO na wananchi.