Wafanya biashara 10 kutoka rwanda watinga kuwekeza mkoani kagera


Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia jenerali Elisha Marco Gaguti akiwa katika picha ya pamoja na wafanya biashara kutoka Rwanda Na Lydia Lugakila – Malunde 1 blogKundi la Wawekezaji 10 ambao ni
Wamiliki wa makampuni mbalimbali ya biashara nchini Rwanda walioamua
kuunda Kampuni moja ya uwekezaji wamewasili mkoani Kagera ili
kuchangamkia fursa ya uwekezaji mkoani Kagera katika Sekta ya ufugaji wa
kisasa na kuanzisha kiwanda cha kusindika nyama.


Wawekezaji hao wamewasili mkoani Kagera leo Septemba 11,2019 na
kupokelewa na Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti ili
kumweleza nia yao na kuwa wapo tayari kuwekeza katika ufugaji na kiwanda
cha kusindika nyama.


Ujio wa wawekezaji hao ni sehemu ya Jitihada za viongozi wa mkoa wa
Kagera kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha uchumi wa nchi za Afrika
Mashariki ikiwa ni mafanikio yaliyopatikana kutokana na Wiki ya
Uwekezaji Kagera kumalizika hivi karibuni iliyolenga kuonesha fursa
mbalimbali za uwekezaji mkoani humo.


Kiongozi wa wawekezaji hao kumi kutoka nchini Rwanda,William Kawamala
amemweleza Mkuu wa Mkoa Gaguti kuwa wapo tayari kuwekeza katika sekta ya
ufugaji wa kisasa wa ng’ombe katika Kampuni za Ranchi za Taifa
(NARCO) baada ya kupata fursa hiyo katika Wiki ya Uwekezaji Kagera
iliyofanyika tarehe 12 hadi 17 Agosti, 2019.


“Sisi baada ya kushiriki Wiki ya Uwekezaji Kagera tulivutiwa kuwekeza
katika Sekta ya ufugaji, na tuliporudi kwetu nchini Rwanda tulikaa
pamoja na kukubaliana tujiunge kwa pamoja wafanyabiashara kumi ili
kuanza uwekezaji mara moja, ndiyo maana tupo hapa ili kuanza hatua za
awali pia tumekuja kuona maeneo ya kufugia na kuweka kiwanda”,
amefafanua Kawamala.


Amesema baada ya kuona maeneo wanataka kuwekeza katika ufugaji wa kisasa
wa ng’ombe, ujenzi wa kiwanda cha kuchinja na kusindika nyama kwa
viwango vya kimataifa.


“Kwa sasa baadhi ya Hoteli kubwa nchini Rwanda zimeanza kuagiza nyama
kutoka nchi za Ulaya wakati tukifuga kisasa hapa Kagera tunaweza
kuilisha Rwanda”, ameongeza Kawamala.


Mkuu wa Mkoa Gaguti amewakaribisha wawekezaji hao na kusema kuwa mkoa upo tayari kuwapa ushirikiano.


Amesema tayari amemwelekeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NARCO Prof.
Philemon Wambula pamoja na baadhi ya wataalam kutoka Sekretarieti ya
mkoa kuwaonesha maeneo yaliyotengwa ili wakubaliane nayo na taratibu
za kusajili kampuni na kuanza uwekezaji zianze mara moja.


“Baada ya Wiki ya Uwekezaji mwitikio umekuwa mkubwa sana wa wawekezaji
kuja kwetu kuchangamkia fursa zilizopo Kagera na sisi tumejipanga
tunawapokea na kuwaelekeza taratibu za uwekezaji, lakini jukumu letu ni
kuhakikisha fursa zote ambazo wawekezaji wameziona wanazitumia katika
uwekezaji ili kukuza uchumi wa mkoa wetu” ,amesema Gaguti.


Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni za Ranchi za Taifa (NARCO),Prof.
Philemon Wambula amesema mkoa wa Kagera bado una fursa kubwa za
uwekezaji katika sekta ya mifugo hasa katika viwanda vya kusindika nyama
na maziwa pia uwekezaji katika malisho ya mifugo aidha, NARCO bado
inayo maeneo makubwa ya kuwekeza. 
Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia jenerali Elisha Marco Gaguti akiwa na wafanya biashara kutoka Rwanda ofisini kwake leo.
Kiongozi wa wawekezaji kutoka nchini Rwanda William Kawamala akitoa
zawadi kwa Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Elisha Marco Gaguti
leo mkoani Kagera.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Elisha Marco Gaguti akiwa na wawekezaji kutoka Rwanda leo mkoani Kagera.

Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia jenerali Elisha Marco Gaguti akiwa katika picha ya pamoja na wafanya biashara kutoka Rwanda