Wafungwa 150 kutoka katika mikoa ya mwanza, shinyanga na tabora wapelekwa gereza la kwitanga mkoani kigoma kulima michikichi

Wafungwa
150 kutoka katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora wamepelekwa
katika Gereza la Kwitanga Mkoani Kigoma ikiwa ni mkakati maalumu wa
Serikali kuliteua gereza hilo kuwa Kituo Kikuu cha Uzalishaji wa zao la 
mchikichi nchini.


Hayo
yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad
Masauni wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mkakati huo uliotolewa
maagizo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katikati ya mwaka 2018 alipofanya
ziara gerezani hapo  ukiwa na lengo la kulifanya Jeshi la Magereza
kuingia katika mfumo wa uzalishaji mali.

“Katika
kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambalo ni agizo la
serikali, wizara tumeongeza nguvukazi hapa kwa kuleta wafungwa 150 na
muda si mrefu tutaongeza wafungwa wengine 300 kutoka magereza mbalimbali
nchini ili kuweza kuongeza uzalishaji huku eneo lenye ukubwa wa ekari
6000 linatarajiwa kulimwa zao hilo sambamba na kusambaza mbegu
zinazozalishwa gerezani hapo kwenda Halmashauri za Mikoa, Taasisi za
Umma, Asasi za Kiraia na Sekta Binafsi,” alisema Masauni

“Lakini
pia ili kuliwezesha gereza hili tumeliagiza Shirika la Uzalishaji Mali
la Jeshi la Magereza kulichukua Gereza la Kwitanga na kuliingiza katika
kundi la magereza yanayowezeshwa na shirika ili kuweza kutatuliwa
matatizo yao ya kifedha badala ya kusubiri bajeti kuu kutoka serikalini
ambayo inakua haitoshi.

Akizungumza
katika ziara hiyo, Mkuu wa Magereza mkoani Kigoma, Kamishna Msaidizi
Leonard Bushiri aliunga mkono hoja ya Gereza Kwitanga kuchukuliwa na
Shirika la Uzalishaji Mali huku akikiri baadhi ya masuala kukwama
kutokana na changamoto za kibajeti.

“Nafikiri
hili suala la gereza kuchukuliwa na Shirika la Uzalishaji Mali
litatatua changamoto nyingi za kibajeti na kiuendeshaji maana gereza
halina gari kubwa kwa ajili ya uvunajina usafirishaji wa mafuta kutoka
gerezani kwenda kwa mtumiaji, hakuna bajeti ya uendeshaji kwa mfano
kukamua lita 100 mpaka 120 za mafuta tunahitaji maji lita 1000 hivyo
fedha kwa ajili ya kununulia umeme ili kusukuma maji ni changamoto,
kwahiyo kuingizwa kwenye shirika itasaidia changamoto nyingi” alisema
ACP Bushiri

Sambamba na kulima zao la mchikichi Gereza Kwitanga linalima pia mahindi, mpunga, mihogo, maharage na Bustani za mbogamboga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *