Wajumbe wa kikao kazi Serikali Mtandao watakiwa kuwa wabunifu

Na, Egidia Vedasto

APC Media, Arusha.

Katika kikao kazi cha tano cha serikali mtandao kilichofanyika Jijini Arusha, ubunifu umesisitizwa zaidi ili kuboresha sekta ya sayansi na teknolojia katika matumizi ya Serikali mtandao (eGA).

Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amehimiza wataalam wa serikali mtandao kuwa wabunifu na kuimarisha ushirikiano kati yao na sekta binafsi.

“Kwa kuzingatia mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, yanayohitaji ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yetu, ikiwemo katika kusanifu na kujenga mifumo ya TEHAMA itakayowezesha kuboresha utendaji kazi katika taasisi zetu, na utoaji wa huduma kwa wananchi, naielekeza e-GA kuendelea kufanya tafiti ili kuleta bunifu za Mifumo ya TEHAMA, ambayo sio tu itaboresha utendaji kazi bali pia itasaidia kuondoa kero za upatikanaji wa huduma mbalimbali za Serikali kwa wananchi”,

“Napenda kuwakumbusha Maafisa Masuuli kuweka mazingira mazuri na wezeshi, ya kufanikisha utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao, kwa kuwawezesha Maafisa TEHAMA kupata mafunzo ya mara kwa mara” ameeleza Simbachawene.

Amesema kuwa vikao hivo vimekuwa na manufaa makubwa ya utekelezaji za serikali mtandao kutokana na mawazo mazuri yanayopatikana kutoka kwa washiriki wa vikao hivo.

“Tunajivunia kuona kuwa, idadi ya watumiaji wa simu za mkononi pamoja na internet, inaongezeka mwaka hadi mwaka, ongezeko hili linatupa chachu ya kuboresha upatikanaji wa huduma za Serikali kupitia simu za mkononi, hivyo, taasisi za umma zinapaswa kuchukua hatua za haraka, ili kuhakikisha zinatumia fursa ya ongezeko hili, kuboresha utoaji wa huduma zenu kwa wananchi kidijitali kupitia simu za mkononi” amefafanua Simbachawene.

Aidha, ameongeza kuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imejipanga kuboresha utendaji kazi katika taasisi za umma, pamoja na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma mtandao kwa umma kidijitali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba, amesema
Mamlaka inaahidi kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo miongoni mwa Taasisi za Umma na Binafsi, ambao ni wadau muhimu wa serikali mtandao, ili kwa pamoja waweze kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii kupitia TEHAMA.

“Niwahakikishie washiriki wote mliopo hapa kuwa, Mamlaka itaendelea kushirikiana na Taasisi za Umma katika Kubuni, Kusanifu na Kujenga Mifumo mbalimbali ya TEHAMA, itakayosaidia kutatua changamoto zilizopo katika jamii yetu, itakayowezesha Serikali kutoa huduma kwa wananchi kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu zaidi” ,

“Pamoja na hayo kama Mamlaka tumejiwekea mikakati kwa lengo la kuhakikisha Serikali Mtandao inaimarika, niiombe Serikali kupitia Wizara, kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu, katika kuhakikisha Serikali ya kidijitali inafanikiwa zaidi” amesema Mhandisi Ndomba.

Vilevile Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Dkt. Jasmine Bunga ameeleza kuwa katika kikao hicho wamepata fursa ya kujadiliana kwa pamoja, kuhusu mbinu za kuboresha na kukuza jitihada za Serikali Mtandao nchini, Kupitia majadiliano yaliyotokana na mada mbalimbali zilizowasilishwa, washiriki hao wameweka maazimio, ambayo Mamlaka itasimamia utekelezaji wake na kutoa mrejesho kwenye kikao kazi kijacho.

“Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ipo tayari kupokea maelekezo yoyote kwa ajili ya utekelezaji, sambamba na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuijenga Serikali ya Kidijitali, ambalo tunaamini litafikiwa kupitia jitihada za serikali mtandao zilizo imara na thabiti” amesema Dkt. Bunga.

Kikao hicho muhimu kilichofanyika kwa siku tatu, kimejumuisha Wadau wa Serikali Mtandao takriban 1,000 kutoka katika taasisi mbalimbali na kubeba kaulimbiu “Jitihada na Ubunifu wa Serikali Mtandao kwa Utoaji wa Huduma za Umma kwa Ufanisi” .