Wakandarasi mradi wa maji same-mwanga watakiwa kuongeza kasi

Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa maji wa Same-Mwanga wametakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wake ili ukamilike kwa wakati.Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ametoa maelekezo
hayo Septemba 28, 2019 wakati wa ziara yake iliyolenga kukagua hatua ya
ujenzi iliyofikiwa na Wakandarasi wanaotekeleza mradi huo ambao ni
kampuni ya M.A Kharafi & Sons na kampuni ya Badr East Africa
Enterprises.

Mara
baada ya kujionea shughuli zilizokuwa zikiendelea na kupokea taarifa ya
mradi kutoka kwa wakandarasi hao, Mhandisi Sanga alieleza kutoridhishwa
na kasi ya utekelezwaji wake na aliwasisitiza kuhakikisha kuwa mradi
unakamilika kwa wakati.

Mhandisi
Sanga aliwataka Wakandarasi kuwa wepesi kwenye kufanya mawasiliano na
Wizara kila wanapokutana na changamoto yoyote ambayo ipo nje ya uwezo
wao ili ufumbuzi upatikane haraka bila kuchelewesha shughuli za ujenzi
wa mradi.

“Sijaridhishwa
na kasi yenu ya ujenzi wa mradi. Kama kuna changamoto mnakutana nazo
zilizo nje ya uwezo wenu mhakikishe mnawasiliana na Wizara mapema
iwezekanavyo ili tupate ufumbuzi,” alisema Mhandisi Sanga.

Aliongeza
kwamba Serikali inachohitaji ni kuona matokeo na haipo tayari
kumvumilia mkandarasi ambaye anachelewesha mradi bila ya kuwa na sababu
za msingi.

“Wanachohitaji
wananchi ni maji, Serikali haitomvumilia Mkandarasi ambaye atashindwa
kwenda na kasi inayokubalika,” alibainisha Mhandisi Sanga.

Mhandisi
Sanga vilevile aliwakumbusha wakandarasi hao kuhakikisha manunuzi ya
vifaa vinavyohitajika kwenye ujenzi wa mradi huo yanafanyika hapa nchini
badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi hasa ikizingatiwa kwamba vingi
vinapatikana hapa hapa Nchini.

Wakandarasi
hao kwa nyakati tofauti walimuahidi Naibu Katibu Mkuu Sanga kuongeza
kasi ya utekelezaji wa mradi sambamba na kuzingatia maelekezo
aliyoyatoa.

Mradi
wa Same-Mwanga ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa na
Serikali kwa lengo la kuondoa kero ya maji kwa wakazi wa Miji ya Same na
Mwanga, Mkoani Kilimanjaro na baadaye Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga.

Ziara
hiyo ya Naibu Katibu Mkuu Sanga kwenye mradi huo ni ya kwanza tangu
ameteuliwa na kuapishwa kushika wadhifa huo Septemba 22, 2019