Wakulima mboga mboga na matunda wataja changamoto zinazowakwamisha

Msimamizi wa Miradi wa taasisi ya
TCRS mkoa wa Morogoro,Rehema Samweli, akizungumza na wakulima wa kijiji
cha Diovuva, kata ya Kiloka, Halmashauri ya Morogoro vijiji.
Baadhi ya wakulima wakimsikiliza
kwa makini Msimamizi wa Miradi wa taasisi ya TCRS, mkutano uliolenga
kubaini changamoto zinazowakabili na kutafuta nmana ya kuwaunganisha na
masoko ya mijini.
NA VICTOR MAKINDA. MOROGRORO
 Wakulima wa mboga mboga na
matunda wa kijiji cha Diovuva kata ya Kiloka, Halmashauri ya Morogoro
vijijini wamesema kuwa wanakabiliwa na changamoto lukuki zinazo kwamisha
juhudi zao za kujikwamua kiuchumi kupitia sekta ya  kilimo, sekta
inayoajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania.
Wakizungumza katika mkutano wa
wakulima hao uliondaliwa na Taasisi ya kuwahudumia wakimbizi ya
Tanganyika (TCRS), mkutano uliolenga kuzibaini changamoto za wakulima
hao na kutafuta namna ya kuzitatua, wakulima hao walisema kuwa ukosefu
wa soko la uhakika, bei duni ya mazao sambamba na ujazo mkubwa maarufu
kama rumbesa ni miongoni mwa changamoto zinazo wakabili.
“ Sisi wakulima wa mboga mboga na
matunda wa kijijini hapa tunakabiliwa na changamoto nyingi. Kubwa ni
kukosa soko la uhakika la kuuza mazao yetu. Kijiji hiki hakina soko.
Lipo gulio tu ambalo hufanya kazi mara mbili kwa wiki. Kama ujuavyo
baadhi ya mazao tunayozalisha huoza haraka. Tunaposubiri siku mbili kwa
wiki kwa ajili ya kuuza mazao hayo kwenye gulio hutusababishai hasara ya
kuoza au tunauza kwa bei ya chini kwa kuhofu kuwa hakuna mahali na siku
nyingine tunawez kuuza. Alisema  Siraji Rajabu mkulima wa Nyanya
kijijini hapo.
 Siraji aliongeza kusema kuwa
ukosefu wa barabara ya uhakika ya kusafirishia mazao yao ni kikwazo
kingine kinachowafanya kuuza mazao yao kwa bei ya chini hali
inayowasababishia hasara.
 Naye Kudra Jumanne mkulima wa
mboga mboga wa kijijini hapo alisema kuwa ukosefu wa huduma za ugani ni
miongoni mwa changamoto zinazowakabili na kupelekea kuzalisha kwa hasara
kwa kuwa mazao yao hushambuliwa na wadudu.
 “ Sijui kama tunaye afisa ugani
hapa kijiji kwetu. Hatumjui na hatijawahi kupata huduma zake. Tunalima
kienyeji tu, hatujui namna sahihi ya kutumia mbegu, madawa ya kuulia
wadudu na mbole. Mazao yetu yanashambuliwa sana na wadudu.Hatujui nani
tumweleze kwa kuwa ukimtafuta mtaalamu wa kilimo kwa ajili ya kupata
maelezo ya  kitaalamu hapatikani. Alisema Kudra.
Naye Imani Idy mkulima wa vitunguu
saumu na tangawizi kijiji hapo alilalamikia ujazo mkubwa wa mazao
maarufu kama lumbesa kuwa ni kikwazo kwa ukuaji wa uchumi wao.
 “Wanapokuja wanunuzi siku ya
gulio, ni tatizo kubwa. Hawataki ujazo wa kawaida. Kinyume chake
wanatutaka wakulima kujaza lumbesa. Lumbesa inatufanya kuuza mazao mengi
kwa bei ndogo ambayo haifanani na gharama za uzalishaji. Tunashangaa
serikali ya kijiji na kata wamekaa kimya kuhusu kadhia hizi ambazo
wakulima tunazipata. Alisema Imani.
Akizungumzia changamoto hizo,
Diwani wa kata ya Kiloka, Jamila Taji, alisema kuwa ni kweli wananchi wa
kijiji  hicho wanakabiliwa na changoto ya barabara ya Kiloka Diovuva,
ambayo haipitiki hasa masika, ukosefu wa soko la kijiji. Yeye kama
diwani amekuwa akisisitiza masuala hayo katika vikao ya Halmashauri  kwa
kipindi kirefu na kwa sasa mipango ya ujenzi wa soko na barabara hiyo
ipo mbioni. 
“ Kuhusu huduma za ugani yupo
mtaalamu wa kilimo wa kata, lakini hakuna wa kijiji. Labda wakulima
hawamtumii lakini yupo  na ninaahidi kumsukuma aende kwa wananchi
kuwahudumia. Na hili la ujazo wa lumbesa nitamwelekeza mtendaji
kufuatilia. Alisema Taji.
 Msimamizi wa miradi wa shirika la
TCRS mkoani Morogoro, Rehema Samweli akieleza madhumuni ya mkutano huo,
alisema kuwa shirika lake limedhamiria kuwasaidia wakulima wa kijiji
hicho kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo changamoto ya
masoko kwa kuwaunganisha na wafanyabisahara wa mijini ili wawe na 
uhakika wa kuuza mazao yao kwa kwa bei yenye tija.