Na Joctan Myefu , Njombe
WASIMAMIZI (Farm Managers) 70 kutoka kampuni tofauti za mashamba ya parachichi yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 900 mkoani Njombe wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kufanya kilimo hai ili kuweza kuzalisha kisasa na kupata mazao mengi zaidi.
Mafunzo hayo yaliyotolewa na kampuni ya Guavay pia yalilenga kuwajengea uwezo maafisa hao kuweza kuongeza thamani na ubora utakaokuwa na ushindani katika soko la ndani na nje ya Tanzania.
Mkurugenzi wa kampuni ya Guavay, Ahadi Katela amesema kampuni yake imelazimika kutoa elimu hiyo ya kilimo hai kwa wakulima ili kutengeneza soko la uhakika ndani na nje ya Tanzania na kuwawezesha wakulima wa Tanzania kiuchumi zaidi.
Christina Myonga msimamizi wa shamba la shule ya sekondari Mtwango na Yohanes Nyawike ni baadhi ya wanufaika wa mafunzo ya kilimo hai ambao wanasema kwa kipindi kirefu wamekuwa wakipata mazao duni kutokana na kutozingatia taratibu za kilimo hicho na kwamba elimu hiyo inawafanya kwenda kufanya mapinduzi huku pia wakiomba wataalam wa serikali na taasisi za kilimo kuendelea kuwatembelea na kuwaelimisha.
Nae muwezeshaji wa mafunzo hayo Musa Joshua amesema mbali na kutoa elimu kwa wasimamizi lakini amewashauri wawekezaji wakubwa na wadogo kuhakikisha wanaweka mazingira bora na rafiki kwa mnunuzi na mfanyakazi ili kuongeza hamasa kwa wengine .