Waliovamia mpaka wa tunduma watii agizo la rais la kubomoa

Wananchi waliovamia Mpaka wa
Tanzania na Zambia eneo la Tunduma wakitii agizo la Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na kubomoa majengo na
vibanda vyao ili kuacha wazi eneo la Mpaka huo.
Zaidi ya asilimia 80 ya Wananchi
waliovamia Mpaka wa Tanzania na Zambia eneo la Tunduma wametii agizo la
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na
kubomoa majengo na vibanda vyao ili kuacha Mpaka wazi.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen.
Nicodemus Mwangela ameyasema hayo mara baada ya kukagua maendeleo ya
utekelezaji wa agizo la Rais na kukuta wananchi wametii na wamebomoa.
“Ninawapongeza wananchi wa
Tunduma kwakuwa wameitikia agizo la Rais na utekelezaji unakwenda vizuri
sana, nyumba na vibanda vingi vimebomolewa na watu wanahamisha bidhaa
na vifaa ambavyo watavitumia wakienda sehemu nyingine, hivyo
ninawapongeza sana kwa Mwitikio mzuri.”, amesema Brig. Jen. Mwangela.
Ameongeza kuwa kutokana na
kuridhishwa na kasi ya kubomoa ameamua kuwaongezea siku tatu ambazo
zitatumika kumalizia kuhamisha bidhaa na vifaa kutoka katika eneo la
mpaka na baada ya hapo chochote kitakachobaki hapo kitabomolewa na
serikali.
Brig. Jen. Mwangela amesema
wananchi waliobaki wanapaswa kuondoka na kuacha Mpaka wazi kwakuwa
vyombo vya Ulinzi na Usalama kwenye mipaka waweze kutekeleza majukumu
yao bila bila kukwamishwa na kituo pia hakutaruhusiwa shughuli za
biashara katika eneo la Mpaka.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Songwe George Kyando amesema Jeshi la Polisi limerahisishiwa namna ya
kupambana na uhalifu na kuzuia Magendo kutokana na kushafishwa eneo la
mpaka.
Kyando amesema anampongeza Rais
Magufuli kwa amri ya kusafisha mpaka huo kwani hali ya amani itazidi
kuimarika katika eneo hilo na pia ameshuhudia zoezi la kubomoa
likifanyika kwa amani.
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Songwe
Philon Kyetema amesema kabla ya usafishaji wa Mpaka, zoezi la kupambana
na wahamiaji haramu lilikuwa gumu kwakuwa walikuwa wanaweza kuingia na
kutoka nchi jirani kwa urahisi kupitia vichochoro.
Amesema Wananchi wa Tunduma
wategemee hali kuimarika Zaidi kwakuwa sasa wataweza kufanya ukaguzi
wakati wote na kwa kutumia njia mbalimbali kama magari pikipiki na hata
kwa miguu kwakuwa wamerahisishiwa mazingira ya kufanyia kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *