Wameondoka majenerali wa sekta binafsi tanzania

Na Paul R.K Mashauri




 Pichani
juu kushoto ni Elvis Tables Musiba, Ali Mufuruki na pichani chini kulia
ni Sir. Andy Chande, Ruge Mutahaba pamoja na Dkt.
Reginald Mengi enzi za uhai wao.




Miaka michache
iliyopita tulimpoteza Elvis Tables Musiba aliyekuwa Mwenyekiti wa TPSF (Tanzania
Private Sector Foundation). Mwaka jana tukampoteza Sir. Andy Chande aliyekuwa
kiongozi wa sekta binafsi toka enzi za ukoloni. Mwaka huu tumewapoteza
wafanyabiashara 3 wakubwa ambao walikuwa viongozi na watu muhimu sana kwa sekta
binafsi Tanzania. Dr. Reginald Abraham Mengi aliyekuwa Mwenyekiti wa CTI
(Confederation of Tanzania Industries) na TPSF, Ruge Mutahaba aliyekuwa mjumbe
wa MOAT (Media Owners Association of Tanzania) na mjumbe wa TRA Stakeholders
Forum na jana tumempoteza Mr. Ali Mfuruki aliyekuwa Mwenyekiti wa CEO Round
Table.






Vijana wengi
wamewaona na kuwasikia hawa watu “the generals” lakini wengi hawajui
historia ya sekta binafsi Tanzania na mchango wao katika kuifikisha sekta
binafsi hapo ilipo. Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipoeleza japo kwa kifupi
mchango wao kwa sababu kwa namna moja au nyingine wote hawa kuanzia Sir. Andy
Chande, Elvis Tables Musiba, Dr. Reginald Abraham Mengi, Mr. Ali Mfuruki na
Ruge Mutahaba nimefanya nao kazi za sekta binafsi kwa karibu sana.






Sir. Andy Chande nilifanya
naye kazi akiwa ni Mwenyekiti wa “boards” mbalimbali za taasisi kama
MOI, IMTU, TRL nk. Na pia alikuwa mshauri katika “board” ya kampuni
yangu mwenyewe. Ni bahati mbaya sana kwamba mwezi moja kabla ya kifo chake,
mimi na Sir. Andy Chande tulipanga kukutana ili mimi Paul Mashauri nimfanyie
“interview” ya namna sekta binafsi ya nchi hii ilivyokuwa kabla na
baada ya uhuru. “Interview” ile ilikuwa itumike kama kipindi cha TV
ili wengi zaidi wanufaike na uzoefu aliokuwa nao. Bahati mbaya Sir. Andy Chande
alifariki kabla hatujakamilisha jambo hilo jema.






Elvis Tables Musiba
nilifanya naye kazi akiwa Mwenyekiti wa TPSF na mimi nikiwa mjumbe wa kamati
mbalimbali za sekta binafsi Tanzania. Tulisaidiana kuchangisha
fedha”fundraising” kwa shughuli mbalimbali za kitaifa, na alitumia
wakati huo kunisimulia mambo mengi sana.






Mr. Ali Mfuruki
nilifanya naye kazi akiwa ni Mwenyekiti wa CEO Round Table na mlezi wa TRBN
(Tanzania Responsible Business Network) chini ya UN Business Compact na mimi
nikiwa ni mjumbe wa “secretariat” ya TRBN.






Dr. Reginald
Abraham Mengi nilifanya naye kazi yeye akiwa ni Mwenyekiti wa CTI na mimi
nikiwa ni mjumbe wa kamati ya SME ya CTI. Na Ruge Mutahaba nilifanya naye kazi
wote tukiwa wajumbe wa TRA Stakeholders Forum.






Mara nyingi wote
hawa walitumia muda wao mwingi kunisimulia vitu vingi sana wao wakiwa wakubwa
kwangu kiumri na mimi nikiwa mdogo sana kwao. Wakati huo nilikuwa sijui kwanini
wananiambia mambo yote hayo ya sekta binafsi kwa sababu kwanza nilikuwa mdogo
sana na pili sikuwa na nafasi wala heshima kubwa kama walizokuwa nazo wao
lakini jana baada ya kupata taarifa za kifo cha Mr. Ali Mfuruki nikagundua
pengine walitaka siku moja niyasimulie hayo ili kizazi cha leo kipate kuelewa.






Wafanyabishara
vijana, viongozi vijana katika serikali na wajasiriamali vijana wanaochipukia,
lazima waelezwe kwamba historia ya sekta binafsi Tanzania haiwezi kuelezwa
pasipo majina ya hawa wote niliowataja hapo juu. Lakini pia wapo wengine ambao
wameshatutoka na wengine ambao bado wapo hai. Pia sitatenda haki nisipowataja
japo baadhi yao. Hao ni pamoja na marehemu Mzee Mwakitwange, Dr. Reginald
Abraham Mengi, Mzee Anorld Kileo, Dr. Juma Mwapachu, Elvis Tables Musiba, Mzee
Iddi Simba na wengine ambao sikupata kuwafahamu. Hawa walikuwa waanzilishi wa
TCCIA mwishoni mwa miaka ya 80 kabla ya baadhi yao kuondoka TCCIA na kuanzisha
CTI. Kwanini waliondoka na TCCIA kuanzisha CTI? Hiyo ni mada nyingine ambayo
inahitaji makala tofauti na hii.






Ukiondoa Mzee
Mwakitwange ambaye alitangulia mbele za haki zamani kidogo, wengine wote
akiwemo Mzee Anorld Kileo, Dr. Juma Mapachu na Mzee Iddi Simba nimepata kufanya
nao kazi na kupata simulizi zao. Mzee Anorld Kileo ambaye alikuwa ni CEO wa TBL
kwa muda mrefu sana na kiongozi wa TPSF yeye aliniita ofisini kwake na kunikalisha
chini kwa masaa zaidi ya 3 akinieleza sekta binafsi ilipotoka na namna
walivyopambana kuifikisha hapo ilipo. Ukurasa huu hautoshi kuandika historia
yote ya ujasiriamali Tanzania ambayo vijana wengi wangependa kuijua lakini Dr.
Juma Mwapachu aliandika kitabu chenye historia hii vizuri sana. Mimi nitagusia
yale niliyoelezwa na hawa “generals” wa sekta binafsi Tanzania kwa
kifupi sana.






1.     Sir. Andy Chande,
Mwanzilishi, Chande Mills






Sir Andy Chande
alinieleza kwamba baada ya Uhuru wa nchi hii, Rais wa kwanza wa Tanzania Mwl.
Julius K. Nyerere alitaka kumteua kwenye baraza la mawaziri. Lakini akamwambia
Mwalimu Nyerere, naomba uniache kwenye sekta binafsi. Mwalimu Nyerere
aliheshimu mawazo ya Sir. Andy Chande. Lakini Mwalimu Nyerere akaamua kumteua
Sir. Andy Chande kuwa mjumbe wa kamati ya uchumi na maendeleo mara tu baada ya
Tanzania kupata uhuru. Kwa vijana wasiomfahamu Sir. Andy Chande huyu ndiye
aliyekuwa mfanyabiashara wa kitanzania mwenye nguvu kubwa za kiuchumi wakati wa
ukoloni na hata baada ya kupata uhuru. Aliendesha biashara ya kifamilia
iliyoitwa Chande Mills ambayo baadaye ilitaifishwa na serikali mwaka 1967
wakati wa “Nationalization” na kuwa NMC (National Milling
Corporation) kiwanda ambacho baadaye kilikuja kununuliwa na Bakhresa.






Sir. Andy Chande
ndiye aliyekuwa mtanzania mwenye asili ya kiasia kuanza kutoa misaada kwa watu
(philanthropism) kuanzia wakati wa uhuru mpaka alipofariki dunia miaka michache
iliyopita. Kilichonishangaza kuhusu Sir. Andy Chande ni kwamba hata baada ya
serikali kutaifisha biashara yake, bado aliendelea kutumia mtandao wake wa watu
“network” akili na maarifa yake kuitumikia nchi. Sir. Andy Chande
ananisimulia anasema, baada ya serikali kutaifisha biashara yake, Mwalimu
Nyerere alimuita Ikulu, akamuuliza; Rafiki yangu Chande; unataka kwenda wapi
baada ya serikali kuchukua biashara yako kwa manufaa ya umma?






Sir. Andy Chande
akamuambia Mwalimu Nyerere; “sina pa kwenda”. Mwalimu akamuambia
“sasa kuanzia leo, wewe ndio utakuwa Mwenyekiti wa bodi ya kampuni hii
mpya inayomilikiwa na wananchi wote wa Tanzania. Sir. Andy Chande akajibu
” sawa Mh. Rais”. Na ikawa hivyo. Ingekuwa sisi vijana wa leo, rafiki
yako ndiyo kiongozi wa nchi au DC au Mkuu wa mkoa au Waziri, anakufahamisha
maamuzi ya serikali, tungeleta urafiki na mambo binafsi kwenye mambo ya nchi.
Lakini Sir. Andy Chande alikuwa anajua kutofautisha ni wakati gani Nyerere,
“rafiki” yake anaongea na ni wakati gani Nyerere, “Rais wa nchi
na Amiri Jeshi Mkuu” anaongea. Alikuwa anajua mipaka yake.






Kutokana na uwezo
wa Sir. Andy Chande, Mwalimu Nyerere alimpa uenyekiti wa “boards”
nyingi sana ikiwa ni pamoja na TRL, ATC nk. Pia alikuwa Mwenyekiti wa
“board” ya Kioo Ltd, Shaaban Robert Secondary School, IST, Barclays
bank, Taasisi ya walemavu buguruni nk. Siwezi kuzimaliza zote ni nyingi mno.






Nilikuwa nyumbani
kwake Upanga alipokuwa akisimulia haya. Nikamuuliza sasa uliwezaje kukubali
kuwa Mwenyekiti wa “board” ya kampuni ambayo umeihangaikia miaka
mingi na sasa si yako tena. Akasema mke wangu alinitia sana moyo. Lakini pili
kwenye biashara usiweke mambo moyoni. Ukiweka mambo moyoni utakufa. Moyoni
nikajisemea; Huyu kampuni yake aliyoisotea miaka mingi imechukuliwa. Tena siyo
kampuni yenye mapato ya shilingi milioni 10 au bilioni moja. Unazungumzia
mabilioni ya shilingi. Lakini bado maisha yakaendelea. Wewe umepoteza mteja
mmoja unataka kufunga biashara. Kwanini? Hayo ni masomo ambayo nataka vijana
wengi wayashike, kwamba;







     
I.         
Mke au mume wako
ana mchango mkubwa sana katika maisha yako ya uongozi, biashara au
ujasiriamali. Unapooa au kuolewa lazima uangalie mtu ambaye atakutia moyo
wakati ukipitia changamoto za maisha kama ilivyokuwa kwa Sir. Andy Chande. Sio
mke au mume ambaye atakukimbia ukifilisika au ukifilisiwa au ukishushwa cheo au
ukifukuzwa kazi.






Wakati Sir. Andy
Chande akiniambia haya, mke wake alikuwa ni mgonjwa na alikuwa anapata matibabu
nchini Uingereza. Pamoja na umri wao mkubwa walipendana sana na kutiana moyo.
Na mara nyingi nilipowatembelea niliona Sir. Andy Chande akimhudumia mke wake
kwa hali na mali. Kipindi hicho pia Sir. Andy Chande naye hali yake ya kiafya
haikuwa nzuri lakini hakuacha kufanya kazi. Alikuwa akiandika makala katika
magazeti mbalimbali ya Uingereza na Canada. Sir. Andy Chande alikuwa rafiki
mkubwa wa familia ya Malkia wa Uingereza-Qeen Elizabeth, Waziri mkuu wa Canada,
na Marais wastaafu akiwemo Mh. Rais Ali Hassan Mwinyi, Mh. Rais Benjamin Mkapa
na Mh. Rais Jakaya Mrisho Kikwete.






   
II.         
Somo la pili ni
kwamba ukiwa mfanyabiashara au mjasiriamali, usiweke mambo moyoni, utakufa. Sir
Andy Chande na Mwalimu Nyerere walikuwa ni marafiki wakubwa. Lakini maamuzi ya
kutaifisha biashara ya Sir. Andy Chande hayakufanywa na mwalimu kama “mtu
binafsi” ingawa yeye alikuwa ni mkuu wa nchi. Yalifanywa na serikali. Iwe
yalikuwa ni maamuzi mazuri au mabaya, Sir. Andy Chande aliyapokea na kuyaunga
mkono. Urafiki wao uliendelea na yeye aliendelea na maisha kama vile hakuna
lililotokea.






Leo ukimkopa rafiki
yako hela akakuambia hana hela za kukusaidia au hawezi kukupa ana mipango na
hela alizonazo, una “mdelete” mpaka kwenye simu yako,
“unamblock” facebook, “unamunfollow twitter, instagram na
youtube”. Ukimpigia simu rafiki yako asipopokea mara 2 au mara 3, unatuma
ujumbe mfupi; “acha ujinga pokea simu” hata hujui kama yuko
hospitali-ICU kalazwa au bafuni anaoga.



Uko wapi ujasiri wa
akina Sir. Andy Chande katika kizazi cha leo? Iko wapi nidhamu ya akina Sir.
Andy Chande katika kizazi cha wakati huu? Sir. Andy Chande ananiambia wakati
akiwa na Chande Mills, mama Maria Nyerere alikuwa akienda kiwandani kuchukua
mabaki ya mahindi kwa sababu alikuwa anafuga. Akasema mama Maria alikuwa hataki
akifika kiwandani apewe “priority” wengine wasubiri. Alikuwa anapanga
foleni kama wanawake wengine. Hata yeye alipojaribu kumshawishi ahudumiwe
kwanza alikataa. Vijana wa leo ambao ni viongozi jifunzeni kitu hapa kutoka kwa
mama Maria Nyerere. Wake au waume zenu wajishushe. Wasitake kupewa
“priority” kwa sababu tu ni wake au waume wa viongozi. Akienda benki
au saloon, mwambie na yeye apange foleni kama wengine. Ndio watu wakubwa
“great people” wanavyoishi. Hawana makuu ingawa ni wakuu.






2.     Elvis Tables
Musiba, Mwenyekiti wa zamani, TPSF






Nikiwa mtoto mdogo
nilikuwa nasoma vitabu vya Elvis Tables Musiba. Moja kati ya vitabu ambavyo
sitopata kuvisahau ni kitabu kinachoitwa NJAMA. Kitabu kile cha kipelelezi
kilikuwa kina “character” anaitwa Willy Gamba. Ulikuwa ukisoma vitabu
vya Elvis Tables Musiba ni kama unaangalia sinema ya Rambo. Nakumbuka
nilipokinunua kitabu kile sikulala usingizi mpaka nilipokimaliza. Willy Gamba
alikuwa mtu hatari sana ndani ya ile simulizi. Na Elvis Tables Musiba alikwa ni
gwiji na mwandishi mkubwa na mzuri sana. Kila ninapokutana na rafiki yangu Eric
James Shigongo ambaye pia ni mwandishi wa vitabu namkumbuka Elvis Tables
Musiba. Siku moja nitamuuliza Eric James Shigongo alipata wapi hamasa ya
kuandika vitabu. Inawezekana alisoma pia vitabu vya Elvis Tables Musiba.






Nilipokutana na
Elvis Tables Musiba nilishangaa kugundua kuwa alikuwa ana kipaji kingine cha
biashara na uongozi. Wakati tunachangisha fedha kwa ajili ya kongamano moja katika
sekta ya utalii, aliniita ofisini kwake Mirambo House karibu na ofisi za benki
ya dunia. Tulikuwa tunahitaji kuchangisha kama shilingi milioni 100. Elvis
Tables Musiba akamuomba katibu muhtasi wake amletee simu. Sikuelewa simu ya
nini kwenye kuchangisha fedha. Nilitegemea tungeshirikiana kuandika barua na
“proposals” za kuchangisha fedha. Lakini haikuwa hivyo. Simu
ilipoletwa akaanza kazi. Alikuwa anatuuliza mnataka kampuni gani ituchangie
fedha. Kwa hiyo kazi yetu ikawa ni kutaja majina ya makampuni na yeye anapiga
simu. Nilishangaa kuona Elvis Tables Musiba hahitaji tumpe namba za simu.
Alinyanyua simu na kupiga kila tulipotaja kampuni. Na alipopiga hakuongea na
katibu muhtasi au mkurugenzi wa fedha. Aliongea na CEO, Director General au
Mwenyekiti wa “board”. Namba alizipata wapi? sijui. Lakini ndani ya
saa moja tulikuwa na shilingi milioni 60.






Nikagundiua huyu si
mtu wa mchezo. Ana “connections” za ajabu. Nikamuuliza hebu niambie
haya mambo unayafanyafanyaje mbona kwangu mageni? Akasema “reciprocate”.
Hili ni neno la kiingereza linalomaanisha “rudisha wema’. Elvis Tables
Musiba aliwasaidia wengi kufika pale walipo ikiwa ni pamoja na CEOs. Kumbuka
amekuwa Mwenyekiti wa “boards” za kampuni nyingi. Wengi wa hawa CEOs
ameshiriki kuwafanyia usahili kwa wao kuwa pale. Ndio maana haikumchukua muda
kupata milioni 60. Alikuwa akiongea na watu ambao ni sehemu ya mchango wake
katika maisha ya mafanikio yao. Hii ikanifanya nimdadisi zaidi. Nikamuuliza
wewe ulianzaje biashara?






Akasema mtaji wangu
wa biashara ulitokana na kuuza vitabu. Vitabu kama NJAMA ndivyo vilivyonitoa.
Lakini nilipoanza biashara haikuwa rahisi. Mimi nilikuwa mtanzania wa kwanza
“mswahili” kumiliki “Bureau De Change”-anasema Elvis Tables
Musiba. Lakini siku moja nikiwa Musoma, nikasikia kwenye redio kwamba biashara
yangu iko mikononi mwa serikali. Kidogo nipate kichaa. Lakini sikukata tamaa
nikaanza upya. Akasema nyie vijana wa siku hizi mnalalamika mazingira magumu ya
biashara. Nawashangaa sana. Tuulize sisi. Haikuwa rahisi kama mnavyofikiria.
Kutoka kwa Elvis Tables Musiba nikajifunza yafuatayo;







     
I.         
Biashara ni
mahusiano na watu. Elvis Tables Musiba kutumia saa moja kupata milioni 60 sio
mchezo. Aliwekeza kwa watu. Leo hii kutafuta Tsh. 10,000/= ya luku ukikwama
usiku wa manane na hauna salio kwenye simu ni shughuli pevu. Unaweza ukapiga
namba zote kwenye simu yako usipate hata shilingi moja. Lakini Elvis Tables
Musiba alitumia saa moja tu kupata shilingi milioni 60. Ina maana kila dakila
alipata shilingi milioni 1.







   
II.         
Kipaji chako ndio
mtaji wako. Badala ya kulalamika huna mtaji, angalia una kipaji gani? Elvis
Tables Musiba alikuwa na kipaji cha kuandika hadithi. Ndicho kilichompa mtaji
wa kuanzisha biashara. Eric James Shigongo aliwahi kuniambia pia, kwamba kipaji
chake cha kuandika hadithi ndicho kilichomsaidia kuanzisha kampuni ya magazeti
pendwa na kudumu mpaka leo (Global Publishers). Mifano ni mingi. Bila mpira
Mbwana Samata angekuwa wapi? Bila mpira George Weah angekuwa Rais wa Liberia?
badala ya kulalamika anza na kipaji chako? Mimi nilianza kwa kuandaa
makongamano. Unaweza ukawa unaandaa harusi vizuri kila mtu anashangaa. Lakini
bado unafikiri hicho siyo kipaji. Unafikiri kipaji ni “kuimba” tu!
Mwenzako makongamano yalinipeleka mpaka Ikulu, yakanipa na mtaji wa kuanza.







  III.         
Usikate tamaa.
Elvis Tables Musiba anasema amefilisika mara nyingi katika maisha yake lakini
alipambana akarudi tena kwenye mstari. Hakujinyonga. Baadhi ya biashara zake
zilikwama. Lakini hakukata tamaa wala hakujenga chuki na watu. Kifupi,
hakutafuta mchawi. Alianza upya na kusonga mbele. Alishirikiana na watu katika
sekta binafsi na serikalini. Hiyo ndiyo roho ya “ujasiri wa mali” au
“spirit” ya ujasiriamali au “entrepreneurship”. Ni mlolongo
wa kushindwa na kushinda, kushindwa na kushinda mpaka kieleweke.






3.     Dr. Reginald Abraham
Mengi, Mwenyekiti Mwanzilishi wa IPP Group na Mwenyekiti wa zamani wa CTI na
TPSF






Dr. Reginald
Abraham Mengi alinishirikisha mwanzoni kabisa wakati akianza kuandika kitabu
chake cha “I Can, I Must, I Will”. Nakumbuka alinipigia simu akasema
njoo ofisini. Akaniambia nataka uwe sehemu ya team itakayonisaidia kukamilisha
hili zoezi. Akaniomba nimtafutie vijana wengine wa kushirikliana na Prof.
Msamali Nangoli, mwanazuoni wa Uganda aliyekuwa akiishi nchini Kenya, mwandishi
wa kitabu maarufu kiitwacho “No More Lies About Africa”. Prof.
Msalami Nangoli alikuwa rafiki mkubwa wa Nelson Mandela, mpigania Uhuru na Rais
wa kwanza wa serikali ya kidemokrasia nchini Afrika ya kusini. Akiwa gerezani,
Nelson Mandela alikuwa akisoma makala za Prof. Msamali Nangoli, makala ambazo
zilipitishwa gerezani kiujanja kama kifungashio cha chapati. Kumbuka akiwa
gerezani, Mandela hakuruhusiwa kusoma hata magazeti.






Ili kukamilisha
zoezi la kuandika kitabu cha Dr. Reginald Abraham Mengi chini ya uongozi wa
Prof. Msamali Nangoli, nilipewa “tapes” za hotuba za Dr. Reginald
Abraham Mengi nyingi sana (mabox kwa mabox) ili nizipitie. Pia tuliwahoji watu
wengi waliofanya kazi na Dr. Reginald Abraham Mengi. Bahati mbaya sana katikati
ya safari ya kumsaidia Dr. Reginald Abraham Mengi kuandika kitabu chake, Prof.
Msamali Nangoli akafariki dunia na Dr. Reginald Abraham Mengi akasitisha zoezi
kwa muda. Baadaye akapata namna nyingine ya kumalizia kitabu chake kizuri.






Tulipokuwa na Prof.
Msamali Nangoli tulimshawishi sana Dr. Reginald Abraham Mengi kubadilisha
“title” au jina la kitabu lakini alikataa. Sisi tulipendekeza kitabu
chake kiitwe; Dr. Reginald Abraham Mengi-How I became Rich; Financially,
Morally, Materially. Lakini hakutaka hata kutusikiliza. Baadaye nilikuja
kugundua tulikuwa tunakosea sana kumshawishi abadilishe jina la kitabu cha
“I Must, I Can, I Will”. Kwanini?






Kwa sababu siku
moja nikiwa nyumbani kwake Kinondoni, nilimuuliza. Kwanini “I Must, I Can,
I will”?. Akasema kwa sababu maisha ya biashara yana changamoto sana.
Akaniuliza Paul, kwani unafikiri changamoto za biashara Tanzania ni zipi.
Moyoni nikasema sasa Dr. ananiuliza swali gani “simple” namna hii. Au
anataka kupima uwezo wangu wa kufikiri? Nikamwambia kubwa ni 3. Kwanza Mitaji
au “Capital”, Pili Masoko au “Markets”, Tatu Rasilimali
Watu au “Human resource”. Akasema umekosa. Akasema kwanza Roho Mbaya,
Pili Chuki, Tatu Wivu. Nilichoka kichwa. Akasema ili ufanikiwe lazima
ukabiliane na hizi changamoto 3 nilizokutajia kisha uunganishe na hizo za
mitaji, masoko na rasilimali watu. Ndio maana ya “I Must, I Can, I
Will”. Lazima udhamirie kutoka moyoni kupambana na changamoto.






Dr. Reginald
Abraham Mengi akasema tulipotoka ni mbali kuliko tulipo. Akasema nakumbuka
wakati nimeanzisha biashara ya maji ya kunywa, nilienda kwenye maonyesho ya
sabasaba kuonyesha biashara mpya ya maji. Akasema watu waliokuwa wakipita
kwenye banda langu walikuwa wananishangaa sana. Wanasema “huyu mchaga
anapenda sana hela”. Mpaka anatuuzia maji? Kweli leo hii nchi hii
tumefikia hatua ya kuuziana maji? Dr. Reginald Abraham Mengi akasema kwa hiyo
unaweza ukaona “Kilimanjato Pure Drinking Water” imeshamiri ukafikiri
ni lelemama. Haikuwa rahisi. Bora hawa ambao wanaanza kuuza maji leo. Sisi
tulioanza tulipata shida. Kwa sababu hakuna aliyezoea kuuziwa maji. Lakini Paul
ukweli ni kwamba huwezi kushindana na mtu aliyeanza. Aliyekutangulia
amekutangulia tu!






Dr. Reginald
Abraham Mengi akaendelea kusema zaidi ya hapo kujenga sekta binafsi haikuwa
rahisi. Kumbuka historia ya nchi hii toka kipindi cha wakoloni. Toka enzi hizo
biashara zilikuwa kwa matabaka. Wa kwanza pale juu ni wazungu, wa pili waarabu
na wa tatu wahindi. Sisi wazawa wa “kiswahili” tulikuwa hatufikiriwi
kabisa kuwa “matajiri”. Kuna wakati nilinunua Mercedez Benz lakini
nilikuwa naogopa kuliendesha. Kwa sababu mifumo ya kiuchumi ilikwishakamatwa na
matabaka mengine. Kwahiyo unavyoona sekta binafsi imefika hapa ni mapambano
kwelikweli. Mswahili kumiliki kiwanda miaka ya sabini na themanini na Mswahili
kuwa kiongozi wa sekta binafsi ambayo haina waswahili wengi ulikuwa ni mtihani
ambao ilibidi kuushinda. Haikuwa kazi rahisi. Mimi Paul Mashauri nimeona na
kusimuliwa mengi pengine nahitaji kitabu kizima kuzungumza ya Dr. Reginald
Abraham Mengi. Lakini kuna mafundisho machache nataka niyataje hapa;







     
I.         
Biashara si
lelemama. Changamoto ni nyingi kuliko fursa. Lazima ubadilishe hizo changamoto
ziwe fursa ili fursa ziwe nyingi kuliko changamoto. Hii haiwezekani pasipo kuwa
na moyo mgumu “a iron heart”. Kama unataka uache kazi uanze biashara
ukifikiri ni mteremko jifikirie tena na tena na tena. Nakumbuka wakati
nimemualika Dr. Reginald Abraham Mengi kuongea na wanafunzi wa chuo kikuu cha
Dar es Salaam alirudia hilo. Akasema; “safari ya mafanikio ni kama pambano
la ngumi. Kuna makonde ya kuyakwepa, kuna makonde ya kuyazuia ambayo yakikupata
yanasambaratisha uso wako au kukuua kabisa lakini kuna wakati ambao lazima
ujibu mapigo ili ushinde pambano. Mh. Jokate Mwegelo, DC, Kisarawe, kipindi
hicho akiwa chuoni, alikuwa “Moderator” katika tukio hilo. Anaweza
akayakumbuka maneno haya.







   
II.         
Usiogope kuanzisha
njia pasipo na njia. Usiogope kuwa wa kwanza kufanya jambo ambalo wengine
wanasita kufanya. Maana yake ni kwamba “be the pioneer”. Dunia
tunayoishi iko hapa ilipo sababu ya “pioneers”. Christopher Columbus
angeogopa kusafiri kutoka Spain pengine America (New Land) ingechelewa sana
kutambulika katika uso wa dunia. Hata wewe usiwe mtu wa kusubiri wenzako
waanze. “Legends” sio wale wanao “copy na kupaste” Legends
ni waanzilishi. Kuanza sio lazima iwe ni kwenye biashara. Hata kwenye familia
yako unaweza ukawa wa kwanza kuwa “mbunge”.






4.     Mr. Ali Mfuruki,
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CEO Round Table






TRBN (Tanzania
Responsible Business Network) ilipoanza niliombwa na Partner wa KPMG Ketan
Patel pamoja na Partner wa Deloitte Joe Eshun niwe “Moderator” katika
sherehe za uzinduzi wa TRBN pale Serena Hotel. Tulikuwa na CEOs zaidi ya 300.
Mgeni rasmi alikuwa ni Mr. Ali Mfuruki, Mwenyekiti wa CEO Round Table. Baada ya
ufunguzi nilikuwa na muda wa kutosha wa kuongea na Mr. Ali Mfuruki. Jambo moja
Mr. Ali Mfuruki aliniambia ambalo sitolisahau ni kwamba lazima uwe na msimamo
na lazima ukubali kupoteza baadhi ya vitu ikiwa ni pamoja na fedha kusimamia
unayoyaamini. Akaniambia nyie vijana sasa hivi ndio mmekuwa mameneja kwenye
makampuni na viongozi wa serikali na taasisi mbalimbali. Sasa wakati mwingine
unakutana na kijana kwenye kampuni ambaye amepewa mamlaka, kijana ambaye
unaweza kumzaa anataka akuzungushe, akunyanyase ili umpigie magoti. Mimi
siwezi. Bora nikose hela kuliko kushusha heshima yangu.






Wapo vijana ambao
wanamsikia Mr. Ali Mfuruki leo hii lakini hawajakutana na Mr. Ali Mfuruki na
kuzungumza naye ana kwa ana. Sijui umesikia nini juu yake lakini Mr. Ali
Mfuruki alikuwa na msimamo wa kipekee. Alikuwa anafikiria vizuri sana sio
katika biashara zake tu hata kwa nchi. Ndio maana kifo chake kimetushtua kama
Taifa. Unaweza ukawa unafikiria vizuri lakini kwa mambo yako binafsi na familia
yako. Hilo ni jambo zuri na ndiyo jambo la pili baada ya kumfikiria Mungu.
Lakini unapojiongeza na kufikiria Taifa na watu wengine ndani ya Taifa unakuwa
wa tofauti zaidi. Ndivyo alivyokuwa Mr. Ali Mfuruki.






Kuna siku
nilikutana naye nikamuuliza Mr. Ali Mfuruki lini unaandika kitabu? Akaniambia
nimeanza kuandika. Siku niliposikia ametoa kitabu, nikawahi bookshop Mlimani
City kununua. Lakini baada ya kusoma kile kitabu nikagundua nilichofikiria kuwa
kitakuwepo kwenye kitabu sicho. Mr. Ali Mfuruki hakuwa ameandika kitabu kuhusu
yeye na mke wake na watoto wake. Alikuwa ameandika kitabu kuhusu uchumi wa
viwanda. Huyo ndio Mr. Ali Mfuruki. Ndiyo sababu alidumu kama Mwenyekiti wa CEO
Round Table kwa miaka mingi. Sio kwamba alipenda kuhodhi madaraka. Alikuwa ana
uwezo kichwani. Na vyeo vingi alikuwa anakataa. Na pale alipokubali alijitoa
kwa dhati. Amekuwa Mwenyekiti wa “boards” za Mwananchi Communications
Ltd, amekuwa kwenye “board” ya Geita Gold Miming (GGM), Mwenyekiti wa
“board” ya Vodacom nk. Waulize waliofanya kazi naye. Kile kilikuwa
kichwa kingine.






Wakati fulani
nilialikwa katika uzinduzi wa “Private Equity Fund” moja pale Golden
Tulip Hotel. Alikuwepo Mh. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Mh. Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, Waheshimiwa mawaziri na wafanya biashara. Mr. Ali Mfuruki alikuwa
miongoni mwa waalikwa pia. Siku ile Mr. Ali Mfuruki aliongea kitu kikubwa sana.
Akasema, wakati Marekani inataka kwenda mwezini miaka ya 60. Rais wa nchi hiyo
J.F. Keneddy alitangaza kwamba Mmarekani yoyote atakayekuja na wazo au
“idea” au “ubunifu” au “teknolojia” ambayo
itaisaidia Taifa la Marekani kufika mwezini au kufika hatua moja mbele katika
ndoto ya nchi kwenda mwezini, serikali ya Marekani italipa fedha kununua hilo
wazo au huo ubunifu. Mr. Ali Mfuruki akasema; ili sisi kama Taifa tuweze kwenda
mbele lazima kuwe na mbinu za kujenga “uhitaji” au “demand”
ya ugunduzi na ubunifu “Creativity and innovation” . Akasema
“kufikiria” ni kazi. Kugundua kitu ni gharama. Lazima ufanye
“research” au “utafiti”. Tukitaka watu wetu wawe wabunifu
lazima tutengeneze mbinu za kumfikirisha mtu akijua kabisa kuwa nguvu zake
hazitoenda bure.