Wanafunzi 16 na mwalimu mmoja wajeruhiwa kwa radi na kuua mmoja

Wanafunzi 16 na mwalimu mmoja wa shule ya sekondari Chief Kidulile
iliyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe wamepigwa radi februari 19 majira
ya saa tisa alasiri na kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja na kuacha
majeruhi 16.

Akifafanua kuhusu tukio hilo kamanda wa jeshi la
polisi mkoa wa Njombe Hamis Issa akiwa mkoani Morogoro kikazi amesema
amepokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa vijana wake aliowatuma ambapo 
amesema katika tukio hilo mwanafunzi mmoja wa kiume kufariki dunia
punde baada ya kukimbizwa hospitali na mwingine mmoja kujeruhiwa vibaya
mguuni na jichoni huku pia akisema wengine 15 walipata majeraha madogo .

Kutokana
na tukio hilo kamanda Issa ametoa rai kwa wananchi kuchukua tahadhali
msimu wa mvua kwa kuto tembea peku,kuweka vizuia radi na kujiepusha na
kitendo cha kukaa maeneo matupu ama ya wazi.

Seil Morel ambaye ni
mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Ludewa anasema madaktari
walipokea watu 17 ambao ni wahanga wa tukio hilo ambapo katika jitihada
za kunusuru uhai wao wamelazimika kutoa huduma usiku na mchana hatua
ambayo imekuwa na matokeo chanya kwani wanafunzi 15 wameruhusiwa asubuhi
akiwemo mwalimu huku pia akidai mmoja amefariki na mwingine mmoja
akiendelea kupata matibabu zaidi kwa kuwa amejeruhiwa vibaya .

Dr Morel amesema wanafunzi wakike 11 wamejeruhiwa katika tukio hilo ,wakiume 5 na mwalimu mmoja wa kiume .

Nae
mkuu wa shule ya sekondari Chief Kidulile Aloyce Kapelele anasema tukio
hilo limeleta mshituko mkubwa shuleni hapo kwakuwa halijawahi kutokea
na kwamba jitihada za kuweka vidhibiti radi zinafanyika huku kuhusu
wanafunzi walioruhusiwa hospitali wanaendelea na masomo kama kawaida .