Wananchi Jijini Arusha wanufaika na (Samia Legal Aid)

Na, Egidia Vedasto.

APC Media, Arusha.

Wananchi Jijini Arusha wamepongeza uwepo wa Wiki ya msaada wa kisheria (Samia Legal Aid), unaoendelea kutolewa kwa wananchi Jijini Arusha kuelekea siku ya Mwanamke Duniani, lengo likiwa ni watu wote wenye changamoto za muda mrefu kuhusu masuala ya kisheria yanatatuliwa.

Baadhi ya wananchi ambao wamepata ufumbuzi wa kero zao wamebainisha namna walivyopata majibu kwa muda mfupi bila kutoa gharama zozote.

Mmoja wa wajasiriamali katika eneo la Chuo cha Uhasibu Arusha Zita Kibao amesema”Namshukuru sana Mama Samia Suluhu Hassan kwa mkakati huu ambao umetuokoa sisi wafanyabiashara wadogo, tena bila hata kutoa fedha, nimefurahi mno maana nilifukuzwa katika eneo langu la biashara na watu waliojifanya kuwa ndio wamiliki wa eneo lile”,

“Lakini baada ya kufika hapa katika mabanda ya yanayotoa msaada wa kisheria nimewaeleza wakaniambia nikaendelee na majukum yangu kama ilivyokuwa hapo awali, wakati huo timu maalum ikijipanga kufika katika eneo hilo ili kubaini watu hao wanaotusumbua” amesema Zita.

Katika namna hiyohiyo Yusuph Mollel kutoka Wilaya ya Longido ameshukuru kutatuliwa kwa mgogoro wake wa ardhi uliodumu kwa miaka mitano.

“Nilijua pengine ntakufa bila ya kupata haki yangu kwa kuwa mimi ni mzee, lakini nina furaha kubwa kuona shida yangu inapatiwa majibu, Sitasahau kumuombea Mama Samia katika uongozi wake, ni mama mwenye huruma na upendo kwetu watu wa hali ya chini” amefafanua Mollel.

Awali akifungua maadhimisho ya wiki ya kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Jumanne Sagini amesema kupitia wiki hii ya msaada wa kisheria ya (Samia Legal Aid ) anategemea wananchi wengi watajitokeza kuleta kero zao ili zitatuliwe, hatua itakayofanya kila mmoja kufurahia siku ya mwanamke duniani na kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Nchi Samia Suluhu Hassan.

“Watu wenye uhitaji wa masuala ya kisheria ni wengi na wanaofanikiwa ni wachache kutokana, na sababu za kifedha kwa maana ya Mawakili, kusimamia kesi zao, hivyo nawasihi wananchi wa Jiji la Arusha na viunga vyake kuhudhuria wiki hii kwa wingi ili mpate msaada bila gharama yoyote” amefafanua Sagini.

Huduma ya msaada wa kisheria (Samia Legal Aid) chini ya Wizara ya Katiba na Sheria itahitimishwa Machi 07, ili kupisha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika Machi 08 Jijini Arusha