Wananchi kata ya kibasuka walalamikia upatikanaji wa maji safi na salama.

Na Mwandishi wetu Tarime.


Wananchi kata ya Kibasuka wilayani Tarime mkoani Mara wanalazimika kuchota maji ya mtaro kando kando ya barabara kutokana na kutembea mwendo mrefu kutafuta maji ya bomba jambo ambalo linasababisha  baadhi ya familia kusambaratika.

Wakiongea na Arusha blog wananchi hao wamedai kuwa wanalazimika kutumia maji ya  mtaro  pale mvua zinapokuwa zimenyesha kutokana na ukosefu wa maji safi na salama na umbali mrefu ili kupata maji safi na salama.

 “Hapa kijijini kwetu weigita kata ya Kibasuka wanawake tunalazimika kutembea umbali mrefu pia kutembea usiku kwa ajili ya kutafuta maji safi na salama na wakati mwingine tunachelewa na wanaume wanalazimika kutupiga na wengine ndoa kuachika”  alisema Beatrice.

 

 

Pia Suzana Marwa ambaye ni mkazi wa kata ya Kibasuka  aliongeza  kuwa wamekuwa wakijengewa visima na wadau wa maendeleo pamoja na serikali na kushindwa kudumu kwa muda mrefu jambo ambalo hufanya tatizo hilo kuendelea kuwa sugu kijijini hapo.

Hivyo wameiomba serikali kuingilia kati kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo kwani maji yanayotumika siyo rafiki kwa ajili ya afya zao.

“Maji haya watoto wanawezakuugua vichocho pamoja na matumbo kwa sababu pia mifugo inatumia maji haya ambayo umeona tunachota baada ya mvua kunyesha.

 alisema Suzana.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha wegita alizidi kusisitiza  serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kusaidia utatuzi wa miundombinu ya maji ambayo imekuwa changamoto.

Awali akizungumza na wananchi wa kijiji cha Wegita katika Ziara yake  Naibu waziri wa TAMISEMI  Mwita Waitara na Mkurugenzi wa  Halmashauri ya wilaya ya Tarime Apoo Castro Tindwa walisema kuwa Halmashauri inatambua uwepo wa tatizo hilo na tayari imeagiza wakuu wa idara husika kuhakikisha wanashughulikia tatizo hilo haraka iwezekanavyo.