Wanaushirika kigoma itumieni fursa ya kilimo cha michikichi

 

  

 

Naibu
Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Charles Malunde, amewataka
Viongozi wa Vyama vya Ushirika vinavyolima zao la Michikichi mkoani
Kigoma kushirikiana kwa pamoja ili kuongeza nguvu ya kuzalisha na kukuza
miche bora ya Chikichi kwenye vitalu ili wakulima wapate miche hiyo kwa
wakati pale inapohitajika.

Bwana
Malunde ametoa wito huo  Jumanne, Novemba 24, 2020 mjini Kigoma
alipokutana na viongozi wa Vyama vya Ushirika vinavyolima zao la
Michikichi ambapo amewataka kushirikiana Serikali katika kuongeza
uzalishaji wa michikichi mkoani humo.

“Wanaushirika
na Wanakigoma kwa ujumla itumieni fursa hii ya kilimo cha zao la
Michikichi kwa kuwa ardhi mnayo na inayofaa kwa kilimo hiki, mkizembea
msishangae watu kutoka maeneo mengine wakachangamkia fursa hii na
kuanzisha mashamba makubwa nakumiliki soko,” amesema Naibu Mrajis.

Aidha,
Bw. Malunde amesema kuwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika watakaoshindwa
kuwahamasisha na kuwashirikisha wanaushirika na wakulima kwa ujumla
kuzalisha na kukuza miche bora ya Chikichi, wajipime na kuona kama bado
wanafaa kuchaguliwa kuendelea kuviongoza vyama hivyo.

“Kama
kiongozi ameshindwa kuwahimiza wanachama wake kushiriki katika kazi za
kujiletea maendeleo; ikiwemo kuongeza uzalishaji wa mazao yao, hatuoni
sababu za yeye kuendelea kukiongoza chama cha ushirika,” amesema Naibu
Mrajis.

Taarifa
iliyotolewa na Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Kigoma,
Robert Kitambo, wakati wa ziara ya Naibu Mrajis imeonesha kuwa eneo
lililopandwa Michikichi mkoani Kigoma ni Hekta 19,656 na eneo linalofaa
kwa ajili ya kupanua kilimo cha Chikichi ni Hekta 48,085.

“Jumla
ya eneo linalofaa kwa kilimo cha Chikichi ni Hekta 67,880 ambapo eneo
hilo kwa ujumla wake linahitaji miche 9,503,340 kuikidhi eneo lote
linalofaa kwa kilimo cha michikichi. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupitia
Sekretarieti ya Mkoa inaendelea kuhimiza na kusimamia ufufuaji wa zao la
michikichi kupitia Taasisi za Serikali zilizopo mkoani Kigoma na Wadau
mbalimbali kutoka Sekta Binafsi,” amesema Kitambo.

Mkoa
wa Kigoma baada ya kutolewa kwa Agizo la Serikali la kufufua kilimo cha
Chikichi mwaka 2018, vyama 13 vya ushirika vimeanzishwa na kusajiliwa:
Luiche Basin AMCOS, Kasuku AMCOS, Simbo AMCOS, Mahembe AMCOS, Chakulu
AMCOS, Bitale Mkongoro AMCOS, Nkungwe AMCOS, Mkuti Mchikichi AMCOS,
Kagongo AMCOS, Mungonya AMCOS, Ngogomyi AMCOS, Wamiki AMCOS na Wami
AMCOS.