Wanawake wa Kimaasai kuchuana Uchaguzi Serikali za mitaa

Egidia Vedasto,

APC Media Arusha.

Wanawake wa Jamii ya Wafugaji (Masai) Wilayani Longido katika Mkoa wa Arusha wamejizatiti kugombea nafasi za uongozi serikali za mtaa, kama ilivyo kwa wanaume tofauti na miaka ya nyuma.

Akizungumza katika Kigoda cha mwanamke kwenye mfululizo wa mada za Wiki ya AZAKI Diwani Viti Maalum Tarafa Longido, Upendo Ndoros, amewataka Wanawake kuthubutu, na kuwa tayari kuwania nafasi za uongozi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu

“Kutokana na umuhimu wa mwanamke kuwa kiongozi katika jamii, tayari nimewashawishi wanawake wenzangu 11 na wako tayari kuchukua fomu na kugombea nafasi hiyo, nikiri kwamba sio rahisi kwa jamii yetu ya Kimasai kuaminika kuongoza jamii, lakini ili wanawake tusikilizwe, tutetee haki zetu na kupinga vitendo vya ukatili hatuna budi kuamua na kutekeleza haya” ameeleza Ndoros.

Kwa upande wake Kiongozi wa mila wa jamii ya Kimasai Laigwanani Lucas Sambeke amesema wanawake wenye nafasi za uongozi ngazi ya jamii na hata serikali, wamefanya mabadiliko makubwa katika jamii hiyo na kuleta chachu ya maendeleo kwa ujumla.

“Kabla sijapata elimu kutoka Shirika la Legal Services Facility (LSF) nilijua mwanamke akiwa kiongozi atakuwa kiburi, dharau na kutotimiza wajibu wake kama mwanamke kwenye familia, lakini imekuwa tofauti na mtazamo wangu juu ya hilo” ameeleza na kuendelea,

“Kwa sasa mimi ni miongoni mwa viongozi wa mila wanaoshawishi jamii kumuamini mwanamke kupitia vikao na sherehe zetu, sababu nimeshuhudia wanavyobadilisha hali ya uchumi wa familia, kufanya maamuzi ya busara na kutetea haki za watoto na wanawake wengine, niko tayari kuwaunga mkono katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu” amesema Sambeke.

_Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Namanga iliyopo Wilayani Longido_

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Umoja wa vikundi vya wanawake vya Maendeleo Wilayani Longido, Bi Nambori Nabak amepongeza namna mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali yanavyowapa wanawake elimu na mbinu za kujikwamua na umaskini, kupinga ukatili, na kupata nafasi za utawala kama ilivyo kwa wanaume.

“Nawashukuru sana Shirika la LSF, mmetufungua macho na kutupa ujasiri mkubwa, leo mimi nina hati miliki ya ardhi, ni kiongozi wa vikundi zaidi ya 300, na nimejua haki zangu, hii ni hatua kubwa na ninasema nitapigana usiku na mchana kuhakikisha wanawake tunapata nafasi za uongozi katika jamii yetu ili maamuzi yakifanyika maoni na mchango wa mwanamke uonekane” amefafanua Bi Nabak.

Sambamba na hayo Mtendaji wa kijiji cha Eworendeke Esupath Laizer amesema jamii inaendelea kubadilisha mtazamo juu ya mwanamke kwani mchango wake ni mkubwa na unaonekana licha ya majukumu makubwa aliyonayo.

“Sisi serikali tunaendelea kupiga vita ukeketaji na tumeunda kamati za siri zinazotupa taarifa, tunamuelimisha mwanamke namna ya kuzungumza na mwanae, kupinga mfumo dume na kutoa taarifa za ukatili na vitendo vingine vinavyokinzana na haki za mwanamke, pamoja na hayo tunahakikisha mtoto wa kike hakatishi masomo yake ili aweze kutimiza ndoto zake”

“Na katika jitihada zote za Serikali tunatambua mchango wa Asasi za Kiraia, mnatusaidia kuona mbali zaidi na kubadilisha maisha ya wananchi wengi” amesema Laizer.

Mwanafunzi wa kidato cha pili mwenye ulemavu Katika Shule ya Sekondari Namanga Jackline Andrew amekiri kuwepo kwa mabadiliko kwenye jamii jinsi inamchukulia mwanamke katika ulimwengu huu wa sasa kwa jinsi wanatekeleza mambo makubwa.

“Tunapewa elimu shuleni na kwenye vikundi vya mitaani tunapokuwa nyumbani, ni dhahiri mashirika yana mchango mkubwa kwa mtoto wakike, kipekee nawashukuru shirika la LSF kutujengea bweni, kutupa vitanda na magodoro, badala ya kulala wanafunzi watatu kitanda kimoja sasa hivi tunalala wawili na tuna furaha” ameeleza Jackline.

Viongozi wa Jamii ya Kimasai wakiwa katika Kigoda cha Mwanamke Kata ya Kimokowa wakiwezeshwa na Shirika la Legal Services Facility (LSF) wa pili kutoka kushoto Mwenyekiti wa Umoja wa Vikundi vya Maendeleo Wilaya Longido, (tatu) Diwani Viti maalum Tarafa Longido Upendo Ndoros, (nne) Laiguanan Lucas Sambeke, wa kwanza kulia ni Mtendaji kijiji cha Eworendeke Esupath Laizer
Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Legal Services Facility Lulu Mwanakilala