WATAKIWA KULEA VIPAJI VYA MICHEZO ILI KULETA FAIDA KWA TAIFA

Na Seif Mangwangi
Arusha.

Waalimu,makocha na wakufunzi wametakiwa kuendelea kuibua na kulea vipaji mbalimbali vya michezo ili kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji kutimiza ndoto zao na kuwa faida ya baadae kwa taifa.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia na makundi maalum wakati akifunga kongamano la Wadau wa Michezo Wanawake ambalo limefanyika leo katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Kongamano hilo limeandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia tamasha la Kimataifa la Tanzanite Festival ambalo mwaka huu limefanyika hapa mkoani Arusha lengo likiwa ni kuadhimisha sherehe za siku ya Wanawake Duniani ambayo yanafanyika Jijini Arusha kitaifa.

Jingu amesema Waalimu,makocha na wakufunzi wana nafasi kubwa ya kuhakikisha nchi inapiga hatua katika michezo na kuwataka kuendelea kuzalisha,kuibua na kulea vipaji vya vijana wadogo.

“Michezo imekuwa ni ajira hivyo niwaombe nendeni mkaibue vipaji vya vijana ambao watakuja kupambana kwa ajili ya kuiwakilisha nchi kimataifa”.

Katibu Mkuu wa BMT,Neema Msitha amesema kongamano hilo limefanikiwa kufuatia washiriki wengi kujitokeza hali mbayo inawapa moyo kuona kwamba wadau wamedhamiria kuendeleza michezo.

“Kongamano hili tuliliandaa kwaajili ya wanawake lakini unaona hadi Wanaume wamejitokeza, hii inaonyesha namna wanaume wanatuunga mkono… lengo kuu la kongamano ilikuwa ni kujadili namna gani ya kufaidika na fursa zilizopo kwenye michezo kwa upande wa Watoto wa Kike”.

Amesema mada mbalimbali zimejadiliwa katika kongamano hilo na washiriki ambao wengi walikuwa ni waalimu wa Shule za Msingi na Sekondari,Makocha,viongozi wa Vyama na mashirikisho ya Michezo pamoja na wamiliki wa Vituo vya michezo.

Amesema wadau hao wamejadili fursa zilizopo kwenye michezo kwa Wanawake lakini pia baadhi kutoa ushuhuda wa namna wamefanikiwa kupitia michezo.