Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania TCRA Dkt. Jabiri Bakari akimpa maelezo ya utendaji
wa Mamlaka hiyo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.
Pauline Gekul wakati wa kikao na Menejimenti ya Mamlaka hiyo. PICHA NA:
TCRA
Naibu Waziri wa Habari ,Utamaduni
,Sanaa na Michezo Pauline Gekul akiwa katika makumbusho ya TCRA
kuangalia namna ya watu walipokuwa wanawasiliana
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania TCRA Dkt. Jabiri Bakari akimpa maelezo ya utendaji
wa Mamlaka hiyo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.
Pauline Gekul wakati wa kikao na Wajumbe wa Menejimenti ya Mamlaka hiyo
(hawamo pichani). PICHA NA: TCRA
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akiwa katika pamoja na Watendaji wa
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Mara baada ya kufanya kikao cha
majadiliaalno.
***************************
- Uteuzi Wajumbe wa Kamati ya Maudhui waiva
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imehimiza matumizi bora na
salama ya mfumo wa Mtandao, ili kuhakikisha maudhui mtandaoni yanasalia
kuwa yenye manufaa kwa watumiaji wote na kuhakikisha makosa ya uvunjifu
wa sheria za mtandao yanapungua, watumiaji wamekumbushwa kutumia vema
huduma hizo ili kuchagiza ukuaji wa uchumi na kuepuka matumizi ya
mitandao yanayokiuka sheria za nchi, kanuni na maadili.
Akiwa katika ziara ya utendaji,
alipotembelea Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA, Naibu Waziri wa
Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Pauline Gekul alibainisha
hayo na kuongeza kuwa matumizi sahihi na salama ya mitandao yatawezesha
kufikiwa kwa malengo ya maendeleo kwa watumiaji binafsi na kuiwezesha
Serikali kuongeza tija katika maendeleo ya uchumi.
Katika ziara hiyo ambayo Naibu
Waziri pia alipata fursa ya kujifunza namna Mamlaka hiyo inavyofanya
kazi alitoa wito kwa vituo vya utangazaji wa redio na televisheni nchini
kuhakikisha vinarusha maudhui yanayozingatia maadili ya kitaifa badala
ya kuweka kipaumbele urushaji maudhui yasiyofaa yanayotweza na kubomoa
maadili na Utamaduni wa Jamii.
“TCRA tunashirikiana nao kwa upande
wa Wizara yetu kuhakikisha kwamba maudhui ambayo yanapelekwa na vyombo
vya Habari kwa wananchi yanakuwa sahihi lakini pia yanaangalia maadili
ya Taifa letu. Nitoe tu rai kwa jamii, tunapotumia mitandao hii tutumie
kwa namna ya kujenga na si kubomoa” alisisitiza Naibu Waziri.
Naibu Waziri pia, alihimiza umuhimu
wa kuzingatia Sheria na Kanuni kwenye Sekta ya Utangazaji wa Redio na
Televisheni, kwa ajili ya Umoja, Mshikamano na Maendeleo ya Nchi.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri
Gekul alipata fursa ya kupokea wasilisho juu ya utendaji kazi wa TCRA na
kushauriana na Menejimenti ya TCRA juu ya masuala mtambuka
yanayoangukia katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
ambapo Naibu Waziri alipokea Maelezo na kupata ufafanuzi namna Mamlaka
hiyo inavyosimamia huduma za maudhui ya utangazaji na mtandaoni.
Akizungumzia Kamati ya Maudhui
ambayo hufanya kazi na TCRA, Naibu Waziri amebainisha kuwa wajumbe wa
Kamati hiyo watateuliwa hivi karibuni baada ya waliokuwa wakihudumu
katika Kamati hiyo muda wao wa utumishi kutamatika.
“Kamati ile ya Maudhui muda wake
ulikuwa umeisha lakini tumekubaliana ndani ya wiki ijayo Kamati wale
wajumbe wawe wameshateuliwa na Mheshimiwa Waziri amelifanyia kazi hili
jambo, kwa hiyo nimewahakikishia TCRA kwamba wasiwe na wasiwasi, hiyo
Kamati ikiingia basi Waziri atakapokuwa amewateua wataendelea na kazi
hiyo ya kudhibiti maudhui katika mitandao” alisema na kuongeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
TCRA Dkt. Jabiri Kuwe Bakari alibainisha kuwa katika mitandao ya kijamii
zimo fursa nyingi za maendeleo kwa ajili ya wananchi na Taifa na
kuwatolea wito wananchi kuzitumia vilivyo fursa hizo ili kujinufaisha
kiuchumi badala ya kutumia mitandao isivyopasa kinyume na Sheria za
nchi.
“Kwa hiyo tunapoingia kwenye (cyber
space) mtandaoni, ambayo ina nafasi kubwa sana ya kutengeneza ajira
unaweza ukapata fursa ya biashara au kazi nzuri tu ya kufanya ukiwa
ndani ya mtandao, badala ya kuingiza, kutengeneza au kuzungusha maudhui
ambayo hayafai kwa Jamii” alisisitiza Kuwe.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri
Gekul alitembelea kituo cha Makumbusho ya Mawasiliano, Dawati la Huduma
kwa Wateja wa Huduma na Bidhaa za Mawasiliano na Kituo cha Kufuatilia
Maudhui.