Watumishi wa maliasi watakiwa kuhamishia ofisi katika maeneo ya hifadhi ili kulinda maliasili

NA TIGANYA VINCENT

WATUMISHI
wa Mamlaka na Wakala zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii
wametakiwa kuhamia katika maeneo ya hifadhi ili kulinda na kuzuia
uharibifu wa maliasili kwa ajili ya maendeleo ya Nchi.

Kauli
hiyo imetolewa  na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala
wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Tabora , Watumishi wa Mamlaka
ya Usimamizi wa Wanyapori(TAWA), Wakala wa Huduma za Mistu Tanzania
(TFS) Kanda ya Magharibi na Hifadhi za Taifa(TANAPA) kwenye ziara yake
ya kikazi.

Alisema
Taasisi zote zinahusika na usimamizi na ulinzi wa  maliasili zinatakiwa
kujenga Ofisi ndani ya Hifadhi na watumishi kuhamia huko ili iwe rahisi
kukabiliana na uharibifu wowote unaotaka kufanyika.
Dkt.
Kigwangala aliongeza katika Ofisi zilizopo nje ya hifadhi wabaki
watumishi wachache ikiwemo Watendaji wakuu na waliobaki waende porini
kwa kuwa tayari walishapata mafunzo ya jinsi ya kupambana na waharibifu
wa maliasili.

“Hatuwezi
kulinda maliasili tukiwa maofisini …ni lazima tujenge post kwenye
hifadhi zetu na watumishi wahamie huko wakalinde maliasili zetu , ofisi
wabaki wachache ikiwemo viongozi wa Kanda… wao watakwenda kukagua
utendaji kazi wa watumishi wanaowasimamia” alisisitiza

Alisema
ni jukumu lao kuhakikisha maliasili zilipo ikiwemo wanyamapori , ndege
na mimea inalindwa kwa ajili ya faida ya kizazi cha sasa na kijacho na
kuhakikisha wanazuia uharibifu wowote ndani ya Hifadhi nchini.

Waziri
huyo alisema kuwa Kanda ya Magharibi ndio pekee imebaki na mistu mingi
ya asili ni vema watendaji wanaohusika kulinda na kuhifadhi
wakahakikisha haiendelei kuharibiwa.

Katika
hatua nyingine Dkt. Kigwangala ametoa siku 14 kwa Taasisi zilizopo
chini Wizara ya Maliasili na Utalii katika kanda ya Magharibi kukaa
pamoja na kuanisha mipaka halisi ya Hifadhi mpya za Taifa, mapori ya
akiba na Hifadhi ya Mistu  na maeneo ya wananchi ili kuondoa mwingiliano
na migogoro.

Alisema
kumekuwepo na mlingiliano ambao umetokana na baadhi ya maeneo ya
hifadhi moja kusomeka katika eneo jingine la hifadhi na kuleta utata.

Aidha
Dkt. Kigwangala alizitaka Taasisi hizo kuhakikisha wanaweka upya mipaka
katika Msitu wa Hifadhi wa Ulyankulu ambapo kuna sehemu ambayo wananchi
wameshavamia na kufanya makazi na kujenga huduma mbalimbali.

Alisema
mipaka hiyo itasaidia wananchi kuendelea kuingia katika msitu huo na
kuendesha shughuli mbalimbali ambazo zinatishia uendelevu wa msitu huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *