Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wawekezaji
waliochukua vitalu katika Ranchi ya Mabale wilayani Misenyi Mkoa wa
Kagera ambapo amewaagiza kuhakikisha wanayatumia maeneo hayo kwa malengo
yaliyokusudiwa kwani wasipofanya hivyo watanyang’anywa na kupatiwa
wawekezaji wengine.
Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel
akifafanua jambo wakati wa kikao cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi na
wawekezaji katika Ranchi ya Mabale wilayani Misenyi Mkoa wa Kagera
ambapo pia amewaeleza kuwa wizara inamalengo ya kuhakikisha uzalishaji
wa mifugo na mazao yake unaongezeka.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiwa kwenye kitalu namba 2
kinachomilikiwa na mfugaji, Primus Karokola (kulia) wakati alipotembelea
kitalu hicho kuangalia mifugo iliyopo kwenye Ranchi ya Mabale wilayani
Misenyi Mkoa wa Kagera. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
(Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki aliyesimama katikati akiwa
kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles
Mbuge (wa pili kutoka kulia), Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
(Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kulia), Katibu Tawala
Mkoa wa Kagera, Prof. Faustine Kamuzora (wa pili kutoka kushoto) na
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter
Msoffe (wa kwanza kushoto) mara baada ya kumalizika kwa kikao kifupi
kilichofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiwa kwenye picha ya pamoja
na viongozi kutoka wizarani na wawekezaji wa vitalu mara baada ya
kumalizika kwa kikao kilichofanyika kwenye moja ya kitalu katika Ranchi
ya Mabale wilayani Misenyi Mkoa wa Kagera.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki amewataka wawekezaji
kwenye vitalu vya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kufuata taratibu
zilizowekwa kulingana na mikataba yao.
Ndaki
ameyasema hayo wilayani Misenyi Mkoa wa Kagera wakati alipotembelea
Ranchi ya Mabale na kuzungumza na baadhi ya wawekezaji wenye mifugo
katika vitalu hivyo.
Waziri
Ndaki amesema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wawekezaji kuchukua
vitalu na kutovitumia kama ilivyoelekezwa kwenye mikataba kitu ambacho
kinasababisha maeneo kuwa mapori na kuvamiwa na watumiaji wengine wa
ardhi.
Wizara
kupitia NARCO imejipanga kuhakikisha wafugaji wanapata maeneo ya vitalu
kwa ajili ya kufugia kitu ambacho kitasaidia kuondokana na tatizo la
malisho na kupunguza migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na watumiaji
wengine.
“Hivyo
wizara kwa sasa imejipanga kuhakikisha wawekezaji katika vitalu
wanatumia maeneo hayo kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha wanalipa kodi kwa wakati,” alisema Waziri Ndaki.
Vilevile
alisema kuwa wizara kwa sasa inaiona NARCO kama ni sehemu ya kotokea
kwani kupitia kampuni hiyo wizara itaweza kuongeza ukusanyaji wa mapato
na kuongeza kipato wa wafugaji.
Akiwa
katika Ranchi hiyo Waziri Ndaki amemtaka mwekezaji wa Kampuni ya Chobo
Investment kuachia eneo analolimiliki kwa sasa wakati akiendelea
kujipanga ili wawekezaji wengine ambao tayari wanayo mifugo waweze
kulitumia. Aidha, amemuhakikishia mwekezaji huyo kuwa atapewa eneo
kwenye Ranchi nyingine ikiwa atafuata masharti ya mkataba wa NARCO.
Vilevile
kutokana na changamoto iliyoibuliwa kuhusu muda mfupi wa ukodishaji
vitalu, Waziri Ndaki amewaagiza NARCO kuangalia uwezekano wa kuongeza
muda wa mikataba ya muda mfupi ili iwe ni ya miaka mitano badala ya
mwaka mmoja wa sasa.
Naye
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia sekta ya Mifugo,
Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wizara imejipanga kuhakisha
uzalishaji wa Mifugo na mazao yake unaongezeka na kuhakikisha wawekezaji
katika sekta wanasaidiwa ili wasikwame katika uwekezaji wao.
Akizungumza
kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo,
Abdallah Mayomba amesema kuwa uwepo wa Ranchi katika Wilaya hiyo
umesaidia sana kupunguza migogoro ya ardhi lakini pia imesaidia
kupunguza tatizo la malisho ambalo lilikuwa linawasumbua wafugaji.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti wawezekaji hao wamemueleza waziri kuwa bado
wanahitaji maeneo kwa ajili ya kufugia na kuwa wanaishukuru serikali
kupitia NARCO kwa ajili ya kutenga maeneo hayo na kuwashushi gharama ya
ukodishaji wa vitalu.