Wazazi waaswa kutoficha watoto wenye midomo sungura

kijana mwenye mdomo sungura

Na Joachim Nyambo,Mbeya.
WAKAZI
wa mikoa ya Nyanda za juu kusini wametakiwa kuitumia fursa ya utoaji
bure Huduma ya Matibabu ya Mdomo Sungura inayofanyika katika Hospitali
ya Rufaa kanda ya Mbeya(MZRH) kwa kushirikiana na Shirika lisilo la
kiserikali la Kimarekani la Smiletrain.
Rai
hiyo imetolewa na Mtaalamu wa Upasuaji wa Mdomo Sungura katika
Hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya,Dkt Omary Matola alipozungumzia Mradi
wa Utoaji wa huduma hiyo unaoendelea katika hospitali hiyo.
Dk
Omary alisema bado wapo wazazi na walezi wanaoendelea kuamini kuwa
katika familia au ukoo kuzaliwa kwa mtoto aliye na tatizo la mdomo
Sungura ni nuksi na hivyo baadhi yao kuwafungia ndani watoto hao.
Alisema
ni wakati kwa jamii kuachana na dhana hizo potofu na badala yake
kuzitumia fursa za utoaji bure wa huduma za upasuaji katika hospitali
mbalimbali nchini zinazotoa huduma hiyo ikiwemo MZRH.
Alizitaja
Hospitali nyingine zinazotoa huduma hiyo bure kwa sasa hapa nchini kuwa
ni KCMC ya mkoani Kilimanjaro,Bugando ya Mwanza,Siriani
Arusha,Dodoma,Tumbi mkoani Pwani na CCBRT jijini Dar es salaam.
“Mdomo
sungura ni tatizo la kuzaliwa kama matatizo mengine na
linatibika.Tuachane na dhana kuwa ukizaa mtoto mwenye tatizo hili kuwa
ni nuksi kwenye ukoo au familia.Ni jambo la kusikitisha mpaka leo hii
pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau wengine bado kuna
watu wanawafungia ndani watoto wenye matatizo haya.”Alisema Dkt Omary.
Aliyataja
matatizo anayokumbana nayo mtoto mwenye mdomo sungura kuwa ni pamoja na
kushindwa kunyonya hasa kwa wale walio na mdomo wazi wa ndani,kupata
maambukizi ya sikio na kupelekea usikivu finyu,matatizo ya kinywa na
meno,na kama atakosa matibabu ya mapema atakuwa na matatizo kwenye
uzungumzaji na pia unyanyapaa.
Hata
hivyo Dkt Omary alisisitiza mambo yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya
mtoto kupelekwa Hospitalini kwaajini ya upasuaji wa mdomo sungura kuwa
ni pamoja na mtoto awe ametimiza umri wa miezi mitatu,awe na uzito
usiopungua kilogramu tano na uwingi wa damu usiwe chini ya 10.