- Watakiwa kutumia nishati safi kumuunga mkono Rais Samia
- Gambo awagawia mitungi ya gesi ya Oryx akiunga mkono jitihada za Rais
Na Seif Mangwangi, Arusha
Wazee wa Mkoa wa Arusha wamemuomba Mbunge wa Arusha Mjini kuwaombea kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwapatia nafasi moja ya viti maalum vya ubunge kwaajili ya uwakilishi wa wazee Bungeni ili mwakilishi huyo aweze kufuatilia maslahi ya wazee tofauti na sasa.
Ombi hilo wamelitoa leo Februari 19,2025 Jijini hapa katika kikao cha pamoja na mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo alipokuwa akihamasisha wazee hao kuunga juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ambapo pia waligawiwa mitungi ya gesi ya kampuni ya Oryxy.
Mwenyekiti wa baraza la Wazee hao, Mhina Sazua amesema wazee wamekuwa wakitengwa na kutoshirikishwa kwenye shughuli za maendeleo hivyo ni vyema wakapata mwakilishi mmoja bungeni ili afuatilie maslahi yao.

” Naomba niseme wazi kabisa hapa kwamba sisi wazee tunatengwa, hatushirikishwi kwenye miradi ya maendeleo, naomba Mbunge ufikishe kilio chetu, tuna matatizo mengi hatuna pakuyapeleka,”amesema Sezua.
Mbunge Gambo amesema wazee ni Lulu ya Taifa na mawazo yao yamekuwa yakiheshimiwa na ndio sababu Rais Samia amekuwa akikutana nao mara kwa mara, lakini kwa kuwa wanataka uwakilishi kwenye ngazi za maamuzi atawasilisha ombi lao.
Amewataka kuunga mkono jitihada za Rais Samia kutumia nishati safi ya kupikia ili kuokoa mazingira na kutumia nafasi hiyo kuzungumza na familia zao kuungana na Rais Samia kubadili mfumo wa matumizi ya nishati na kuanza kutumia nishati safi.
Gambo amesema utawala wa Rais Samia umetekeleza miradi mikubwa ya kimaendeleo katika Jiji la Arusha hivyo wananchi wa Jiji hilo wanatakiwa kuendelea kumuombe mema Rais huyo kwa wema wake aliowatendea na ambao ameendeela kuutenda.

“Nachelea kusema Rais Samia amekuwa akitoa kipaumbele sana kwa wakazi wa Arusha tofauti na mikoa mingine, tunatakiwa kumpongeza sana na kujivunia uwepo wake, katika uchaguzi Mkuu mwaka huu naamini nyie ndio mtakuwa wa kwanza kumpigia kura nyingi hii ni kwa sababu ameleta miradi mingi sana na ya upendeleo,”amesema.
Amesema Rais samia amegusa sekta mbalimbali katika jiji la Arusha ikiwemo sekta ya michezo kwa kujenga uwanja mkubwa wa kisasa kwaajili ya mashindano ya Afcon ambapo utaenda sanjari na ujenzi wa miundombinu ya barabara ambazo zitakuwa zikitoka na kuingia uwanjani hapo, sekta ya maji kaleta fedha nyingi pamoja na umeme na afya.

Kwa upande wake mjumbe wa kamati kuu ya CCM Taifa , Halima Mamuya ametoa wito kwa viongozi kusambaza agenda ya nishati safi kwa makundi yote ili kuhamasisha mabadiliko ya matumizi ya nishati.

Akitoa salamu za shukrani, Mjumbe wa baraza la wazee mkoa wa Arusha, Hamimu Ngalawa ameitaka Serikali kupitia upya utaratibu wa utoaji wa huduma ya afya kupitia Bima ya Afya kufuatia dawa nyingi na matibabu kuondolewa na mfuko huo.
