Waziri kalemani ateua wajumbe wa bodi ya tanesco

WAZIRI
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameteua Bodi mpya ya Wakurugenzi ya
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) yenye wajumbe wanane.

Dkt.
Kalemani amefanya uteuzi Novemba 13, 2019, unatokana na Rais John
Magufuli kumteua Dkt. Alexander Kyaruzi kuwa Mwenyekiti wa Bodi kwa
kipindi kingine cha pili.

Rais Magufuli alimteua Dkt. Kyaruzi Novemba 9, mwaka huu baada ya kuwa ameshika wadhifa huo kuanzia Mei 2016 hadi Mei 2019.

Dkt. Kalemani alisema wajumbe hao wapya watakaa madarakani kuanzia Novemba 13, 2019 hadi Novemba 12, 2022.

Aliwataja
wajumbe hao kuwa ni Balozi Dk James Nzagi (alikuwa Mjumbe wa Bodi ya
Wakurugenzi wa TANESCO iliyomaliza muda wake) na Dkt. John Kihamba
(Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Saam – DUCE).

Wengine
ni Dk Lugano Wilson (Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uhandisi na Mkuu wa
Teknolojia za Nishati – TIRDO), John Kulwa (Mkuu wa Idara ya Ukaguzi
Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Shirikishi – MUHAS) na Denis
Munumbu (Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa –
TAKUKURU).

Wengine
ni Dk Gemma Modu (Mkurugenzi NACTE), Mathew Kirama (Mkurugenzi Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma) na Gilay Shamika (Mjumbe katika
bodi iliyopita).

Dkt. Kalemani alimpongeza Rais Magufuli kwa kumuamini na kumteua tena Dkt. Alexander Kyaruzi kuisimamia Bodi hiyo.

Alimtaka
Mwenyekiti huyo kulitumikia Shirika kwa Kasi, weledi na nidhamu ili
kuwahudumia watanzania kwa kuondoa kero ndogo na kuifanya heshima ya
Watanzania kwa TANESCO iendelee.

“Ni
matumaini yetu mtakuja na ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya katika
kutekeleza azma ya Hapa Kazi Tu ili kulipa nguvu Shirika letu,” alisema
Dkt. Kalemani.

Kwa
wajumbe wote, aliwataka wachape kazi ili kuhakikisha wadau wa Tanesco
wanafaidi huduma nzuri na kuhakikisha Umeme unawafikia watanzania wote.

Kwa
upande wake, Mwenyekiti Dk Kyaruzi alimshukuru Rais Magufuli kwa
heshima kubwa kwake kwa kumteua tena kulisimamia shirika hilo.

Alisema
TANESCO miradi mingi ya kimkakati ukiwamo Mradi wa Kufua Umeme wa
Maporomoko ya Maji wa Julius Nyerere wa megawati 2,115 na wa Rusumo
mkoani Kagera.

Alisema
miradi hiyo na mingine wataisimamia kikamilifu kwa kuweka mikono yao
humo kwa kufuata miongozo mbalimbali wanayopewa na viongozi wao.

Miongoni
mwa waliohudhuria ni kikao hicho ni, Naibu Waziri Nishati Mhe. Subira
Mgalu, Katibu Mkuu Nishati Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Mhandisi Leonard
Masanja Kamishina wa Umeme na Nishati Jadilifu, Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) Dkt. Alexander
Kyaruzi, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dkt.Tito Mwinuka na Viongozi
Wandamizi wa Wizara ya Nishati.