Waziri lugola awataka wananchi kutoa taarifa za wahamiaji haramu kuondoa ujambazi, utekaji mikoa ya mipakani nchini

Na Felix Mwagara, MOHA-Katavi

WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka wananchi wa mikoa ya
mipakani nchini kutoa taarifa za wahamiaji haramu ili kudhibiti matukio
ya ujambazi, utekaji katika maeneo hayo.

Lugola alisema uhalifu katika mikoa hiyo licha ya kuwa imethibitiwa kwa
kiasi kikubwa lakini bado baadhi ya mikoa ukiwemo Mkoa wa Katavi,
wahalifu utumia njia zisizo rasmi kuingia nchini na kufanya matukio ya
uhalifu.
Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Ikola, Wilayani
Tanganyika, Mkoa wa Katavi, leo, Lugola aliwataka wananchi hao kutoa
taarifa kwa vyombo vya dola, kwa mtu au watu ambao wanawatilia mashaka
ili kudhibiti matukio mbalimbali ya uhalifu.
“Mnapaswa kuwa wazalendo kwa kutoa taarifa za wahamiaji haramu katika
maeneo yenu ili kuisaidia serikali yenu kuwasambaratisha wahamiaji
haramu ambao wanafanya uhalifu wakishirikiana na Watanzania
wasiowaaminifu waishio mipakani, hii haiwezekani, na kamwe Serikali
haiwezi kuchezewa,” alisema Lugola.
Lugola aliongeza kuwa, Tanzania ina Serikali ambayo ipo makini katika
kuwalinda watu wake, hivyo kwa majambazi ambao wanafanya matukio
mbalimbali ya utekaji lazima washughulikiwe ipasavyo bila kuonewa
huruma.
“Wahamiaji haramu wapo mitaani kwetu, na mnawajua, hivyo mnapaswa kutoa
taarifa kwa maafisa uhamiaji, Jeshi la Polisi au vyombo vingine vya dola
nchini, ili Serikali ya Dkt. Magufuli iweze kuwatia mbaroni haraka
iwezekanavyo,” alisema Lugola.
Kwa upande wake, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Katavi, Kamishna Msaidizi,
Vicent Haule alikiri kuwepo na changamoto hiyo, na kuahidi kuwasaka
wahamiaji haramu kupitia vyanzo vyote vya uchunguzi.
Haule alisema maeneo ya mipakani yana changamoto licha ya kuwa ofisi
yake inafanya kazi usiku na mchana kupambana na wahamiaji haramu, na
wapo tayari kupokea taarifa za wahamiaji hao watakapopewa na wananchi.
“Tunamshukuru sana mheshimiwa Waziri kwa kutupa maelekezo mbalimbali,
hasa ya kuhusu masuala ya wahamiaji haramu, na uraia hasa pale makazi ya
Katumba na Mishamo, kwasababu amewataka wakazi waliopewa uraia
wasivunje sheria za nchi kwa kwenda Burundi na kurudi nchini bila
kufuata sheria,” alisema Haule.
Aidha, Lugola aliwataka Polisi kuwasaka na kuwakamata majambazi na
kuwasambaratisha bila woga wowote maana mhalifu hawezi kuchekewa.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Lilian Matinga, alimshukuru Waziri
Lugola kwa kufika katika wilaya hiyo na kuahidi maagizo yote aliyoyatoa
kwa Wilaya hiyo watayafanyia kazi kupitia vikao vyao vya kamati ya
ulinzi na usalama.
Waziri Lugola amemaliza ziara yake Mkoani Katavi kwa ksuikiliza kero
mbalimbali za wananchi kupitia mikutano ya hadhara na kukagua miradi
mbalimbali ya maendeleo mkoani humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *