Waziri lugola ayasimamisha magari yaliyotaka kusababisha ajali, dereva wa basi akamatwa, abiria warudishiwa nauli na kutafutiwa usafiri mwingine

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Kangi Lugola (kulia), akimuuliza maswali dereva wa basi la abiria la
Manoni Safari, Marijani Saidi ambaye alitaka kusababisha ajali eneo la
Kijiji cha Nyashishi, Wilayani Busega Mkoani Simiyu, leo, kutokana na
mwendokasi na kulazimisha kuovateki.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Kangi Lugola (katikati), akisoma karatasi yenye taarifa ya leseni yake,
zilizoandikwa na Polisi dhidi ya dereva wa basi la abiria la Manoni
Safari, Marijani Saidi (kushoto), ambaye alitaka kusababisha ajali
nyingine Kijiji cha Nyashishi, Wilayani Busega Mkoani Simiyu, leo,
kutokana na mwendokasi na kulazimisha kuovateki.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Kangi Lugola (wapili kushoto), akisimamia kondokta wa basi la Manoni
Safari (katikati), akiwarudishia nauli zao abiria wa basi hilo, baada ya
kukamatwa na Waziri huyo kutokana na mwendokasi uliotaka kusababisha
ajali Kijiji cha Nyashishi, Wilayani Busega Mkoani Simiyu, leo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
…………………
Na Felix Mwagara, MOHA, Busega.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Kangi Lugola ameyakamata magari mawili yaliyotaka kusababisha ajali kwa
kufukuzana na kulazimisha kuovateki bila ya kuwa na tahadhari katika
barabara kuu ya Mwanza Mara. 
Magari hayo ni basi lililokuwa na
abiri liitwalo Manoni Safaris lenye namba za usajili T800DCU, pamoja na
lori namba T865CVJ, yaliyokuwa yanatokea Mwanza kuelekea Mkoani Mara,
yalipofika Kijiji cha Nyashishi, Wilayani Busega Mkoani Simiyu yakiwa
mwendokasi yakawa yanalazimisha kuovateki bila kuwa na tahadhari.
Waziri huyo  akiwa safarini
akitokea Wilayani Bunda, leo, alishuhudia magari hayo yakiwa mwendokasi
na yakilazimisha kuovateki hali iliyosababisha magari yaliyokuwa
yanatokea Mkoani Mara kuyakwepa kwa shida ili kuepusha ajali isitokee.
Baada ya tukio hilo, Waziri huyo
alimwelekeza dereva wake kugeuza gari na kuyakimbiza magari hayo hasa
basi hilo Manoni Safaris lenye namba za usajili T800DCU, ambalo ndilo
lililokuwa na makosa dereva akijua magari yanakuja mbele yake lakini
akawa analazimisha kuovateki akilikimbiza lori ambalo lilikua mbele
yake. 
“Huyu dereva hana tahadhari na mtu
hatari sana, alitaka kutuua na pia kuua abiria wa basi hili, lazima
afunguliwe mashtaka apelekwe mahakamani na iwe fundisho kwa madereva
wazembe wa aina hii, na nimeambiwa na abiria hapa kuwa aliwapuuza baada
ya kuambiwa apunguze mwendo,” alisema Lugola.
Waziri huyo alimkamata dereva wa
basi hilo na kumtaka atoe leseni yake, kabla ya kupelekwa Kituo cha
Polisi Busega kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka, na alielekeza abiria wa
basi hilo warudishiwe nauli zao na watafutiwe basi lingine ili
waendelee na safari.
Dereva wa basi hilo, Marijani
Saidi alikiri kufanya kosa na alimuomba msamaha Waziri huyo, hata hivyo
alikataliwa kutokana na kuvunja sheria za usalama barabarani na kutaka
kusababisha ajali.
Akizungumzia tukio hilo, abiria wa
basi hilo, Mwita Machela, alisema walimtaka dereva huyo kuacha
kuendesha mwendokasi lakini aliwapuuza na kuendelea na safari.
“Waziri yupo sahihi kutusimamisha
maana ametuokoa pia, huyu dereva alikua mwendokasi, tulimuonya aache
lakini hakutusikiliza, sasa haraka yake imeishia hapa, na sisi
tumepotezewa muda wetu kutokana na uzembe wake,” alisema Lugola.
Waziri Lugola alisimamia kondakta
wa basi hilo akiwarudishia nauli abiria hao, pamoja na kuhakikisha
wanapandishwa katika mabasi yaliyokua yanapita katika barabara hiyo. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *