Waziri lugola: rais ameagiza line za simu ambazo hazijasajiliwa hazitazimwa

Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema hakuna Mtanzania yeyote
ambaye simu yake itazuiwa kutumika, kwa sababu hajasajili, kwa kigezo
cha kutokuwa na Kitambulisho cha Taifa.

Kwa maana hiyo, ikifika Desemba 31 mwaka huu, ambayo ni mwisho wa
kusajili laini za simu kama mtu hajapata kitambulisho cha taifa, laini
yake ya simu haitazimwa na ataendelea kuitumia.

Aidha, Lugola amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho Vya
Taifa (NIDA), kuhakikisha kwamba maofisa wa NIDA wilaya zote, wanapeleka
namba za vitambulisho vijijini ; na si kutegemea kuzipata katika simu.


Lugola ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma jana Jumatano  Novemba 13, 2019 wakati akijibu mwongozo wa  mbunge wa Kavuu (CCM) Dk Pudensiana Kikwembe.
 
Katika mwongozo wake alisema uandikishaji wa vitambulisho vya taifa, umekuwa na changamoto maeneo ya vijijini. 

Alisema kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa hasa vijijini hususani majimbo ya Kavuu na Mlele, ambako uandikishaji umekuwa ni shida.

“Kama inavyojulikana mwisho ni Desemba mwaka huu, naomba kujua kauli ya
serikali nini kinafanyika ili waweze kupata vitambulisho,”alisema
Pudenciana.


Akijibu
mwongozo huo, Lugola aliwatoa hofu wasiwasi Watanzania kuwa utaratibu
wa utambuzi, usajili na utoaji wa vitambulisho kwa wananchi, ambao wana
sifa za kupata vitambulisho ni endelevu.

“Zoezi hili halina mwisho wala halina tarehe kwamba ikifika tarehe
fulani kuna Mtanzania hajapata kitambulisho, basi huyo Mtanzania
hatapata kitambulisho tena, Watanzania wasiwe na wasiwasi, hili ni zoezi
endelevu na ndio maana kila mwaka kuna Watanzania ambao wanafikisha
miaka 18.” alisema.

Akizungumzia suala la usajili wa laini kwa vidole, Lugola alisema:
“Naomba niwatoe wasiwasi Watanzania wote kwamba maelekezo Rais John
Magufuli hakuna Mtanzania ambaye simu yake itazuiwa kutumika eti kwa
sababu hana kitambulisho cha taifa na hivyo hajasajili laini yake.”