Waziri mkuu aagiza wakurugenzi wawili wa halmashauri wafike ofisini kwake kesho

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Mtama na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda ya Kusini, wafike ofisini
kwake Dar es Salaam kesho asubuhi na taarifa kuhusu skimu wa umwagiliaji
wa Narunyu.
Ametoa agizo hilo leo mchana (Alhamisi, Oktoba 17, 2019) wakati
alipoenda kukagua skimu hiyo ambayo imekuwa ikilalamikiwa tangu 2017.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama ni Bw. Warioba Gunze na Mkurugenzi wa
Umwagiliaji wa Kanda ya Kusini, ni Mhandisi Mndeme.
Amechukua uamuzi huo baada ya kufika eneo la mradi na kupokea malalamiko
ya wanajumuiya ya umwagiliaji kutoka kwa Mwenyekiti wao, Bw. Bakari
Awadhi juu ya kusuasua kwa mradi huo lakini alipotaka apate maelezo ya
wataalamu hakuna hata mmoja ambaye alikuwepo.
“Nilitaraji niwakute hapa Mkurugenzi wa Halmashauri, Afisa Umwagiliaji
wa Wilaya na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda. Nimeagiza wanikute
uwanja wa ndege Lindi au Dar es Salaam na kesho asubuhi waje ofisini
kwangu wanipe taarifa kamili ya mradi huu. Nataka nijue fedha
zilizobakia zaidi ya sh. milioni 240 ziko wapi.”
“Walipaswa niwakute hapa wananisubiri kwa sababu nilitoa taarifa tangu
jana kwamba nitapita hapa. Nimepata taarifa kwamba wamesafiri kutoka
Mtwara na leo asubuhi walikuwepo Lindi mjini. Waje ofisini kesho,
wakishindwa, nitachukua maamuzi mengine,” amesema.
Akielezea umuhimu wa mradi huo wakati akizungumza na baadhi ya
wanaushirika waliokuwepo, Waziri Mkuu amesema ni wa muhimu kwa sababu
unatiririsha maji wakati wote. “Huu ni mradi wa kuringia. Mradi huu
unatiririsha maji wakati huu wa kiangazi, tena mengi tu.”
Amesema kutokana na umuhimu wa mradi huo, hivi sasa wangekuwa
wanazalisha mazao ya kila aina. “Hapa ni mahali pa kuzalisha mazao
mengi, leo unalima mahindi, ukivuna unapanda matikiti, ukitoa unapanda
nyanya. Sasa nitapasimamia mwenyewe,” amesisitiza.
Amewataka wanaushirika wanaounda jumuiya ya umwagiliaji wahakikishe kila
mmoja anatambua eneo lake na mara kazi ikianza wawe tayari kuanza
kilimo. “Huu mradi una manufaa kwa watu wa Ruo, Mahumbika hadi Mnazi
Mmoja. Lazima tuung’ang’anie kwa sababu kuna idadi kubwa ya wakulima
wanaoutegemea. Huu mradi lazima tuuvalie njuga.”
Waziri Mkuu alipofika uwanja wa ndege wa Lindi, maafisa hao walikuwa
hawajafika kwa sababu simu zao hazikupatikana, na akaagiza waje Dar es
Salaam kesho asubuhi.
Mapema, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Bw. Shaibu Ndemanga alimweleza Waziri
Mkuu kwamba katika mafaili aliyoyapitia ofisini kwake alibaini kwamba
mradi huo ulitengewa sh. milioni 788 ambapo mkandarasi wa kwanza Chest
Investments Company alilipwa sh. milioni 121 lakini akashindwa kazi.
“Mkandarasi wa pili ambaye ni D & L naye alilipwa zaidi ya shilingi
milioni 400 naye pia akashindwa kazi ya kuondoka tope. Kwenye ripoti,
inaonesha zilibakia sh. milioni 249,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa wanajumuiya ya umwagiliaji ya Narunyu, Bw. Bakari
Awadhi alisema skimu hiyo yenye ukubwa hekta 1,200 imekuwa ikijaa maji
na kufunika mitaro na hatimaye kujaa mchanga.
Alimwomba Waziri Mkuu awasaidie kuifufua skimu hiyo kwa sababu inawanufaisha wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *