Waziri mkuu aeleza jinsi ya kufikia nchi ya kipato cha katiWAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema ili Tanzania ifikie lengo la kuwa nchi ya kipato cha kati
inayoongozwa na uchumi wa viwanda, haina budi kuhakikisha kuwa inatimiza
vigezo kadhaa, kikiwamo cha ukuaji wa uchumi kwa kiwango cha asilimia
12 kwa mwaka.


Amesema vigezo vingine ni
mchango wa viwanda katika Pato la Taifa usiopungua asilimia 15; utoaji
ajira rasmi na za moja kwa moja uongezeke na kufikia asilimia 40 ya
ajira zote; na sekta ya viwanda iweze kuiingizia nchi mapato ya fedha za
kigeni zaidi ya asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni.


Alitoa kauli hiyo jana usiku
(Alhamisi Oktoba 17, 2019) wakati akizungumza na wageni na washiriki
waliohudhuria hafla ya utoaji Tuzo za Rais kwa Wazalishaji Bora wa mwaka
2018 iliyofanyika kwenye hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.


Waziri Mkuu ambaye alikuwa
mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli alisema: “Ili kufikia
vigezo hivyo na kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya viwanda, ni lazima
tujizatiti na kuimarisha ushirikiano wa karibu baina ya sekta ya umma na
sekta binafsi,” huku akiwasihi washiriki katika hafla hiyo waitumie
fursa hiyo kutafakari mbinu mpya za kufikia vigezo hivyo muhimu vya
kuijenga Tanzania mpya ya viwanda.


“Kila mmoja wetu anatambua
umuhimu wa sekta ya viwanda katika kukuza uchumi wa nchi yoyote duniani.
Viwanda ndivyo vimekuwa chimbuko la maendeleo ya haraka ya nchi
mbalimbali duniani na mhimili mkuu wa kutegemewa katika kuondoa
umasikini kwa kutoa ajira nyingi na za uhakika kwa wananchi. Maendeleo
ya sayasi na teknolojia yanategemea sana sekta ya viwanda.”


“Takwimu pia, zinaonesha
kwamba katika mwaka 2018, sekta ya viwanda imetoa ajira rasmi 306,180
ikilinganishwa na ajira 280,899 za mwaka 2017; sawa na ongezeko la
asilimia tisa. Tutaendelea kuchukua hatua zinazostahiki ili kuwezesha
sekta hii ikue kwa haraka na kutoa mchango mkubwa zaidi katika Pato la
Taifa na hivyo kuchangia katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini wa
wananchi wetu,” alisema Waziri Mkuu.


Aliema kutokana na jitihada
kubwa zinazoendelea kufanywa na Serikali za kujenga uchumi wa viwanda,
jumla ya viwanda vipya zaidi ya 4,000 vimejengwa katika mikoa
mbalimbali. “Viwanda vilivyojengwa vinazalisha bidhaa za ujenzi (saruji,
nondo, vigae, mabomba, marumaru, n.k); pamoja na viwanda vya kusindika
mazao ya kilimo ikiwemo nafaka, matunda, mafuta ya kupikia na bidhaa za
ngozi,” alisema.


Alisema viwanda vingi
vimeanzishwa nchini na ni faraja kuona wawekezaji wa ndani nao
wanaendelea kufungua viwanda vipya pamoja kuongeza uwekezaji wao. “Moja
ya viwanda vinavyohamasishwa ni vile vinavyochochea uzalishaji wa ajira
kwa wingi. Ujenzi wa viwanda vipya nchini, katika kipindi cha Serikali
ya awamu ya tano, umechangia kupatikana kwa ajira mpya 482,601 nchi
nzima,” alisema.


Mapema, akimkaribisha Waziri
Mkuu kuzungumza na wenye viwanda na washiriki wa hafla hiyo, Waziri wa
Viwanda na Biashara, Bw. Innocent Bashungwa alisema wizara yake kwa
kushirikiana na sekta binafsi itaendelea kuondoa kero zinazokwamisha
ufanisi na ukuaji wa sekta ya viwanda zikiwemo kero kubwa
zinazolalamikiwa na sekta hiyo.


Alizitaja baadhi ya kero hizo
kuwa ni ucheleweshaji wa malipo ya madai ya kodi za ongezeko la thamani
(VAT) na asilimia 15 ya ziada inayolipwa na waagizaji wa sukari ya
viwandani; ushindani usio na uwiano na bidhaa za bei nafuu kutoka nje ya
nchi kama vile nondo, mabomba ya plastiki, nguo na mavazi, bidhaa za
ngozi na marumaru.


“Pia tutaangalia upya uwepo wa
utitiri wa tozo na ada za juu zinazotozwa na taasisi mbalimbali za
Serikali, ongezeko la kodi ya kuagiza mali ghafi kutoka nje ya nchini,
na kucheleweshwa upatikanaji wa vibali vya kufanya kazi kwa wataalam wa
kigeni wasiopatikana hapa nchini (expetriates employees),” alisema.


Kuhusu usajili wa makampuni,
Waziri Bashungwa alisema Wizara hiyo kupitia Wakala wa Usajili wa
Biashara na Leseni (BRELA) imekamilisha kuweka mifumo ya kusajili majina
ya biashara kwa njia ya mtandao. “Mifumo hiyo inawawezesha
wafanyabiashara kusajili jina la biashara, uandikishwaji wa makampuni,
usajili wa alama za biashara na usajili wa viwanda mahali popote walipo
kupitia tovuti ya wakala (www.brela.go.tz).”


Naye Mwenyekiti wa Shirikisho
la Viwanda Tanzania (CTI), Bw. Subhash Patel, alisema CTI inaunga mkono
azma ya Rais Magufuli ya kuleta viwanda nchini. “Hakuna nchi itakuwa
imefanikiwa duniani bila kuwekeza kwenye viwanda,” alisema.


Akielezea uwepo wa fursa za
biashara kwa wawekezaji wa Kitanzania, Bw. Patel alisema Tanzania ina
majirani ambao hawana bandari na hiyo ni fursa tosha ya kuwekeza na
kuendeleza biashara kwenye nchi jirani.