Waziri mkuu ataka mikoa iliyobakia itekeleze agizo lake kuhusu uwekezaji

Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka mikoa ambayo bado haijatekeleza agizo
lake la kuandaa makongamano ya uwekezaji ihakikishe inafanya hivyo mara
moja.

Ametoa agizo hilo jana mchana (Jumamosi, Oktoba 19, 2019) wakati
akifungua Kongamano la Uwekezaji kwa mkoa wa Pwani katika ukumbi wa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
“Nitumie fursa hii kuwapongeza viongozi wa mkoa wa Pwani kwa kutekeleza
agizo nililolitoa Juni 18, 2018 wakati wa kongamano la tatu la
uwezeshaji wananchi kiuchumi la kuhakikisha mikoa yote inaandaa
kongamano la uwekezaji na inakuwa na mwongozo wa uwekezaji wa mkoa.
Mikoa ambayo haijatekeleza agizo hilo, ifanye hivyo mara moja,” amesema.
Waziri Mkuu amesema mkoa huo umeweza kubaini fursa zilizopo katika mkoa
wa Pwani na kuzitangaza kupitia mwongozo wa uwekezaji ambao pia
ameuzindua leo.
Amesema kaulimbiu ya kongamano hilo isemayo: ‘‘Ijenge Tanzania, wekeza
Pwani mahali sahihi kwa uwekezaji (Build Tanzania, Invest in Pwani, the
Best Place for Investment)” ina maana kuwa, licha ya mkoa wa Pwani
kubainisha na kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo,
unajipambanua vizuri na kuonyesha kuwa ni kwa namna gani umejiandaa na
umetengeneza mazingira bora yanayovutia wawekezaji wa ndani na nje.
“Ili kudhihirisha dhamira ya dhati ya kukuza uchumi kupitia viwanda,
nimeelezwa kuwa mkoa umetenga hekta 53,016 kwa ajili ya uwekezaji wa
viwanda ambavyo vitatumia rasilmali zilizopo ndani ya mkoa na maeneo
mengine ya nchi kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha
maisha ya wanachi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa
Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe wanasimamia miundombinu
inayoelekea kwenye viwanda vilivyopo kwenye maeneo yao.
“Kila mmoja ahakikishe maji, umeme na barabara vinafika kila eneo ambalo
mwekezaji anataka kujenga kiwanda. Nitumie fursa hii kuwaomba mlete
mabadiliko chanya yanayotokana na maboresho yanayofanywa na Serikali ya
awamu ya tano.”
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa kongamano
hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Bibi Angella
Kairuki alisema kwamba Serikali imeanza kutekeleza mapendekezo ya mpango
wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini (Blueprint for
Improving Business Environment Regulatory Licensing in Tanzania) kwa
kuondoa tozo 163 zilizokuwa zikilalamikiwa na wawekezaji.
“Pia tumetenganisha majukumu ya TBS ya TFDA ambayo sasa ni TMDA. TBS
itashughulika na vyakula na TMDA itashughulika na dawa na vifaatiba.
Vilevile, tumeondoa ada za usajili sehemu za kazi ambazo zamani ilikuwa
ni sh. 28,000 na sasa hivi zinatolewa bure,” alisema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikillo aliwataka watu
wote wanaotaka kuwekeza nchini waufikirie kwanza mkoa wa Pwani kwa
sasabu uko kimkakati na una fursa nyingi ikiwemo hali nzuri ya usalama
na kwa maana hiyo mitaji yao italindwa.
“Mkoa wetu uko kwenye eneo la kimkakati la kuwezesha biashara kwa kuwa
uko karibu na bandari ya Dar es Salaam na uwanja wa ndege; uko karibu na
soko kubwa ambalo ni Dar es Salaam; unapitiwa na reli zote kwenda
mikoani na nchi jirani; unapitiwa na barabara kuu itokayo Dar es Salaam
na pia una bandari kavu ya Kwala.”
Mbali ya hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa alisema faida nyingine ambayo mkoa huo
unayo ni uwepo wa miundombinu ya maji, umeme na nishati ya gesi asilia
ambayo imeanza kutumiwa na baadhi ya viwanda kama Goodwill na Lodhia
Steel.
Naye Dkt. Tausi Kida, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchumi ya Kijamii (ESRF)
ambayo ilisimamia uandaaji wa mwongozo wa uwekezaji kwa mkoa wa Pwani,
alisema taasisi yao inasaidia kuandaa na kuchambua fursa zilizopo kwenye
mikoa mbalimbali. “Hadi sasa tumekwishaisadia mikoa 17 kuandaa miongozo
ya uwekezaji na kwa sasa mikoa 12 imeshakamilisha na mikoa mitano iko
kwenye hatua mbalimbali,” alisema.
Akitoa taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid
Nsekela ambao ni wadhamini wakuu, Afisa Mkuu wa Biashara, Benki ya CRDB,
Dkt. Joseph Witts alisema benki hiyo imeendelea kugusa sekta zote za
uchumi na hivyo kuongeza tija kwenye mnyororo mzima wa uzalishaji.
Alisema huduma zao zimelenga kuongeza tija na ufanisi katika sekta ya
viwanda nchini ikiwemo utoaji wa mikopo ya biashara kwa ajili ya
kuongeza mikopo ya uendeshaji (working capita loans) na mikopo ya
uwekezaji (investment loans).
“Benki yetu inatoa mikopo ya biashara na uwekezaji katika maeneo
mbalimbali ambapo mikopo ya kilimo ni shilingi bilioni 357, uzalishaji
wa viwanda (shilingi bilioni 214), biashara (shilingi bilioni 347),
mahoteli (shilingi bilioni 87) na sekta ya madini (shilingi bilioni
91),” alisema.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *