Waziri mkuu, kassim majaliwa akagua miradi wa nyumba za nssf, zilizopo tuangoma katika wilaya ya kigamboni, jijini dar es salaam

WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema nyumba zote zinazojengwa na Taasisi za
Umma katika wilaya Kigamboni jijini Dar es salaam zinapaswa kukamilika
haraka ili ziuzwe ua kupangishwa kama ilivyokusudiwa.

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Novemba 27, 2019) baada ya kukagua miradi
ya ujenzi wa nyumba za NSSF, NHC na Watumishi Housing iliyopo katika
wilaya ya Kigamboni.

Waziri Mkuu amesema inasikitisha kuona kwamba watumishi wa umma na
wananchi  jijini Dar es Salaam hawana nyumba nzuri za kuishi wakati zipo
nyumba nyingi  nzuri zimejengwa na zinahitahi umaliziaji mdogo tu ili
ziweze kukalika.


Hivyo, Waziri Mkuu ameitaka Menejimenti ya NSSF kakamilisha haraka
ujenzi na uwekaji wa miundombinu ya umeme, maji safi na maji taka 
katika nyumba zake 161 zilizoko  Tuangoma, 820 zilizoko Mtoni Kijichi na
439 zilizoko Dungu ili ziuzwe na kuepusha uwezekano wa uharibifu
unaoweza kutokea  kwa nyumba hizo kakaa muda mrefu bila kupata wanunuzi
au wapangaji.

Ili kufanikisha jambo hilo Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Mthamini Mkuu wa
Serikali atathimini nyumba hizo na kutoa   bei halisi ya soko kwa sasa
ili kuwawezesha Watanzania wengi na hasa watumishi wa Umma kununua na
kupanga katika nyumba hizo.

Pia, Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa wilaya  na viongozi wa Halmashauri ya
wilaya ya Kigamboni kuwasaidia watumishi wa wilaya na Halmashauri hiyo 
kuingia mikataba rafiki itakayowawezesha watumishi  hao kupewa
kipaumbele katika kununua au kupanga kwenye nyumba hizo.

Mheshimiwa Majaliwa pia ameitaka Menejimenti ya NSSF kufikiria namna ya
kuzungumza na viongozi wa vyuo mabalimbali kama vile Chuo cha Usimamizi
wa Fedha (IFM), Chuo cha Mwalimu Nyerere ili wanafunzi wa vyuo hivyo
wapatiwe fursa ya kupanga katika nyumba hizo kwa bei watakazomudu.

Pia Mheshimiwa Majaliwa ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es salaam
ukishirikiana na SUMATRA  kuanzisha njia za mabasi ya daladala 
zitakazoanzia au kupitia kwenye nyumba za NSSF Mtoni Kijichi na Dungu
ili kuwezesha wapangaji na wananchi watakaonunua nyumba hizo kupata
usafiri wa umma.

Vilevile, Waziri Mkuu ameuagiaza uongozi huo kuhakikisha kwamba eneo la
Mtoni Kijichi zilipojengwa nyumba za NSSF na NHC linapata huduma za
Shule, Kituo cha Afya na Kituo cha Polisi kwani litakuwa na wakazi wengi
.

Ili kuongeza thamani ya nyumba hizo na kuvutia wapangaji na wanunuzi,
Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Menejimenti ya NSSF kuboresha barabara
kwenye mitaa yote zilipojengwa nyumba hizo kwa kushirikiana na TARURA.

“Nashauri ziwekwe taa za sola kwenye barabara za mitaa yote ya nyumba
hizi ili kupendezesha eneo na kuwafanya wananchi wahamasike kununua na
kuishi katika nyumba hizi” amesema Majaliwa.

Akiwa kwenye Mradi wa Nyumba za NHC Mtoni Kijichi, Mheshimiwa Majaliwa 
alitembelea Shule ya Awali ya Kids Paradise na kufurahishwa na utaratibu
mzuri wa shirika hilo wa kukumbuka kujenga jengo zuri la Shule hiyo na
kulipangisha ili kuhakikisha kwamba  watoto wanaoishi katika nyumba hizo
wanapata fursa ya kusoma elimu ya awali.

Akizungumza baada ya kukagua Mradi wa ujenzi wa nyumba za NHC Mwongozo,
Mheshimiwa Majaliwa ameutaka uongozi wa NHC  kuwa karibu na wateja
wanaopanga au kununua nyumba zao. “ Shughulikieni malalamiko yote 
yanayotolewa na wateja wenu ili wajenge imani kwenu, Alisisitiza
Majaliwa.

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Wenye
Ulemavu Jenista Mhagama alisema wizara yake imeyapokea maelekezo yote
yaliyotolewa na Waziri Mkuu na kwamba watafanya kila njia ili
kuhakikisha kwamba majengo yote yanakamilika haraka na kuuzwa au
kupangishwa.

Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, william Lukuvi 
alimwambia Waziri Mkuu kuwa amekwishatoa maagizo kwa NHC ijenge uzio
japo wa waya  na wapande michongoma ili kuweka ulizi kwenye eneo la
nyumba zao za Dungu.

Mheshimiwa Lukuvi alisema amewapa NHC miezi mitatu ili wafanye
marekebisho katika nyumba ambazo zimelalamikiwa na wateja kuwa zina
kasoro ili kujenga imani kwa wateja wao.

Mapemba Mkadiriaji Majengo wa NSSF, Abon Mhando ambaye pia ni  Kaimu
Meneja wa  Miradi wa NSSF alimwambia Waziri Mkuu kuwa Mradi wa ujenzi wa
nyumba wa Tuangoma  una jumla ya nyumba 161 na kati ya hizo nyumba 76
zimekamilika. Aliwataja wakandarasi wanaojenga mradi huo kuwa ni Kampuni
za CASCO, Advent na NANDRA.

Alisema  Mradi wa Dungu una jumla ya nyumba 439 na kati ya hizo nyumba
95 zimekamilika na jumla ya makampuni 13 yameshiriki katika ujenzi wa
mrdi huo.

Kuhsu mradi wa Mtooni Kijichi  Mhando alisema  mradi huo una jumla ya nyumba 820 na kati ya hizo nyumba 417 zimekamilika.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU