Waziri mwambe akutana na menejimenti na wakuu wa taasisi zilizochini yake kupokea vipaumbele na mikakati yao

Waziri
wa Viwanda na Biashara Mhe. Geoffrey Mwambe akizungumza wakati
akifungua kikao kazi cha siku mbili kilichowakutanisha Menejimenti,
wakuu wa idara, Vitengo na wakuu wa taasisi zilizochini ya Wizara hiyo
kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja na kujadili utekelezaji wa
bajeti, kikao kilichofanyika jijini Dodoma.



Naibu
Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe akizungumza
na Menejimenti, wakuu wa idara, Vitengo na wakuu wa taasisi zilizochini
ya Wizara hiyo katika kikao kazi kilicholenga kuweka mikakati ya pamoja
na kujadili utekelezaji wa bajeti hiyo, kikao kilichofanyika jijini
Dodoma.


Katibu
Mkuu Wizara ya Viwanda na biashara Prof. Riziki Shemdoe akizungumza na
Menejimenti, wakuu wa idara, Vitengo na wakuu wa taasisi zilizochini ya
Wizara hiyo katika kikao kazi kilicholenga kuweka mikakati ya pamoja na
kujadili utekelezaji wa bajeti hiyo, kikao kilichofanyika jijini Dodoma.


Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Ludovick Nduhiye akizungumza
na Menejimenti, wakuu wa idara, Vitengo na wakuu wa taasisi zilizochini
ya Wizara hiyo katika kikao kazi kilicholenga kuweka mikakati ya pamoja
na kujadili utekelezaji wa bajeti hiyo, kikao kilichofanyika jijini
Dodoma.


Baadhi
ya watumishi wa Menejimenti, Wakuu wa idara, vitengo na wakuu wa
taasisi zilizochini ya Wizara ya Viwanda na Biashara wakimsikiliza
Waziri wa Wizara hiyo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kilicholenga
kuweka mikakati ya pamoja na kujadili utekelezaji wa bajeti hiyo, kikao
kilichofanyika jijini Dodoma.

 
Na Alex Sonna – Dodoma.
 

Waziri
wa Viwanda na Biashara Mhe. Geoffrey Mwambe amekutana na kufanya kikao
na Menejimenti, wakuu wa idara, Vitengo na wakuu wa taasisi zilizochini
ya Wizara hiyo kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja na kujadili
utekelezaji wa bajeti hiyo katika kufikia malengo yaliyowekwa na kila
taasisi kueleza malengo yake na vipaumbele vyake.

Akifungua
kikao hicho cha siku mbili Waziri Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) amezitaka
kila taasisi kuhakikisha zinafanya kazi kwa weredi na ubunifu mkubwa na
katika bajeti yake kila taasisi ilenge katika miradi ya maendeleo na
ipewa kipaumbele katika mipango ya utekelezaji wa bajeti yake.

“Nataka
kila taasisi ihakikishe katika bajeti yake inalenga miradi ya maendeleo
itakayosaidia kukua kwa taasisi, pia kila taasisi ipunguze kwa kiasi
kikubwa matumizi yasiyo ya lazima tunataka bajeti ilete tija” amesema
Mhe. Mwambe.
 

Aidha
amezitaka taasisi katika bajeti yake zilenge vipaumbele vichache
ambavyo vitatekelezeka na sio kuweka vipaumbele vingi na bajeti ikawa
haitoshi na fedha kutawanywa katika sehemu mbalimbali na mwisho wa siku
hakuna matokeo katika utekelezaji wake.
 

Amezitaka
taasisi kufanya kazi kiubunifu ambapo amebainisha kuwa Tanzania ni nchi
ambayo imejaliwa kuwa na fursa nyingi lakini bado hazijaleta tija kwa
jamii na kuwa ni wajibu wa taasisi kuwa wabunifu nini kifanyike fulsa
hizi ziwafikie walengwa hasa katika teknolojia.
 

“Ukiangalia
katika kilimo hasa vijijini miaka nenda rudi tunatumia majembe ya mkono
hiyo tija itapatikana sangapi na taasisi za utafiti zipo tu, kabla ya
kuondoka katika hiki kiti nataka nizindue jembe lililobuniwa na CAMARTEC
linaloleta mapinduzi” amesema.
 

Ameongeza
kuwa “Hatuna kiwanda cha kutengeneza nguo lakini malighafi zipo na kila
siku yanasafirishwa marobota mengi na mwisho wa siku tunauziwa nguo,
wakati uwezo tunao wa kuwa na viwanda hapa nchini nataka hili lifanyiwe
kazi haraka sababu nguvu kazi tunayo” amesema.
 

Ameitaka
Mamlaka ya maendeleo ya biashara nchini TANTRADE kuja na mikakati ya
kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ya biashara hasa kwa wajasiliamali
katika halmashauri zote ili kuwaendeleza wafanyabiashara hao kukua
kutoka hapo walipo na kuwa na biashara kubwa.
 

Pia
ameitaka TANTRADE kuwa na mikataba ya mazao ya kibiashara kama korosho
badala ya kusubiri minada ambayo sio uhakika huku akitaka kuja na
teknolojia inayofaa ili kuhakikisha korosho zote zinabanguliwa na sio
kuuza korosho ghafi kuongeza thamani ya zao hilo.
 

Aidha
amekitaka chuo cha elimu ya biashara CBE kubadili mtazamo wake na
kuanza kutoa elimu itakayomuwezesha mwanafunzi anapomaliza chuo kwenda
kuanzisha biashara na sio mtazamo wake wa sasa wa kuzalisha wasimamizi
wa biashara huku akitaka kishirikiane na vyuo vingine katika kuboresha
kada hiyo.
 

Kwa
upande mwingine ameitaka tume ya ushindani kufanyakazi kwa ubunifu na
si kufanyakazi kwa mazoea ili kuhakikisha inafanyakazi na wawekezaji
vizuri na sio kuwa kero kwa wawekezaji hapa nchini na hasa katika
kushughulikia mapungufu ya wawekezaji hapa nchini.

“Tume
ya ushindani msiwasumbue wenye viwanda kuna njia nyingi badala ya
kufunga biashara yake na huyo mwenye kiwanda kuona namna ya kumaliza
mapungufu hayo sio kumfungia kiwanda chake” amesema.
 

Naibu
wa Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) amewataka
watumishi katika wizara hiyo kufanya kazi kwa nidhamu na uadilifu mkubwa
na kila kiongozi katika nafasi yake ajitathmini katika utendaji wake wa
kazi kama anafaa kuwa katika nafasi aliyopo.
 

Aidha
amekemea vitendo vya uchepushaji wa fedha za miradi ambapo taasisi
nyingi zimekuwa zikitumia fedha kutekeleza miradi ambayo haikukusudiwa
tangu awali huku akizitaka taasisi zinazotekeleza miradi inayofanana
kushirikiana na sio kila taasisi inatekeleza kivyake wakati mradi ni
mmoja.
 

Kwa
upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki
Shemdoe amesema kikao hicho ni cha siku mbili kwa ajili ya kujadili
vipaumbele vya kila taasisi na bajeti yake namna ya kutekeleza ili
kuleta tija katika malengo ya kuanzisha taasisi hizo zilizochini ya
Wizara ya Viwanda na biashara.