Waziri simbachawene awasweka ndani viongozi wa kijiji, mafundi bomba ruwasa

Na Mwandishi Wetu, Kibakwe,

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amewaagiza Polisi kumkamata Mwenyekiti, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Chogola, Jimbo la Kibakwe na Mafundi  Bomba wawili wa Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani Mpwapwa kwa kosa la kuhujumu mradi wa maji wa Kijiji hicho.Mamia ya wnanchi wa Kijiji hicho ambao walikuwa na hasira ya kukosa maji kwa muda mrefu walimlalamikia Waziri huyo, wakidai maji ambayo yalikuwa yanatoka kwa wingi kijijini hapo, lakini kwasasa hayatoki kutokana na viongozi wao wa kijiji kuhujumu mradi huo wa miaka mingi.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho wa Kata ya Chogola, Waziri Simbachawene alisema viongozi hao ambao walikuwepo katika mkutano huo wanapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao pamoja kuhujumu mradi huo.

Simbachawene alisema amefanya ukaguzi wa mradi huo na kupata maelezo ya kutosha kutoka kwa wananchi, viongozi wa vijiji pamoja na Ruwasa, kuwa ‘air valve’ ya bomba kuu la maji ambayo yanasambaza Kijiji hicho imeondolewa na haijulikani ilipo na pia mabomba ya chuma yameondolewa na kuwekwa ya plastiki.

“Valve ya bomba la maji iliyokuwepo katika mradi huu ni ya mwaka 1973 ambayo mradi huo ulikamilika, lakini wananchi wanalalamika kuwa valve ya mwaka 1973 haipo imeondolwa na haijulikani ilipo, hivyo ikawekwa ya mwaka 1974 ambayo sio imara na makosa yamefanyika, tunataka hiyo valve irudi hata kama imechakaa, na ikiapatikana iwekwe katika ofisi ya kijiji na wananchi waione,” alisema Simbachawene.

Pia alisema mabomba ambayo yapo katika mradi huo yameondolewa na mafundi bila taarifa ya uongozi wa kijiji, hivyo kusababisha maji kutotoka vizuri na muda mwingine kutokuwepo kabisa.

“Polisi pia muwakamate mafundi bomba wa mradi huu, wamesababisha kuwepo kwa matatizo haya makubwa na mamia ya wananchi wanalalamika ukosefu wa maji kijijini hapa, kwanini walibadilisha mabomba haya na bila taarifa ya uongozi wa kijiji, hii sio sahihi, wanapaswa kukamatwa na kupelekwa, polisi wasakate popote walipo mafundi hao,” alisema Simbachawene.

Baada ya maagizo hayo, Simbachawene aliwataka wananchi wa Kijiji hicho wasizuie mradi huo kukarabatiwa na Ruwasa, na pia Meneja wa Mradi huo kutoka Ruwasa, Mhandisi, Cyprian Warioba hana kosa hivyo wanakijiji wamlinde wakati anaendelea kufanikisha maji yanarudi katika hali yake ya awali kijijini hapo.

“Mhandisi wa mradi huu hana kosa, mpeni ushirikiano aendelee na kazi yake, msizuie mradi huu, acheni uendelee, pia Mhandisi wa mradi nakuagiza hakikisha leo maji yanapatikana hapa kijijini, mabomba yote ya chuma yanarudi na kuyaondoa haya ya plastiki mliyoyaweka, na pia nakupa wiki tatu mradi huu ukamilike nije kuufungua hapa kijijini,” alisema Simbachawene.

Aidha, Waziri Simbachene alisema amezungumza na Waziri wa Maji ana amesema mradi huo wa maji umetengewa shilingi milioni 154, na tayari shilingi milioni 60 zilishatolewa kwa RUWASA ili mradi huo uweze kukamilika na wananchi hao wananufaika kwa kupata maji.

“Nawataka wananchi mtulie sasa, maji mtayapata kama awali, mhandisi afanye kazi yake ili kuanzia leo tupate maji, mpeni ushirikiano, ikiwezekana mpeni mke hapa kijiji, huyu ni kiongozi anatuma tu, hana kosa, makosa yapo kwa viongozi wenu, ndio kuna tatizo,” alisema Simbachawene.

Waziri Simbachawene aliwasili kijijini hapo baada ya siku moja kabla kuzuiwa na wananchi hao wakimuomba kumsaidia kupata maji ambayo yamehujumiwa na viongozi wa kijiji hao pamoja na wafanyakazi wa Ruwasa.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Cyprian Warioba, alimuhakikishia Waziri huyo maji yatapatikana Kijijini hapo kwa siku hiyo hiyo aliyoagiza, na pia maelekezo aliyoyatoa atayafanyia kazi.

Hata hivyo, baada ya ukaguzi wa mabomba hayo alibaini kuwa kuna mgogoro baina ya wananchi na viongozi wa kijiji hicho kwa kubadilisha valve pamoja na kungo’a bomba za maji hali ambayo imepelekea wakazi wa kijiji hicho kutopata maji kwa muda mrefu.

Viongozi wa vijiji waliokamatwa ni Mwenyekiti wa Kijiji, James Kisagase na Mtendaji wa Kijiji, David Msumuche pamoja na mafundi wa bomba wa Ruwasa ambao walikuwa bado wanatafutwa na polisi.

Simbachawene amemaliza ziara yake ya siku mbili katika jimbo lake ambapo alikuwa anakagua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na viongozi wa kata mbalimbali jimboni humo.

Mwisho/-