Waziri wa ardhi william lukuvi aja na muarobaini wa uchelewesha utoaji hati za ardhi nchini

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekuja na
muarobani wa ucheleweshaji utoaji hati za ardhi kuagiza Karatasi na
Majalada ya kutunzia kumbukumbu za ardhi sasa kuchapishwa Chuo cha Ardhi
Tabora sambamba na idara za ardhi katika kila halmashauri kupatiwa
vifaa  vitakavyowezesha uandaliwaji Hati za Ardhi.

Lukuvi alisema hayo leo tarehe 27 Januari 2020 wakati akifungua mafunzo
ya Utunzaji Kumbukumbu na ukusanyaji Maduhuli ya Serikali kupitia Kodi
ya Pango la Ardhi kwa Wataalamu wa sekta ya ardhi kutoka mikoa sita ya
Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida, Dodoma na Morogoro yanayoendelea
jijini Dodoma.

Alisema, pamoja na uchapishwaji Karatasi na Majalada ya utunzaji
kumbukumbu za ardhi kuanzia bajeti ijayo ya Serikali hataki kusikia
Afisa Ardhi kwenye halmashauri yoyote anatumia fedha zake za mfukoni
kununua vifaa kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.

‘’Kuanzia sasa karatasi zote tutachepa wenyewe kwenye Chuo chetu cha
Ardhi pale Tabora ili kuepuka ucheleweshaji uliokuwa ukijitokeza halafu
nije kuona halmashauri inachelewesha hati kisa karatasi’’ alisema
Lukuvi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, katika halmashauri kuna wananchi wamekamilisha
taratibu zote za kupatiwa hati za ardhi lakini wamekuwa wakicheleweshewa
jambo linalosababisha wananchi kukosa hati kwa wakati na kuikosesha
serikali mapato kupitia kodi ya pango la ardhi.

‘’Tatizo Maafisa Ardhi badala ya kushughulikia Majalada ya ardhi
wanataka mpaka wawaone Wamiliki wake, usipomuona Mpima au Afisa Mipango
Miji basi unaweza kuambiwa eneo lako ni hatarishi au la makaburi,
wanataka kula bila kunawa ’’ alisema Lukuvi.

Hata hivyo, Lukuvi alisema Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha
wananchi hawasumbuki tena kufuatilia Hati ambapo kwa aliyekamilisha
taratibu zote anatakiwa kuipata hati yake ndani ya mwezi mmoja bila
gharama yoyote isipokuwa kodi zilizopangwa kwa mujibu wa sheria.

Alibainisha kuwa, mapema mwaka huu Wizara itaanzisha ofisi za ardhi za
mikoa zitakazokuwa na wataalamu wa Upimaji, Mipango Miji, Wathamini na
Usajili na mwananchi hawatakwenda umbali mrefu kuchukua hati na hakuna
huduma ya ardhi itakayotolewa kwa kuvuka mkoa mmoja.

Pia Lukuvi amwataka maafisa ardhi kwenye Halmashauri nchini kuhakikisha
wadaiwa wote wa kodi ya pango la ardhi wanalipa malimbikizo yao ya kodi
ili kukusanya maduhuli ya serikali na kusisitiza utendaji kazi wa
Maafisa hao sasa utapimwa pia kupitia makusanyo ya kodi kwenye maeneo
yao.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, Wizara yake sasa
imejipanga kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchi
nzima na kutoa hati za kielektroni ambazo sasa zinatolewa katika
halmashauri za Ubungo na Kinondoni na kubainisha kuwa ofisi zote za
ardhi zitaunganishwa kwenye Kituo cha Taifa cha Utunzaji Kumbukumbu za
ardhi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt
Angeline Mabuala kupitia mafunzo hayo yaliyoshirikisha wataalamu 106
alisema sekta ya ardhi imekuwa ikikabiliwa na changamoto kama vile
ucheleweshaji utoaji hati za ardhi, utunzaji kumbukumbu za ardhi
usiozingatia taratibu, kutoingizwa viwanja katika mfumo na ukusanyaji
hafifu wa maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.

Alisema , hayo yote yanachangiwa na utendaji wa baadhi ya Maaafisa ardhi
wasiokuwa waaminifu pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kutozipa
kipaumbele idara za ardhi katika maeneo yao jambo linalosababisha
watumishi wa sekta hiyo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

Naye Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Wolter Lungu aliwaeleza washiriki wa mafunzo hayo kuwa makusanyo ya kodi
ya pango la ardhi yamekuwa na chanagamoto mbalimbali kama vile miamala
ya simu kugoma katika mfumo wa ukadiriaji kodi ya pango la ardhi ,
uhamishaji miliki za viwanja pamoja na utumiaji mfumo wa eneo lingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *