Waziri wa maji asitisha vibali vya ujenzi wa miradi kwa wakandarasi kwa kukosa uadilifu

Waziri
wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amesema kuanzia sasa amesitisha kutoa
vibali vya ujenzi wa miradi ya maji kwa wakandarasi kutokana na wengi
wao kuwa wadanganyifu katika makadirio ya gharama za utekelezaji wa
miradi hiyo na kuisababishia Serikali mzigo mkubwa na kukwama kwa miradi
mingi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kauli
imekuja akiwa ziarani mkoani Lindi akitembelea na kukagua ujenzi wa
miradi ya maji katika Manispaa ya Mji wa Lindi na Halmashauri ya Wilaya
ya Lindi katika kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo inaenda kwa kasi
na kukamilika kwa wakati.

Profesa
Mbarawa amesema baada ya kutembelea miradi mingi ya maji amegundua
tabia ya wakandarasi wengi wasio waadilifu kuweka gharama kubwa ili
kupata faida kubwa, na kumfanya kuchukua uamuzi wa kusitisha vibali vya
ujenzi kwa wakandarasi na kutoa kazi hizo kwa Wakala wa Usambazaji Maji
na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) pamoja na Mamlaka za Maji.

Akifafanua
kuwa maamuzi hayo yamelenga kukomesha tabia hiyo ya wizi wa fedha za
Serikali na kuokoa fedha nyingi zinazoweza kutumika katika utekelezaji
wa miradi katika maeneo mengine mengi na pia kuipa nafasi Serikali
kukamilisha ujenzi wa miradi yake kwa wakati.

Katika
hatua nyingine, Profesa Mbarawa amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya
Lindi na Mkandarasi wa Kampuni ya M/S Halem Construction Co. Ltd wakae
chini na kufikia makubaliano ya kuiacha Wizara ya Maji ifanye utaratibu
wa manunuzi ya bomba za kusambaza maji kwa ajili ya Mradi wa Maji wa
Nandambi kwa dhumuni la kuhakikisha unakamilika kwa wakati kutokana na
mkandarasi huyo kusuasua.

Profesa
Mbarawa amesema fedha za ununuzi wa mabomba hayo zipo na ndani ya wiki
mbili mabomba yatakuwa yamefika site kwa ajili ya kukamilisha mradi huo
unaotakiwa kukamilika mwishoni wa mwezi Septemba, 2019 kwa gharama ya
Shilingi milioni 825.

Aidha,
wakazi wa Kijiji cha Nandambi wamweleza Waziri wa Maji, Prof. Mbarawa
kuwa hatua hiyo itakuwa na msaada mkubwa kwao ikizingatiwa kuwa mradi
huo ulioanza utekelezaji wake Agosti, 2018 na unatakiwa kukamilika mwezi
Septemba, 2019 bado mkandarasi hatoi matumaini ya kukamilisha mradi huo
kwa asilimia 100 pamoja na ujenzi wa tenki kuwa umekamilika.

Wakati
huo huo, Kaimu Mkuu wa Mkoa ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema Serikali
ya Mkoa wa Lindi itahakikisha mazungumzo hayo yanafanyika pasipo
kupoteza muda ili hatua iliyobaki ikamilike na wananchi wa Nandambi
wanufaike na maji.