Waziri wa nishati atoa onyo kwa mameneja na wakandarasi wanaotoza wananchi gharama ya nguzo za umeme

Waziri
wa Nishati, Medard Kalemani ametoa onyo kwa mameneja na wakandarasi
wanaotoza nguzo za umeme wananchi na kuwataka waachane na tabia hiyo
mara moja kwakua serikali imegharimia nguzo hizo kwa asilimia 100.


Waziri
Kalemani ametoa kauli hiyo bungeni leo Jumatano Novemba 6, katika
kipindi cha maswali na majibu alipokuwa akijibu swali la nyongeza la
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Halima Bulembo aliyetaka kujua serikali
inazungumzia vipi kadhia ya kulipishwa nguzo za umeme ambayo wananchi wa
Mkoa wa Kagera wamekuwa wakikumbana nayo

Akijibu
hoja hiyo Waziri Kalemani amesema serikali haitaendeleakufumbia macho
suala hilo na kwamba yeyote atakaekamatwa atachukuliwa hatua za kisheria
bila kujali cheo chake.

“Yapo
maeneo bado wakandarasi na mameneja wa Tanesco wanaendelea kutoza nguzo
wateja, ninaomba nitoe tamko kali sana kwamba ni marufuku kutoza nguzo
kwa wateja wote, awe mkandarasi, Meneja wa Tanesco au kibarua na hii ni
kwasababu serikali imegharamia kwa asilimia 100,” amesema Dk. Kalemani.

Aidha
amesema serikali imekuwa ikipeleka umeme katika maeneo yote hasa
vijijini lakini baadhi ya taasisi zimekuwa hazilipiwi na hivyo amewataka
wamiliki wa taasisi hizo kuhakikisha wanalipa kiasi cha Sh 27,000 ili
taasisi zote zipelekewe umeme.