Ziara ya waziri mkuu malinyi yawatumbua mkuu wa wilaya na mkurugenzi wake


Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Magufuli ametengua uteuzi wa
Mkuu wa wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro,Majura Mateko Kasika na
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Malinyi,Mussa Elias
Mnyeti leo Jumanne Septemba 17,2019.Uteuzi wa viongozi watakaojaza nafasi hizo utajazwa baadae.
Jana Jumatatu Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa alieleza kuchukizwa na mgongano uliopo kati ya Mkuu wa Wilaya
ya Malinyi, Majura Kasika na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
wilaya hiyo Mussa Mnyeti, hivyo kumuelekeza Mdhibiti na Mkaguzi wa
Hesabu za Serikali (CAG) na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na
Utawala Bora kwenda kuchunguza weledi wa utendaji kazi wao.


“Ni aibu Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli amewateua vijana wawe
viongozi lakini leo hadi wananchi wa kawaida wanajua mgongano wenu
maofisini. Ni aibu Mkuu wa Wilaya ya Mkurugenzi mnagombana tena wakati
mwingine mnagombania miradi, mmesahau kutekeleza majukumu yenu.”


Waziri Mkuu alitoa maelekezo hayo (Jumatatu, Septemba 16, 2019) wakati
akizungumza na watumishi wa wilaya ya Malinyi pamoja na wananchi katika
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Toboa, akiwa katika siku
ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.


Alisema Serikali imewapa nafasi hiyo ili wakasimamie maendeleo ya
wananchi na inapeleka fedha kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya jamii
kama kuimarisha huduma za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara
lakini wao wanagombania miradi na mingine wanaichakachua.


Waziri Mkuu amesema mbali na CAG na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi
na Utawala Bora kwenda kuchunguza utendaji wa viongozi hao, pia
ameuelekeza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakakague miradi
ya ujenzi inayotekelezwa kwenye wilaya hiyo kama ubora wake unalingana
na thamani halisi.” Baada ya kupata majibu ya uchunguzi na kubaini kiini
cha tatizo ndani ya wilaya hii hatua zitachukuliwa.”


Awali, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Dkt. Haji Mponda alimweleza Waziri
Mkuu kwamba kwenye wilaya hiyo kuna matatizo ya mahusiano kati ya
Serikali na Halmashauri jambo linalosababisha kukwama kwa shughuli za
maendeleo.

 Mbunge huyo alisema kutoelewana kwa viongozi wa wilaya hiyo Mkuu wa
Wilaya na Mkurugenzi kumesababisha mgawanyo mkubwa kuanzia katika Baraza
la Madiwani hadi kwa wananchi mitaani, hivvyo alimuomba Waziri Mkuu
awasaidie katika. Kilipatia ufumbuzi suala hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *