Dkt abbasi ataja wasanii watakaopamba umisseta

 


Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi akizungumza kuhusiana na Mashindano ya Umiseta

 

MAUA Sama mmoja wa wasanii watakaotumbuiza katika Mashindano hayo

MSANII Chege Chigunda ambaye ni miongoni mwa Wasanii watakaotumbuiza wakati wa Ufunguzi wa MAshindano ya UMISSETA

Na John Mapepele, Mtwara

Wasanii mbalimbali wa muziki
wa kizazi kipya, wakiongozwa na Maua Sama na Chegi wanatarajia kupamba ufunguzi
wa Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA)
yatakayofunguliwa kesho Juni 21, 2021 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Mhe. Profesa Joyce Ndalichako (Mb) kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini
Mtwara.

Katibu Mkuu Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, amesema Serikali inayoongozwa
na Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza kikamilifu na inaendelea kutoa kipaombele
kwenye Sekta ya Sanaa hivyo anawaalika wadau mbalimbali kuja kushuhudia burudani
mwanana zinazoendelea kwenye mashindano haya kutoka kwa wasanii wenye vipaji wanaokuja
juu hapa nchini.

Amesema wakati wa
ufunguzi wa UMITASHUMTA wasanii mbalimbali wakiongozwa na Ibrah kutoka Konde
Gang,Beka Flavour, Peter Msechu na Linah Sanga, pia msanii maarufu wa Singeli
Dulla Makabila na Mfalme wa taarabu Mzee Yusuf, walitoa burudani ambapo amesema
katika awamu hii vikundi mbalimbali vya ngoma za asili, kwaya na Sanaa nyingine
vimealikwa ili kuongeza hamasa na kutoa burudani wakati mashindano hayo
yanaendelea.

Aidha, amesema kwenye
mashindano hayo Serikali imealika vilabu, vyama, na mashirikisho mbalimbali
kuona vipawa na vipaji vya wanamichezo hao chipukizi kutoka Tanzania Bara na
visiwani ili waweze kuwaendeza.

Dkt.Abbasi amesisitiza
kuwa mashindano haya yataendelea kutumbuizwa na wasanii mbalimbali kutoka ndani
na nje ya Mkoa wa Mtwara, ambapo burudani pia kutoka vikundi vya ngoma za
asili, kwaya na Sanaa nyingine vitaonesha umahiri wao.

“Hii ni kwa mara ya
kwanza katika historia ya nchi yetu Serikali inakuja na kitu cha tofauti kabisa
kwenye mashindano haya wasanii wametumbuiza, michezo na fani ya sanaa za ndani
zimeshiriki kikamilifu kwa mikoa yote” ameongeza Dkt. Abbasi

Ameitaja michezo
itakayoshindaniwa katika mashindano haya ni mpira wa miguu kwa wasichana na
wavulana, mpira wa miguu maalum kwa wavulana (wenye ulemavu wa kusikia) mpira
wa pete, mpira wa wavu kwa wasichana na wavulana, mpira wa mikono kwa wasichana
na wavulana, mpira wa kikapu kwa wasichana na wavulana, mpira wa meza kwa wasichana
na wavulana, riadha jumuishi, kwaya na ngoma.

Amewataka wazazi
kuondokana na fikra potofu ya kwamba michezo na sanaa ni uhuni badala yake wawahimize
Watoto kushiriki kikamilifu katika michezo kwa kuwa kiuna uhusiano mkiubwa kati
ya taaluma na michezo.

Amesema kauli mbiu ya mwaka huu ambayo inasema “Michezo, Sanaa na Taaluma kwa
Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda

inaelezea uhusiano na nafasi kubwa iliyopo ya Michezo, Sanaa na Taaluma katika
ujenzi wa uchumi wa Taifa hivyo amewataka waratibu wa kila mchezo kuzingatia
sheria na taratibu za michezo husika ili kuwapata washindi bora ili waweze kufika
mbali zaidi kwenye michezo yao.

Amemshukuru Rais Samia
Suluhu Hassan kwa kuipa michezo na sanaa kipaombele  na kuwataka waratibu  na wanamichezo wote kwenye mashindano haya
kuchukulia michezo hii kama  msingi wa mapinduzi
makubwa  kwenye  sekta hizo hivyo  kushiriki kwa weledi zaidi.

Mashindano
yameandaliwa na Wizara tatu zinazohusika na Elimu, Michezo na TAMISEMI chini ya
Kamati ya Uratibu ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu wa Wizara hizo.

Mashindano
haya yalitanguliwa na Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi
(UMITASHUMTA) yaliyofunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa Juni 8, mwaka huu mjini Mtwara na kufungwa
na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Pauline Gekul
Juni 18, 2021.Mashindano ya UMISSETA yanatarajiwa kufungwa rasmi Julai 3, mwaka
huu.