Jose mourinho amrithi mauricio pochettino baada ya kupigwa kalamu tottenham

Jose Mourinho na Mauricio Pochettino
Jose Mourinho ameteuliwa kuwa
mkufunzi mpya wa Tottenham akichukua nafasi ya Mauricio Pochettino
ambaye alifutwa kazi siku ya Jumanne.
Mourinho amepata kuwa
mkufunzi wa Man United na Chelsea hapo kabla, na tayari ametia saini
kandarasi ya kuinoa Spurs hadi mwisho wa msimu wa 2022-23. 
”Jose ni moja ya wa wakufunzi waliofanikiwa sana katika soka”, ameema mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy.
Pochettino
mwenye umri wa miaka 47 alifutwa kazi kama mkufunzi wa Spurs Jumanne
usiku baada ya kuhudumu katika klabu hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.
Katika
kipindi hicho, klabu hiyo yenye maskani yake kaskazini mwa London
ilipata mafanikio ya kutajika na kuwa moja ya timu tishio England. 
Raia
huyo wa Argentina aliiongoza Spurs kufika katika fainali ya kombe la
klabu bingwa Ulaya msimu uliopita ambapo walipoteza kwa Liverpool.
Hata hivyo msimu huu umeanza vibaya, ambapo klab hiyo imekuwa ikipata
vipigo vya mara kwa mara, ikiwemo kipigo cha 7-2 kutoka kwa Bayern
Munich mwezi uliopita. 
Spurs kwa sasa ipo katika nafasi ya 14 ya
msimamo wa ligi ya Primia wakiwa na alama 14, ikiwa ni alama tatu tu juu
ya mstari wa timu zilizo hatarini kushuka daraja. 
Pia, kumekuwa na ripoti kuhusu mkwaruzano kati ya Pochettino na mwenyekiti wa klabu hiyo Daniel Levy.
Hali hiyo, imewalazimu wakuu wa Spurs kumpiga kalamu Pochettino na kusaka usaidizi wa mkongwe Mourinho. 
Mourinho ambaye ni raia wa Ureno amekuwa bila kazi ya ukufunzi tangu alipofutwa kazi na United mnamo Disemba 2018. 
Mkufunzi
wa Bournemouth Eddie Howe, kocha wa RB Leipzig Julian Nagelsmann na
aliyekuwa kocha wa Juventus Masimilliano Allegri wote walikuwa
wakihusishwa na uhamisho wa kujiunga na Spurs, lakini wamezidiwa kete na
Mourinho.

Je, Spurs na Mourinho wataendana?

Spurs
haijawahi kumsajili mkufunzi aliye na mahitaji ya kiwango cha juu zaidi
kama Mourinho, na wala haijawahi kutumia fedha nyingi kuwanunua
wachezaji kama vile alivyozoea katika klabu za Real Madrid na Man
United. 
Hivyo basi mashabiki wengi watashangazwa kwamba huenda
akajiunga na klabu hiyo huku kocha wa RB Leipzig Julian Nagelsman
akionekana kijana zaidi na mwenye uwezo wa kuongoza klabu hiyo.
Lakini Spurs katika miaka ya hivi karibuni wametoka mbali chini ya ukufunzi wa Pochettino . 
Wana
uwanja mpya uliojengwa kwa thamani ya pauni bilioni moja na uwanja wa
mazoezi mbali na kufuzu kushiriki katika ligi ya mabingwa mara nne
mfululizo huku uuzaji wa baadhi ya wachezaji ukiwasaidia na kuifanya
klabu kuwa klabu iliojipatia faida kubwa duniani. 
Kwa sasa wana kikosi chenye talanta.
Mourinho amekuwa nje ya ukufunzi kwa takriban mwaka mmoja sasa na huku akiendelea kuishi mjini London, kazi hiyo inamfaa sana.
chanzo BBC