KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amefungiwa mechi tatu za Ligi
Kuu ya Tanzania Bara kwa kutoa shutuma na kejeli kwa Bodi ya Ligi
katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi dhidi ya Ruvu
Shooting.
Maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Bodi ya Ligi
Kuu ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake cha Septemba
2, mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Taarifa ya Kamati hiyo imesema kwamba baada ya kupitia matukio
mbalimbali ya Ligi Kuu kuftaia raundi ya kwanza ya msimu wa 2019/2020
ulioanza rasmi Agosti 24 imemchukulia hatua hiyo kocha huyo raia wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Taarifa ya Kamati imesema kwamba adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 41(9) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
Pamoja na kufungiwa mechi tatu, Zahera ametozwa faini ya Sh.
500,000 kwa kuvaa mavazi yasiyo nadhifu na ya heshima katika mechi hiyo
ambayo Yanga ilifungwa 1-0, kinyume na Kanuni ya 14(2m) ya Ligi Kuu
kuhusu Taratibu za Mchezo.
Na adhabu dhidi yake imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 41(13) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
Klabu yake nayo, Yanga imepewa Onyo Kali kwa kushindwa
kuhakikisha Kocha wake Mwinyi Zahera anaongoza benchi la ufundi la timu
yake akiwa katika mavazi nadhifu na ya heshima. Adhabu dhidi ya klabu
hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za
Mchezo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ruvu Shooting, Masau Bwire
ametozwa faini ya sh. 200,000 kwa kuingia ndani ya uwanja (eneo la
kuchezea) baada ya filimbi ya mwisho, kinyume na Kanuni ya 14(10) ya
Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu dhidi yake imetolewa kwa
kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Na Mwamuzi Msaidizi Janeth Balama amefungiwa miezi mitatu kwa
kushindwa kutafsiri sheria, hivyo kusababisha akatae bao halali
lililofungwa na Ruvu Shooting katika mechi hiyo iliyofanyika Agosti 28,
2019 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Adhabu hiyo nayo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 39(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.