Wadau wamuunga mkono rais samia michezo ya olympic

 

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo
nchini Yusuph Singo (aliyeshika mfuko) kwenye picha ya pamoja na timu ya riadha
na wafanyakazi ya Kampuni ya Ocean Silent Limited baada ya kukabidhiwa  msaada wa vyakula.   

Mkurugenzi wa Idara ya
Maendeleo ya Michezo nchini Yusuph Singo akiongea na Vyombo vya Habari
akiwataka wadau wa michezo kuendeleza vipaji vya wanamichezo kuanzia kwenye
mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA

Wanariadha wakijipanga
kwa ajili ya kushiriki mbio za mita 1500 kwenye mashindano ya UMITASHUMTA
yanayoendelea mjini Mtwara yaliyofunguliwa na Waziri mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Juni 8, 2021.

v  >Serikali
yawataka washiriki UMITASHUMTA, UMISSETA

Na John Mapepele, Mtwara

Mdau wa michezo nchini, Kampuni
ya Ocean Silent Ltd, amesema anajitolea vyakula kwa ajili ya kuisaidia timu ya
riadha katika kipindi chote kilichobaki wakati timu hiyo inapojiandaa kushiriki
mashindano ya Olympic yanayotarajiwa kufanyika mwezi Julai 2021 katika jiji la
Tokyo nchini Japan ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya Rais
Samia Suluhu katika kuinua michezo hapa nchini.

 

Mkurugenzi wa masoko wa Kampuni hiyo Bwana Muhamed
amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia inafanya kazi nzuri katika kuleta mageuzi
makubwa  kwenye Sekta ya Michezo,Sanaa na
Utamaduni hivyo ni wajibu wa kila mdau kuunga mkono ili sekta  hizo ziweze kuchangia kikamilifu katika
uchumi wa taifa.

 

Akipokea msaada vyakula
hivyo vilivyogharimu milioni 3,5 mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam kwa niaba
ya Serikali kutoka kwa Kampuni hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya
Michezo nchini Yusuph Singo amewashukuru wadau hao kwa kuiunga mkono Serikali
katika juhudi za kukuza na kuendeleza michezo nchini.

 

Mkurugenzi Singo amefafanua
kwamba kambi ya maandalizi ya wanamichezo kwa ajili ya mashindano hayo
inaendelea vizuri mkoani Arusha na timu ya wanamichezo hao inatarajiwa kuondoka
nchini Juni 29, 2021 ambapo inahusisha wanamichezo watatu ambao wamefuzu na
kufikia viwango vya mashindano hayo.

 

Amesema pia wapo wachezaji
wengine wawili ambao wamefuzu kushiriki Olympic maalum Paraolympic kwa wachezaji
wenye ulemavu watakaoshiriki mapema mwezi wa nane.

Ushiriki wa Kampuni ya Ocean
Silent Ltd katika kufanikisha kambi hiyo ni utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya
Michezo ya Mwaka 1995 ikiwa inawataka wadau kushiriki pamoja na serikali katika
kuleta maendeleo katika michezo.

Amesema mkakati wa serikali
kwa sasa ni kuhakikisha michezo kuanzia ngazi za chini hadi taifa ambapo
amesema ni kutokana na mikakati hiyo mwaka huu Mashindano ya UMITASHUMTA na
UMISSETA yanayoendelea mjini Mtwara yameratibiwa na Wizara tatu za Habari, Elimu
na TAMISEMI ili yaweze kuwa na tija kuliko awali.

Amewataka wadau kujitokeza
kuja  kuangalia vipaji vya wanafunzi
katika mashindano haya ili kwa kushirikiana na Serikali waweze kuwaendeleza.

Ameongeza kuwa kauli mbiu ya mashindano hayo ya mwaka huu inayosema “Michezo,
Sanaa na Taaluma kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda”
inasadifu kwa
kiasi kikubwa nia ya Serikali katika kuifanya michezo katika kiwango cha
kimataifa ili ichangie kwenye uchumi wa nchi.

Pia amesema wanafunzi sita watakaofanya
vizuri mashindano ya UMITASHUMTA upande wa Riadha yanayoendelea kwenye viwanja
vya Chuo cha Ualimu mjini Mtwara watapelekwa katika mashindano ya kimataifa ya
Shirikisho la Michezo ya Wanafunzi Duniani (ISSF) yatakayoanza Septemba mwaka
huu nchini Slovenia.