Yanga hoi ccm kirumba yachapwa 2-1 na pyramids ya misri kombe la shirikisho afrika

Manahodha wa timu ya Yanga na Pyramids ya nchini Misri wakiwa katika picha ya pamoja na waamuzi wa mchezo dhidi ya timu hizo kuwania nafasi ya kuingia kwenye makundi kombe la  shirikisho barani Afrika


Na.Mwaandishi Wetu,Mwanza

Timu ya Yanga imejiweka katika
mazingira magumu ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho
baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 na Pyramids FC kutoka Misri
mchezo uliopigwa katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Wageni walikuwa wa kwanza kuandika
bao kupitia kwa kiungo mshambuliaji raia wa Burkina Faso ,Eric Traory
dakika ya 42 baada ya kuachia shuti ndani ya box na kumuacha Shikalo
hana la kufanya.

Hadi  zikwenda mapumziko timu ya Kizazi kipya toka Misri ilikuwa mbele kwa kuongoza bao moja kwa bila.


Kipindi cha pili kilianza kwa timu
zote mbili kufanya mabadiliko hata hivyo wageni walinufaika na
mabadiliko hayo dakika ya 62 Nahodha wa Pyramids FC ,Abdallah  Saied
alifunga bao la pili.

Hata hivyo Yanga walipata bao la
kuvutia machozi dakika ya 88 likifungwa na Nahodha Papy Tshishimbi na
mnamo dakika ya 90 Yanga walipata pigo kwa beki wao kisiki Kelvin
Yondani kuonyeshwa kadi Nyekundu.

Kwa matokeo hayo timu Pyramids FC
imejiweka katika mazingira ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la
Shirikisho kwa mara ya kwanza wakiwa na mabao mawili ya ugenini hivyo
Yanga wanatakiwa kwenda kushinda jumla ya mabao 2-0 ili waweze kupindua
matokeo.