MADIWANI WA CCM, CHADEMA WATIFUANA ARUMERU

Na Mahmoud Ahmad, APCBLOG, ARUSHA 

MADIWANI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika Halmashauri ya Arusha Wilayani Arumeru, wameingia kwenye mtifuano wa kugombea kamati ya fedha baada ya wajumbe waliopendekezwa kuingia kwenye kamati hiyo kupingwa jambo lililosababisha kuibuka kwa mjadala mkubwa miongoni mwao.

 Hali hiyo imetokana na mapendekezo yalioletwa na Serikali yakikinzana na mapendekezo ya walio wengi ndani ya baraza hilo linalongozwa na mwenyekiti Noah Lembrise hali iliyoleta mvutano ndani ya kikao. 

Akiongea kwenye baraza hilo diwani wa viti maalum Jasmine Bachu ameliomba baraza hilo kutoa dakika tano ili warudi na mapendekezo mengine yatakayosaidia kutowagawa wajumbe ndani ya kikao hicho. 

Alisema kuwa kwa msingi huo kama hakuna anayekubaliana na mapendekezo hayo kwa kuwa wao ni wengi katika baraza hilo hivyo maamuzi sahihi sio kuwagawa wajumbe bali kujenga kamati itakayosimamia idara ya fedha. 

“Narudia kuwa hatutakubaliana na mapendekezo hayo kwani hatuwezi kukaa siku nzima kujadiliana na baadae tulete mapendekezo na yaonekane hayana maana mbele ya baraza hilo kwa kuwa kamati za vyama zipo kisheria” 

Nae Diwani wa Olmotonyi John Lengutae alisema kuwa haoni sababu ya kugombea viti na kuwataka madiwani wakubaliane na hoja iliyoletwa mezani hapo kwani waliowatuma wananchi ndio wanahitaji maendeleo na sio kugombea viti wala nafasi kwenye kamati hizo. 

Alisema kuwa kila diwani aliyepo kwenye baraza hilo anayo nafasi sawa na mwingine na hakuna aliyejuu kwani wote walipata ridhaa ya wananchi kujenga msingi ya kuwaletea maendeleo badala ya kugombea maslahi binafsi. 

“Hatujatumwa na wananchi kuja kubishana hapa kuhusu kuwepo kwenye kamati bali kuleta kero zao hivyo tuwe na makubaliano ya pamoja kwenye hilo” 

Kikao hicho ilibidi kitafute kanuni ya kusimama kwa dakika tano ili wajumbe kutoka pande mbili za CCM na Chadema kujadiliana kuhusu hoja za wajumbe wanaotakiwa kuwepo kwenye kamati mbali mbali za baraza hilo 

Mwenyekiti wa baraza hilo Noah Lembrise alisema kuwa kikao hicho kinahitaji busara zaidi kutumika ili kila moja aweze kushiriki na kuwa sehemu ya maamuzi hayo. 

Baada ya hoja za wajumbe katika kikao hicho kutofikiana muafaka, Mwenyekiti wa Kikao Diwani Noah Lembris alikiahirisha kwa muda kupisha mjadala huo ambao umeligawa baraza hilo vipende viwili baada ya baraza hilo awali kuwa chini ya chama cha demokrasia na maendeleo Chadema kwa wingi wa madiwani na sasa chama cha mapinduzi ndio kina wingi wa wajumbe. 

Akiongea kwenye baraza hilo mbunge wa viti maalum Amina Mollel alisema kuwa Hana imani na Mwenyekiti wa kikao hicho Noah Lembrise hakutendewa haki kwa kuwa hakuwa akishirikishwa kama mwakilishi na mbunge halali kwenye baraza hilo kwa kunyimwa nafasi ya kushiriki kamati ya fedha.